Kiunjuri aonya Rais asijiongeze muda

Na STEVE NJUGUNA

KIONGOZI wa chama cha The Service Party (TSP) Mwangi Kiunjuri, amesema kwamba Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake, wanafaa kuondoka mamlakani Agosti 2022.

Alisema kwamba chama chake kitaenda katika Mahakama ya Juu kutaka ushauri kuhusu mipango inayodaiwa kusukwa na serikali ya sasa ya kuongeza muhula wa Rais Kenyatta ofisini.

“Ni lazima waondoke ofisini Agosti 9 mwaka ujao, hakuna kuongeza muhula wa magavana, wabunge au Rais,” alisema.

Bw Kiunjuri alisema kwamba katika Mahakama ya Juu, chama chake kitaomba ufafanuzi kuhusu iwapo Mpango wa Maridhiano (BBI) unaweza kuwa sababu ya kuongeza muhula wa serikali iliyo mamlakani kwa wakati huu.

Alisema litakuwa jambo la busara kwa Rais kumaliza kipindi chake inavyosema katiba na kuondoka ofisini.

“Katiba iko wazi na hivi karibuni tutaelekea katika Mahakama ya Juu kutafuta ushauri kuhusiana na masuala ya kikatiba. Tutaomba Mahakama ya Juu itueleze mambo kadhaa na ushauri kuhusu iwapo BBI inaweza kuwa sababu nzuri ya kuongeza muda wa serikali hii,” alisema Bw Kiunjuri akiwa katika kijiji cha Limunga Kaunti-ndogo ya Laikipia Magharibi wakati wa mazishi ya Sophia Nyambura Kimani, mama wa diwani wa Wadi ya Marmanet, Simon Kanyutu.

Kauli yake ilijiri siku chache baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusema kuwa inakabiliwa na changamoto nyingi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

IEBC ilitaja uhaba wa pesa, muda na vizingiti vya kisheria kama changamoto kuu zinazoikabili katika juhudi zake za kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

Hasa, IEBC inasema kwamba kutotengewa pesa za kutosha kumeifanya ishindwe kuandaa mitambo yake ya kiteknolojia kwa wakati.

Bw Kiunjuri alikosoa Rais Kenyatta kwa kile alichotaja kama kutoyapa kipaumbele mambo muhimu.

“Kilicho muhimu ni kwa serikali kutoa pesa kwa wakati kwa serikali za kaunti ili magavana waweze kulipa wafanyabiashara na wakandarasi ili pesa ziingie katika mifuko yetu. Wafanyakazi wa serikali lazima walipwe kwa wakati ili waweze kulisha familia zao.

“Lakini serikali hii imewavunja moyo Wakenya, tumeona pesa zikitoka kwa IMF na wafadhili wengine lakini tunachofanya ni kujenga barabara huku watu wakikosa chakula,” aliongeza Bw Kiunjuri.

Kiongozi wa TSP alisema kwamba kuna masuala muhimu ambayo yanaendelea kuathiri vibaya Wakenya ambayo yanafaa kushughulikiwa kwa dharura.

Wanasiasa wa Mlima Kenya walia ‘kunyanyaswa’ na rais

Na JAMES MURIMI

BAADHI ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Kati wamelalamika kuwa Rais Uhuru Kenyatta anazima vyama vidogo vya kisiasa eneo hilo.

Viongozi hao wamemtaka rais kupatia vyama vya kisiasa vinavyoibuka eneo hilo nafasi ya kustawi.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri na Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Laikipia, Cate Waruguru waliungana kumtaka Rais Kenyatta kukuza demokrasia katika eneo hilo.

Wawili hao walionekana kuzika tofauti zao za kisiasa kwa kuitisha kikao cha pamoja na wanahabari, ambapo waliitaka serikali isaidie kukuza vyama vya kisiasa vyenye mizizi ya eneo hilo.

“Kama watu wa eneo la Kati ya Kenya, hatuogopi kutoa malalamishi yetu na kutetea vyama vya kisiasa tulivyo navyo. Tunamuomba Rais Kenyatta aturuhusu tujipange kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao,” alisema Bi Waruguru.

“Maeneo mengine yanafurahia demokrasia, lakini katika Mlima Kenya tumelemazwa. Tunataka demokrasia kuhusu siasa za eneo,” aliongeza.

“Iwapo demokrasia haitahakikishwa na rais, basi eneo la Kati ya Kenya litaendelea kutazama maeneo mengine yakitawala siasa za kitaifa,” alisema Bi Waruguru.

Bw Kiunjuri, ambaye ni kiongozi wa The Service Party, alisema vyama vinavyoibuka katika eneo hilo vinakadamizwa na Jubilee kwa kunyimwa haki ya kufurahia demokrasia.

JAMVI: Ishara The Service Party ndilo dau jipya la Ruto kuwania urais

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri, kuzindua chama kipya cha The Service Party (TSP) Jumatano, imeibua maswali ya ikiwa ndicho “dau mbadala” kwa Naibu Rais William Ruto kuwania urais ielekeapo 2022.

Hili linatokana na mwonekano wa nembo na rangi za chama hicho na kauli yake kuwa hatawania ugavana katika Kaunti ya Laikipia.

Na ingawa kulikuwa na matarajio kuwa mwanasiasa huyo alikuwa na mipango ya kuzindua chama cha kisiasa, wadadisi wanasema kuwa kauli yake kuhusu kutowania ugavana ama nafasi yoyote kwenye uchaguzi wa 2022 inapaswa kutathminiwa kwa kina.

Chama hicho kina rangi za manjano na nyeusi, huku alama yake ikiwa moyo, kuonyesha upendo.

Vilevile, rangi zake zinafanana na zile za chama cha United Republican Party (URP) kilichokuwa chake Dkt Ruto, kabla ya kuungana na The National Alliance (TNA) cha Rais Uhuru Kenyatta kubuni muungano wa Jubilee mnamo 2012.

Kulingana na Bw Wycliffe Muga ambaye ni mchanganuzi wa siasa, uzinduzi wa chama hicho una nia fiche, ikizingatiwa kimezinduliwa wakati masaibu ya Dkt Ruto yanaendelea kuongezeka katika Chama cha Jubilee (JP).

Bw Kiunjuri ni mmojawapo wa washirika wakuu wa karibu wa kisiasa wa Dkt Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya.

“Uzinduzi wa TSP si jambo la kawaida. Ni hatua yenye maana fiche kwa wanasiasa wanaojitayarisha kuwania urais ama uongozi wa Mlima Kenya kutoka kwa Rais Kenyatta. Bw Kiunjuri ni mwanasiasa mwenye tajriba kubwa, ikizingatiwa amekuwa siasani kwa zaidi ya miaka 15,” asema Bw Muga.

Na ijapokuwa Bw Kiunjuri hakufafanua undani kuhusu sababu kuu ya kuzinduliwa kwake, Bw Muga anaeleza kuwa huenda chama hicho kikawa “dau la kisiasa kuokoa jahazi ya Dkt Ruto ielekeapo 2022.”

Chama hicho kilizinduliwa siku moja baada ya mfanyabiashara Andrew Simiyu kuwasilisha nia ya kutaka kudumisha jina la chama cha Jubilee Asili.

Mwanzoni mwa wiki hii, Dkt Ruto alizindua kituo cha Jubilee Asili, washirika wake wa karibu kisiasa wakikitaja kama “eneo ambako watakuwa wakikutana kujadili mikakati ya Jubilee” baada ya ‘kufukuzwa’ kutoka makao makuu ya chama katika eneo la Pangani, Nairobi.

Ni hatua iliyozua midahalo kwenye majukwaa mbalimbali ya kisiasa nchini, baadhi ya wadadisi wakidai kuwa Dkt Ruto anajitayarisha kuzindua Chama cha Jubilee Asili.

Ni hilo linalotajwa kumshinikiza Bw Simiyu kwenda katika afisi za Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu kudumisha jina la chama hicho.

“Mienendo ya Dkt Ruto inafuatiliwa kwa ukaribu sana. Uwepo wa Bw Simiyu katika afisi za msajili wa vyama vya kisiasa kutaka kuhifadhi jina la Jubilee Asili unaashiria kivuli cha watu maarufu katika Jubilee, wanaodhani kuwa Dkt Ruto analenga kukitumia chama kuwania urais mnamo 2022. Hiyo huenda ikawa mojawapo ya sababu za Bw Kiunjuri kubuni TSP ‘kuwajibu’ wapinzani wa Dkt Ruto,” asema Bw Muga.

Bw Kiunjuri alifutwa kazi kama waziri na Rais Kenyatta mnamo Januari kwa madai ya kujihusisha kwenye siasa, licha ya mawaziri kuzuiwa na Katiba kujihusisha na masuala ya siasa.

Akiwa waziri, Bw Kiunjuri hakuwa akisita kuhudhuria mikutano iliyokuwa ikiandaliwa na wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ kutoka eneo la Mlima Kenya, wanaomuunga mkono Dkt Ruto.

Hajawahi kutupa marafiki

Na kwenye uzinduzi wa chama hicho, Bw Kiunjuri alisema kuwa tangu aanze siasa zake, hajawahi kuwatupa marafiki wake, ambapo si lengo lake kufanya hivyo hata baada ya kutoka serikalini.

“Urafiki ni nguzo muhimu sana kwenye siasa. Mimi ninafahamu umuhimu wa kudumisha urafiki na kuwakumbuka wenzako wanaokusaidia unapojipata pabaya,” akasema mwanasiasa huyo, bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Ni kauli ambayo wadadisi wanafasiri kuwa dalili ya wazi mwanasiasa huyo yuko tayari kumpigania Dkt Ruto kwa hali na mali, hasa kutokana na masaibu ya kisiasa ambayo yanayomkumba katika JP.

Zaidi ya hayo, hilo linaonekana kama lawama fiche kwa Rais Kenyatta kwa kuendelea kumtenga Dkt Ruto kisiasa, licha ya kumsaidia sana kushinda urais mnamo 2013 na 2017.

“Bw Kiunjuri ni mwanasiasa anayesifkika kwa kuzungumza kwa mafumbo kuwasilisha jumbe zake. Uzunduzi wa chama hicho ni mojawapo ya jumbe anazowasilisha kwa mafumbo hayo,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kumekuwa na uvumi kuwa mwanasiasa huyo huenda akawa mwaniaji-mwenza wa Dkt Ruto kwenye uchaguzi huo, ijapokuwa hajawahi kuzungumzia madai hayo hadharani.

Hii si mara yake ya kwanza kubuni chama cha kisiasa kwani mnamo 2012, alibuni chama cha The Grand National Unity (GNU) alichotumia kuwania ugavana katika Kaunti ya Laikipia mnamo 2013.

Na baada ya GNU ‘kumezwa’ na Jubilee mnamo 2017 Bw Kiunjuri anasema kuwa “hayuko tayari kurudia kosa hilo.”

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wake wanataja hatua hiyo kama “iliyochelewa.”