• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
UAVYAJI MIMBA: Marie Stopes yazimwa

UAVYAJI MIMBA: Marie Stopes yazimwa

Na BERNARDINE MUTANU

Bodi ya Madaktari nchini (KMPDB) imepiga marufuku hospitali za Marie Stopes nchini kutekeleza uavyaji mimba.

Katika barua iliyoandikwa na bodi hiyo, Marie Stopes ilishutumiwa kukiuka sheria kadhaa nchini.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa KMPDB Dkt Daniel Yumbya, hatua hiyo ilitokana na malalamishi ya umma na ilichukuliwa baada ya bodi hiyo kukutana na kamati iliyokuwa ikifanya uchunguzi baada ya malalamishi hayo Novemba 7, 2018.

Mapendekezo ya kamati hiyo yaliidhinishwa na KMPDB Novemba 10, 2018 ambapo Marie Stopes iliagizwa kukomesha mara moja na kujiepusha kutekeleza uavyaji wowote wa mimba katika matawi yake yote nchini.

Uavyaji mimba nchini ni haramu ila ikiwa kina mama wamo katika hatari. KMPDB iliagiza Maria Stopes kutoa ripoti kila juma kwake katika muda wa miezi miwili (siku 60) zijazo kuhusiana na huduma zote inazotoa katika matawi yake yote.

“Marie Stopes inaagizwa kutathmini kanuni zake kuhusiana na huduma za afya ya uzazi ili kuziambatisha na sheria,” ilisema KMPDB na kuongeza kuwa kanuni mpya inazounda zinafaa kuwasilishwa kwake katika siku 60 ili kuidhinishwa.

Kulingana na bodi hiyo, hospitali hiyo imekiuka Sheria ya Matangazo (2016) kwa kupeperusha matangazo yanayopendekeza uavyaji.

Pia, Marie Stopes iliagizwa kuondoa habari ambazo bodi hiyo ilisema ni ya ‘kupotosha’ katika tovuti yake na maeneo mengine mara moja.

Tovuti ya hospitali hiyo (Kenya) haikuwa inafunguka Jumamosi lakini tovuti ya kimataifa, ambayo pia ina habari kuhusiana na Kenya ilikuwa ikifunguka.

You can share this post!

Raila aanza kazi rasmi AU, ahudhuria kikao Ethiopia

JAMVI: Kalonzo atakiwa aombe radhi waasi

adminleo