• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Ugavana: Askofu Margaret Wanjiru sasa akubali Sakaja apeperushe bendera ya UDA Nairobi

Ugavana: Askofu Margaret Wanjiru sasa akubali Sakaja apeperushe bendera ya UDA Nairobi

NA CHARLES WASONGA

ASKOFU Margaret Wanjiru amejiondoa kutoka kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi kufuatia maelewano kati yake na seneta wa sasa wa Nairobi Johnson Sakaja.

Kulingana na maelewano hayo ambayo yalifikiwa chini ya usimamizi wa Naibu Rais William Ruto na vinara wengine wa muungano wa Kenya Kwanza, Jumamosi, Bw Sakaja ndiye sasa atapeperusha bendera ya muungano huo.

Juzi Bw Sakaja alitangaza kujiunga rasmi na chama cha United Democratic Alliance (UDA) na kuondolea dhana ya hapo awali kwamba alihamia chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Musalia Mudavadi.

Askofu Wanjiru ambaye aliwania ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2017 sasa anawania useneta kwa tikiti ya chama cha UDA kinachoongozwa na Dkt Ruto.

“Alasiri ya leo (mnamo Jumamosi) baada ya mashauriano ya kina yaliyodumu kwa majuma machache yaliyopita, tumeafikia kuwa tutamwasilisha Johnstone Sakaja kama mgombeaji wa Ugavana wa Nairobi.” Dkt Ruito akasema kwenye taarifa kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Akaongeza: “Mheshimiwa Askofu Margaret Wanjiru ameondolea mbali azma yake na sasa atawania useneta katika jiji la Nairobi. Ni kutokana na ujasiri wake ambapo tumeweza kufikia makubaliano haya.”

Hali ya vuta nikuvute imeshamiri kwa muda mrefu kati ya Bw Sakaja na Askofu Wanjiru kuhusu ni nani anafaa kupeperusha bendera ya Kenya Kwanza katika kinyang’anyiro cha Ugavana Nairobi.

Kufuatia kujiondoa kwa Askofu Wanjiru sasa ni wazi kwamba Bw Sakaja atapambana na mmoja kati ya Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi wa ODM na Fred Ngatia wa Jubilee katika uchaguzi wa Agosti 9.

Inaaminika kuwa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya utateua mmoja kati ya Wanyonyi na Ngatia kupeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro cha ugavana, Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Jimi Wanjigi amtaka Rais Kenyatta ajitetee kuhusu...

Dhehebu ‘jipya’ katili laendeleza ukeketaji wa watoto ...

T L