• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Uchumi: Ahadi za Raila zakosa msingi

Uchumi: Ahadi za Raila zakosa msingi

NA PETER MBURU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga, ametoa ahadi mbali mbali katika kampeni zake za kuwania urais, ikiwemo jinsi ataboresha uchumi wa Kenya.

Baadhi ya mambo anayoahidi Wakenya ni kuhakikisha kila mtoto Mkenya anasoma kutoka chekechea hadi chuo kikuu bila malipo, kila Mkenya kupata huduma za afya bila malipo, kuwalipa watu maskini Sh6,000 kila mwezi, kuanzisha viwanda vitakavyotoa ajira kwa wengi na kuziba mianya ya ufisadi serikalini.

Akiwa Taita Taveta wiki iliyopita, Bw Odinga aliahidi kuwa akiingia serikalini atakuza uchumi wa Kenya kwa asilimia 10 kila mwaka.Ahadi hiyo, hata hivyo, haina msingi kiuchumi.

Kulingana na mashirika ya kimataifa na humu nchini, athari za Covid-19, kudidimia kwa sekta za viwanda na kilimo ambazo zimeshindwa kuzalisha ajira na bidhaa inavyofaa, kiwango cha chini cha ushuru unaookotwa na serikali na kupanda kwa mzigo wa madeni ya taifa ni masuala ambayo yataendelea kuvuta nyuma ukuaji wa uchumi kwa miaka kadhaa.

Benki ya Dunia inakadiria kuwa uchumi wa Kenya utakua kwa asilimia 4.7 mwaka huu na asilimia 5.1 mwaka ujao, Shirika la Serikali la Utafiti (Kippra) nalo linakadiria kukuwa kwa asilimia 7.1 mwaka huu na 5.4 mwaka ujao, Wizara ya Fedha 5.8 mwaka huu na afisi ya kushauri Bunge kuhusu masuala ya bajeti (PBO) asilimia 4.8 mwaka huu.

Mashirika haya yanakubaliana kuwa mzigo mkubwa wa madeni ukichanganywa na pesa chache inazookota serikali kama ushuru ni baadhi ya mambo yatakayolemaza utekelezaji wa bajeti kwa miaka kadhaa ijayo, hasa katika kupigana na umaskini, hivyo kulemaza ukuaji wa uchumi.

UKUAJI UCHUMI

Uchumi wa Kenya haujawahi kukua kwa asilimia 10 ama zaidi tangu 1972, na ndani ya miongo miwili iliyopita, wakati ulikua kwa kiwango kikubwa zaidi ilikua asilimia 8 mnamo 2010.

Katika ahadi yake vilevile, Bw Odinga alikosa kutilia maanani ukweli kuwa kiuchumi ni vigumu kukadiria jinsi hali itakavyokuwa muda unapozidi miaka mitatu au minne, ndiposa wataalamu wa kiuchumi hukadiria miaka miwili ama mitatu tu.

Pia alikosa maanani ukweli kuhusu athari za janga la Covid-19 kwa uchumi.Ili kuwavuta vijana na akina mama kumpigia kura, Bw Odinga ameendelea kuwaahidi ufadhili wa pesa za kuanzisha biashara kwa mikopo isiyo na riba, akiongeza kuwa hawatadaiwa pesa hizo hadi baada ya miaka saba, ama baada ya miradi wanayoanzisha kuanza kuwapa pesa.

Kulingana na Benki ya Dunia, kuna zaidi ya biashara 138,000 rasmi Kenya na milioni 7.4 ndogo ndogo. Kati ya hizo rasmi, ni asilimia tatu pekee zilizo na zaidi ya wafanyakazi 50 na asilimia 1 pekee zilizo na zaidi ya wafanyakazi 150.

Utafiti umeonyesha kuwa ili kuinua uchumi wa Kenya, kinachohitajika ni serikali kuongeza kiwango cha pesa inazofadhili kilimo ambacho Wakenya wengi hutegemea, kurahisisha mazingira ya utendakazi katika biashara na sekta ya uzalishaji na kuongeza viwango vya ufadhili katika sekta za elimu na afya.

USHURU WA JUU

Lakini serikali inakumbana na hali ngumu kwani haina uwezo wa kupata pesa za kutimiza mahitaji haya, kutokana na watu wachache wanaolipa ushuru, na hali kuwa kiwango kikubwa cha ushuru kinatumika kulipia mzigo mkubwa wa madeni.

Bila serikali kupunguza ushuru wa bidhaa zinazotumika katika uzalishaji viwandani, mashambani, vyakula, mafuta, kuongeza ufadhili katika utafiti wa kilimo, kulainisha sekta ya biashara ndogo ndogo kwa kuwapa wamiliki mikopo ya riba ya chini na kupanua kiwango cha walipa ushuru, nyingi za ahadi hizi haziwezi kutimizwa.

Ukweli ni kuwa Kenya imekuwa ikishuhudia uchache wa wawekezaji kutokana na vizingiti vingi katika mazingira ya biashara, kama vile kuitishwa hongo na maafisa wa serikali ili kupewa vibali vya kuanzisha biashara, ushuru mwingi unaootozwa na serikali na kupandisha gharama ya uzalishaji, pamoja na mazingira mabovu ya usimamizi wa biashara ambapo biashara zingine zinahitaji hadi leseni 40 ili kufanya kazi.

“Mimi nilikuwa Waziri Mkuu wa Kenya kwa miaka mitano, najua pale pesa ziko. Nitaziba hiyo mianya yote ambapo pesa zetu zinaibiwa na nitakuwa na pesa za kutosha kulipa watu wetu,” Bw Odinga amekuwa akisema, hasa katika ahadi ya kuzipa familia maskini Sh6,000 kila mwezi.

Bw Odinga ambaye pia anaahidi kuzidi kurudisha gharama ya stima chini endapo atachaguliwa anasahau kuwa mikataba ambayo serikali imejiingiza na kusababisha bei ya stima kupanda itadumu hadi miaka 20, na kuwa ni mojawapo ya sababu za bei ya juu ya umeme nchini.

Na japo pia aliahidi kuwa kila Mkenya atapokea huduma za afya bila malipo, hakufafanua jinsi hilo litafanyika, ikizingatiwa kuwa mpango wa UHC wa Rais Uhuru Kenyatta ambao ni sawa na anaoahidi umefeli.

Cha muhimu ni kuwa ufadhili wa kutosha katika wizara ya Afya na serikali za kaunti ndio utawezesha hilo na serikali tayari inashindwa kupata pesa hizo.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Juhudi ziwekwe kupunguza uagizaji chakula...

IEBC motoni kwa dai inaendesha ‘usajili haramu’

T L