• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
UBUNIFU: Ageuza taka kuwa mbolea

UBUNIFU: Ageuza taka kuwa mbolea

NA PETER CHANGTOEK

TAKA huleta karaha mno, hususan zinapotapakaa na kusambaa kila mahali.

Hata hivyo, kwa Joyce Waithira, taka zenyewe ni mali safi; huzigeuza kuwa mbolea asilia na kuwauzia wateja.

Waithira ni mwasisi wa kampuni inayojulikana kama EcoRich Solutions, ambayo hukusanya taka na kuzigeuza kuwa mbolea asilia. Kampuni hiyo, iliyoanzishwa 2020, iko katika eneo la Kahawa, na hukusanya taka katika maeneo ya Nairobi na Kiambu.

Anadokeza kwamba aliianzisha kampuni hiyo kwa kuutumia wa Sh6,000, na imemwezesha kupokea tuzo mbalimbali.

“Nilianzisha EcoRich 2020 ili kupunguza mzigo wa taka mijini, hasa katika makao yasiyo rasmi,” asema Waithira, akiongeza kuwa, wazo la kuianzisha kampuni yenyewe lilimjia miaka minne iliyopita.

Anaeleza kwamba, ubunifu huo ulimjia baada ya kugundua kuwa kulikuwa na taka nyingi zilizokuwa zikitapakaa kila mahali.

Anasema kuwa, kwa kukusanya taka ambazo baadaye hugeuzwa kuwa mbolea, kampuni hiyo imesaidia kupunguza taka zinazotapakaa, na hivyo kusaidia kupunguza maradhi yanayohusishwa na uchafu, mathalani malaria na kipindupindu.

Wao hutengeneza mapipa ya kuweka taka na kuwapa watu ili wawe wakiweka taka, hususan za vyakula. Mapipa hayo huzifanya taka kuoza na kugeuza kuwa mbolea.

Baada ya siku kadhaa, wao hukusanya mapipa yaliyo na taka na baada ya taka zenyewe kugeuzwa kuwa mbolea asilia, huuzwa kwa wakulima kupitia kwa watu wanaofanya biashara ya kuuza pembejeo za kilimo.

Mapipa hayo hutolewa bila malipo kwa watu.

“Zaidi ya familia 550 hutumia mapipa ya kuweka taka katika maeneo ya Nairobi na Kiambu. Tunanuia kufanya kazi na familia 1,200 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na kuongeza mbolea tunazozalisha kwa asilimia 30. Hili litatuwezesha kuwafikia wakulima zaidi ya 1,400 mwishoni mwa mwaka,” asema.

Wao hutoa huduma zao katika mitaa ya mabanda kama vile Kibera, ambapo taka nyingi hutupwa mitaroni na katika mabomba ya majitaka.

Joyce Waithira na wshirika wake. PICHA | PETER CHANGTOEK

Bidhaa zao zinajulikana kwa jina EcoRich Organic Fertilizer na huuzwa kwa Sh2,500 kwa gunia la kilo 50.

“Sisi wenye huwahamasisha watu vijijini kuhusu umuhimu wa mbolea hiyo, na kuwapa mafunzo kuhusu umuhimu wa kutumia mbolea asilia,” asema Waithira, ambaye ana umri wa miaka 29.

“Asilimia 95 ya wakulima hawajawahi kutumia mbolea asilia; hivyo basi, hawajui umuhimu wa mbolea asilia, kwa hivyo tunawafunza kwanza kabla hatujawauzia,” aongeza.

Anasema kuwa, kwa sababu ya idadi ya watu inayoendelea kupanda, utupaji taka hobelahobela umekithiri, na ni muhimu watu wapewe mapipa ya kuziweka.

Ametuzwa tuzo ya Women in Agribusiness Award, tuzo zinazotolewa kwa wale wanaotumia ubunifu kutunza mazingira na kuimarisha zaraa.

“Kampuni yetu ni ya kwanza nchini kuwa na ubunifu wa kugeuza taka za chakula kuwa bidhaa iliyo na manufaa,” asema.

Waithira anaongeza kuwa, kwa sababu ya watu wengi wanaoendelea kufurika katika maeneo ya miji nchini, utupaji taka unazidi kuongezeka kila siku, na hivyo kugeuza taka kuwa bidhaa muhimu, ni njia moja ya kuhifadhi maliasili, kupunguza utumiaji wa kawi, na kupunguza athari zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya anga.

“Mipango yetu ya siku za usoni ni kuhakikisha kwamba hakuna marundo ya taka mijini, na kwamba taka zinageuzwa kuwa mbolea zitakazowasaidia wakulima kuongeza mazao yao maradufu. Tunatazamia pkusambaza mbolea kote nchini,” afichua.

Mbali na tuzo ya Women in Agribusiness Award, aliyotuzwa, Waithira pia ametuzwa tuzo ya Diar Awards 2021.

Mbuzi wala taka zilizotapakaa katika mtaa wa Highrise, California, Nairobi. Taka zaweza kugeuzwa kuwa bidhaa adhimu. PICHA | PETER CHANGTOEK

You can share this post!

Kisima cha maji ya chumvi chageuka baraka kwa jamii

Magenge ya wahalifu yaacha wakazi na makovu tele Nakuru

T L