• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
ULAGHAI: Gakuyo alivyotumia injili kuwapunja wawekezaji

ULAGHAI: Gakuyo alivyotumia injili kuwapunja wawekezaji

Na PETER MBURU

MAELFU ya Wakenya ambao waliingia kwenye mtego wa kuwekeza katika shirika la ‘Ekeza’, walivutiwa na sura ya dini aliyovaa mwanzilishi wa shirika hilo, David Kariuki Ngare.

Wengi wao walihisi kuwa hapo pesa zao zingekuwa mahali salama.

Kwa watu wengi wa jamii ya Agikuyu hasa, kila waliposikia jina la ‘mhubiri-mwekezaji’ Ngare redioni miaka kadha iliyopita, walimakinika na kutega masikio wazi kupokea ushauri wake kila siku, mwaka baada ya mwingine.

Bw Ngare alijijenga kama mhubiri-mwekezaji, katika vipindi vyake akijirejelea kama ‘Kasisi’ na mwanzilishi wa kanisa la Calvary Chosen Centre, lililoko Thika, kaunti ya Kiambu.

Mafunzo yake kwenye vyombo vya habari yalikuwa kwa ufupi, kutoa ushauri wa kimaisha na kiuchumi kwa hadhira, kurejelea Biblia kuhusu mafunzo muhimu kama heshima kwa wazazi na umuhimu wa kumheshimu Mungu.

Baadaye kabla ya kukamilisha angeeleza umuhimu wa watu kuwekeza wanapokuwa na nguvu na katika ujana wao. Hapo alizidi kutumia fursa hiyo kuiuza biashara yake ya kununua mashamba makubwa kisha kuyagawanya kuwa ploti ndogo na kuuza ili kupata faida, ya Gakuyo Real Estate.

Katika vipindi vyake alisikika kuwa mtu mwenye ulimi mtamu, maneno na mafunzo ya kuvutia kwa wazee na vijana. Baada ya muda mbinu yake ilifanya kazi kwani watu walianza kujisajili katika shirika lake la Ekeza, idadi ikipanda hadi zaidi ya watu 70,000 ambao waliamua kuwekeza.

Aliwarai watu kujiunga na shirika la ‘Ekeza’ ambapo wangechanga pesa na kwa pamoja kuweza kujinunulia mashamba kwa gharama ya chini, wawe wamiliki.

Kila mara, Bw Ngare alikuwa makini kujirejelea kuwa “naitwa Reverend David Kariuki Ngare, meneja Ekeza Sacco na mwanzilishi wa Gakuyo Real Estate,” hesabu nzuri ya kuchanganya dini na biashara ambayo ilimwendea vyema.

Fursa nyingine ya kuuza dhana yake ya dini-biashara ilikuja wakati wa kampeni za kabla ya uchaguzi wa 2017 ambapo alikuwa ameeleza nia ya kuwania kiti cha ugavana wa kaunti ya Kiambu.

Alitumia pesa kutangaza biashara zake katika vyombo vya habari na katika mikutano ya kisiasa ya chama cha Jubilee, ambapo alipata fursa ya kuhutubia watu.

Hii ilikuwa kando na mbinu nyingine aliyotumia, ambapo angewapeleka waumini sehemu fulani za mashamba yake na kuwataka kujifunga na kuomba ili wapate utajiri na afya nzuri. Ni ujumbe ambao kila mara katika ibada za Jumapili alikuwa akiurejelea, ambazo zilipeperushwa katika vituo takriban vinane vya runinga na mitandaoni.

Lakini mambo yalianza kwenda kombo mnamo 2017, miezi michache tu baada yake kujitosa katika ulingo wa siasa, ambapo aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo William Kabogo alimwaga mtama kuwa Bw Ngare alikuwa amefuja pesa za shirika hilo. Dai ambalo alilipinga vikali.

Alidai kuwa ni maadui wake wa kisiasa waliokuwa wakieneza uvumi huo.

“Mimi ni askofu wenu, sijaiba kitu, mikono yangu ni safi. Mimi ndiye meneja wa Gakuyo Real Estate na Ekeza Sacco na mkisikia uvumi mwingine ukisambaa mjue ni mpango wa kunimaliza,” Bw Ngare alisema.

Tangu wakati huo, kumekuwa na vuta nikuvute ndani ya shirika la Ekeza na kampuni ya Gakuyo, kwani wanachama waliingiwa na hofu kuhusu pesa zao.

Mambo yalizidi unga Alhamisi, wakati wakagunzi wa serikali ambao walikuwa wakichunguza sakata katika shirika hilo la Ekeza walitangaza kuwa Bw ‘Gakuyo’ alitoa zaidi ya Sh1 bilioni kutoka akaunti ya wawekezaji ya Ekeza na kuzitumia kugharamia maisha yake ya kifahari.

Wanachama walikuwa wamewekeza zaidi ya Sh2.5 bilioni.

Bw Ngare alisema hana shida na uamuzi wa serikali kunadi mali yake, mradi atahusishwa.

You can share this post!

Raila angali yafiki yangu – Namwamba

WASONGA: NCPB na HELB zianze miradi mbadala ya kujichumia...

adminleo