• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Tunisia ina kibarua kulaza Ufaransa leo Jumatano

Tunisia ina kibarua kulaza Ufaransa leo Jumatano

NA MASHIRIKA

AL RAYYAN CITY, Qatar

UFARANSA tayari wamefuzu kwa hatua ya 16-Bora, lakini leo Jumatano watakutana na Tunisia ambao ushindi utafufua matumaini yao ya kutinga katika raundi hiyo ya maondoano.

Baadhi ya mashabiki wanatarajia kocha Didier Deschamps kutumia wachezaji wengi wa akiba kutokana na sababu hiyo, lakini huenda mkongwe huyo akateremsha uwanjani kikosi kamili cha kulinda heshima ya taifa lake.

Tunisia walianza kwa sare ya 0-0 dhidi ya Denmark katika pambano lao la Kundi D, kabla ya kulazwa 1-0 na Australia katika mechi iliyofuata, na sasa wanahitaji ushindi dhidi ya mabingwa hao watetezi ili kuendelea kuwa na matumaini ya kufuzu.

Tangu mashindano haya yaanze wiki mbili zilizopita, Tunisia haijafunga bao lolote, kutokana na mchezo wao wa kuzuia, huku washambuliaji wao wakisaidia katika mfumo huo.

Kutokana na kuwa mabingwa watetezi, Ufaransa wanatarajiwa kupigania ushindi, hata kama kocha ataamua kuchezesha wachezaji wengi wa akiba.

Hata kama ataamua kuchezesha kikosi duni, nyota kadhaa akiwemo Kylian Mbappe anatarajiwa kupata nafasi kwa vile anawania tuzo ya Mfungaji Bora, lakini huenda beki wa kushoto Theo Hernandez akapumzishwa na nafasi yake kupewa Camavinga.

Katika mechi mbili zilizopita, staa huyo wa klabu ya PSG alionyesha kiwango cha juu na kuongoza kikosi chake kuibuka na ushindi wa 4-1 na 2-1 dhidi ya Australia na Denmark mtawaliwa.

Beki Lucas Hernandez aliyeumia kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Australia ni baadhi ya wachezaji muhimu watakaokosa pambano la leo, pamoja na mshambuliaji matata Karim Benzema wa Real Madrid.

Nyota huyo wa klabu ya Bayern Munich alichanika sehemu la goti lake la kulia, lakini Olivier Giroud mwenye umri wa miaka 36 anatarajiwa kuongoza mashambuliaji baada ya majuzi kufunga bao la kufikia rekodi ya Thierry Henry ya mabao 51.

Staa huyo wa zamani wa Arsenal na Chelsea alicheza mechi zote saba za Ufaransa za Kombe la Dunia wakati timu hiyo ilitwaa ubingwa nchini Urusi miaka minne iliyopita.

Kwingineko, ushindi au sare dhidi ya Denmark utaiwezesha Australia kufuzu kwa raundi ya 16 Bora.

  • Tags

You can share this post!

Maandamano: Raila akunja mkia

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uingereza sasa kuvaana na Senegal...

T L