Kinara wa chama cha UGM, Neto aitaka IEBC isajili vijana wakazi wa Hola

Na KENYA NEWS AGENCY

KIONGOZI wa Chama cha United Green Movement (UGM) Agostino Neto ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ianzishe mchakato wa usajili wa wapigakura huku ikisalia miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa mwaka ujao.

Akizungumza mjini Hola baada ya kukutana na wanasiasa wanaopanga kukitumia chama hicho katika mwaka wa 2022, katika Kaunti ya Tana River, Bw Neto ambaye alikuwa mbunge wa zamani wa Ndhiwa, alisema IEBC inafaa ianze usajili huo na isiwaache vijana nyuma.

“Ni mwaka wa uchaguzi na vijana wengi bado hawajasajiliwa kama wapigakura, wengine nao hawana vitambulisho. IEBC inafaa iweke mikakati ya kuhakikisha usajili wa vijana kama wapigakura unaanza mara moja,” akasema Bw Neto.

Pia mwanasiasa huyo alimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ahakikishe kuwa vitambulisho vinatolewa kwa vijana kutoka kaunti za Garissa na Tana River ambao walituma maombi baada ya kutimu miaka 18.

Aidha, aliitaka IEBC pia kuwasajili Wakenya wanaoishi ng’ambo kama wapigakura.

 

Chama cha UGM chataka Uhuru atimuliwe kwa kukiuka katiba

NA WACHIRA MWANGI

KATIBU Mkuu wa chama cha United Green Movement Party (UGM) Hamissa Maalim Zaja sasa analitaka bunge lipitishe hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, baada ya korti kuamua kuwa mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ulikumbatiwa kinyume cha sheria.

Bi Zaja alisema serikali ya umoja wa nchi inafaa iundwe akisema jopo la majaji watano walioamua kesi hiyo walianika wazi kwamba Rais Kenyatta alikiuka katiba kwa kuanzisha mchakato wa BBI.

Mwanasiasa huyo alisema Rais Kenyatta aliapa kuilinda katiba na anafaa kuondoka mamlakani kwa kuidhalilisha na kutekeleza mambo kinyume na matakwa yake.

Alitoa wito kwa wabunge waanze mchakato wa kumtimua Rais mara moja ili kuitendea raia haki.

“Bunge linafaa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha afisi ya Rais haikiuki katiba. Huu ndio wakati wa kumuadhibu Rais Kenyatta ambaye anawadhulumu Wakenya na kufanya mambo bila kufuata katiba,” akasema Bi Zaja.

“Mahakama kuu ilisema Rais alikiuka katiba. Bila bunge kumtimua kutoka kwa wadhifa wake, ataendelea kupuuza maamuzi ya korti na kutumia mamlaka yake vibaya,” akaongeza.

Mwanasiasa huyo alisema BBI haikuwa na umaarufu wowote nchini na wanasiasa wakuu nchini akiwemo Rais Kenyatta ndio walikuwa wakiilazimisha raia waikumbatie.Alidai kuwa hata mabunge ya kaunti, kitaifa na seneti yalipitisha ripoti hiyo kwa hofu japo walifahamu kuwa haina manufaa yoyote ya kuchangia ukuuaji wa uchumi wa nchi.