Mhadhiri mwenye miaka 25 anavyotetea haki za walemavu

Na DIANA MUTHEU

AKIWA na miaka 25, John Lokuta Ewoi ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM).

Licha ya ulemavu wake ambapo alizaliwa na mikono mifupi zaidi iliyo na vidole chache, Bw Lokuta amejitahidi kimasomo na kikazi ili aweze kupatana na viwango vya maisha ya kisasa katika jamii.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, Lokuta anasema kuwa mara yake ya kwanza kuingia darasani kufunza, wanafunzi walidhani alikuwa mwanafunzi mwenzao.

“Niliingia darasani na kusimama karibu na ukuta upande wa dirisha. Wanafunzi wote walipoingia darasani, nilisimama mbele na kujitambulisha kama mwalimu wao. Wengi walishangaa, lakini kadri tulipoendelea kukutana na kufunzana, waliweza kuniheshimu kama mhadhiri wao,” akasema huku akiongeza kuwa kiranja wa darasa alimsaidia kumtayarishia kompyuta yake, haswa kuitoa mfukoni na kuiweka ipate moto wa stima, na pia kuandika baadhi ya mambo muhimu ubaoni.

“Kwa mara ya kwanza mtu anaweza kunidharau kwa kuwa nina ulemavu. Lakini nikijitambulisha kwao na kusema nafanya kazi gani, huwa wanamakinika kuniskiliza,” akasema Lokuta.

Hata hivyo, Lokuta alisema kuwa safari yake katika maisha haikuwa rahisi, ikizingatiwa kuwa alizaliwa katika jamii ambayo waliamini kuwa, mama akijifungua mtoto mwenye ulemavu, ni dhahiri kuwa familia yake ilikuwa imelaaniwa.

Kijana huyu ni mzaliwa wa eneo la Baragoi, kaunti ya Samburu na ni mtoto wa nne miongoni mwa watoto nane. Yeye pekee ndiye alizaliwa na ulemavu.

“Nikiwa katika shule ya msingi, nilijihisi kuwa mtu tofauti sana, na wakati mwingi niliamua kujitenga na watoto wengine, sikucheza nao na hata sikuwa na marafiki,” alisema Lokuta.

Lokuta alihudhuria shule ya msingi ya Baragoi na mwaka wa 2009 alifanya mtihani wa kitaifa wa shule ya msingi (KCPE) na akafuzu kwa alama 351.

Licha ya ulemavu wake, alijiunga na shule ya malazi ya Maralal ambapo alisoma pamoja na wanafunzi wengine ambao hawakuwa na ulemavu wowote.

Shule hiyo ilikuwa umbali wa kilomita 105 kutoka nyumbani kwao.

“Maisha katika shule ya upili haikuwa rahisi vile. Nilipokuwa katika shule ya msingi, wazazi wangu walinifulia sare zangu, wakanipigia viatu vyangu rangi na mambo mengine ya msingi niliyohitajika kufanya. Katika shule hiyo ya bweni, wakati mwingine nililazimika kuvalia sare chafu kwa kuwa hakuna yeyote aliyenisaidia upande wa kudumisha usafi,” akasema huku akigusia baadhi ya mambo aliyoweza kujifanyia mwenyewe ni kuandika na kula.

Hata hivyo, anasema maisha yake yalibadilika alipopata marafiki.

“Walinisaidia sana. Walinifulia na kuyafanya maisha yangu rahisi pale shuleni. Mwaka wa 2013 nilifanya mtihani wa kitaifa wa shule za upili (KCSE) na nilifuzu na alama ya B+,” akasema.

Mwaka wa 2014, alijiunga na chuo kikuu cha TUM ambapo alifanya kozi kuhusu maswala ya biashara (BA), na mwaka wa 2018 alipata digrii ya kiwango cha juu zaidi (first class honours).

Chuo hicho kiliweza kugharamikia masomo yake ya shahada, ambayo anaendeleza kwa sasa na pia kumpa kazi ya uhadhiri wa masomo ya biashara.

Wakati huu ambapo shule zilikuwa zimefungwa kwa sababu ya janga la corona, amekuwa akiendeleza masomo yake mtandaoni, na pia kuwafunza wanafunzi wake kwa mtindo huo huo wa kidijitali.

“Nilipojiunga na chuo kikuu, nilijumuika na watu wengi na nikaweza kutambua kuwa pia kulikuwa na watu wengine wenye matatizo mengi kuniliko. Mazingira ya pale yalinibadili kabisa na wanafunzi wenzangu walinikubali jinsi nilivyo, na hapo nilijikubali kabisa na kujipenda zaidi,” akasema Lokuta.

Zaidi alisema kuwa aliweza kuwa jasiri sana, akajitosa katika siasa za chuo na kuchaguliwa kama Kiongozi aliyetetea maslahi ya wanafunzi wenye ulemavu.

Pia, aliweza kushiriki katika shughuli zingine za ziada chuoni na pia michezo, haswa kandanda.

“Napenda mchezo wa kandanda na kwa kawaida nambari yangu ni 10. Watu hudhani nitaumia nikiwa uwanjani lakini kipenga kinapopulizwa na nipate mpira, nitawapiga wachezaji wenzangu chenga na hata kufunga mabao kwa kutumia ujuzi wangu ambao nimekuwa nao tangu utotoni. Nikianguka, huwa naamka bila matatizo yeyote,” akasema Lokuta huku akiongeza kuwa aliweza kuunganisha vijana katika kijiji chao na wakaunda timu moja kwa jina Saint Martin FC ambayo anasema imeweza kushiriki katika mashindano kadhaa na kushinda.

Lokuta anasema kuwa unyanyapaa ndio jambo ambalo huwadhalilisha watu wenye ulemavu.

“Kuna wakati nilienda katika ofisi ya Kiongozi mmoja wa kaunti. Nikiwa mlangoni nikisubiri, nilimwona mzee mmoja amesimama. Nilipomkaribia kumuuliza kama anajua ofisi ya Kiongozi huyo, hata kabla ya kumuuliza alinijibu ‘sina kitu bro’. Nilishangaa sana kwa kuwa alidhani nilitaka kumwomba pesa,” akasema.

Bw Lokuta anasema kuwa familia yake imekuwa ikimsaidia sana na pia kanisa la Kikatoliki la parokia ya Baragoi limempa matumaini katika maisha.

“Licha ya changamoto mingi, namshukuru Mungu kwa kunipa familia inayonijali na kanisa ambalo lilisimama na mimi kwa kila jambo. Kwanza, kanisa hilo lilinisaidia kulipa sehemu ya karo ya shule ya upili na pia likanipa kazi ya ualimu katika moja ya shule ya misheni ili nipate fedha za kujikimu nikijiunga na chuo kikuu,” akasema.

Kwa upande mwingine, Lokuta anasema kuwa ana mpenzi na ana matumaini kuwa mambo yakiwa mazuri anaweza kufunga ndoa naye.

“Mara nyingi maswala ya uchumba huwa na changamoto zake, lakini tunajaribu vivo hivyo,” akasema.

Pia, alisema kuwa ana maono ya kujitosa katika siasa na hata kugombea nafasi kadhaa za uongozi baadaye.

Kijana huyu anasema kuwa walemavu bado hawajaweza kujumuishwa katika sekta zote nchini, ipasavyo.

Amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za walemavu na alipokuwa anafanya mafunzo yake katika baraza kuu la watu wenye ulemavu nchini (NCPWD) baada ya kuhitimu, aliweza kuandika makala mengi akiwasilisha kilio cha walemavu.

Anasema kuwa miradi mingi huwa inatekelezwa bila kuzingatia haki za walemavu.

“Shule nyingi za ghorofa hazina eneo la watu walemavu kutembelea haswa wale ambao hutumia viti vya magurudumu. Pia, vyoo vingi vya umma havijajengwa kumfaidi mlemavu, barabara zetu pia na magari ya umma hayakumzingatia mlemavu,” akasema Lokuta huku akiongeza kuwa miradi kama vile Kazi Mtaani vimetengewa vijana wenye uwezo pekee.

Ombi lake kwa watu watu wenye ulemavu ni wajihami na masomo na ujuzi katika sekta mbalimbali.

“Walemavu wote wajikakamue, ili kunapotokea nafasi zozote za ajira, waweze kutengewa nafasi hizo. Si kwa kuwa wanahurumiwa, lakini kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hizo,” akasema.

Wasio na uwezo kusikia kutumia maski spesheli kusoma midomo ya wazungumzaji

Na MISHI GONGO

WALEMAVU wasio na uwezo wa kusikia katika Kaunti ya Mombasa wamepokea maski spesheli kutoka kwa Muungano wa Watu Wanaoishi na Ulemavu Pwani.

Maski hizo zimeundwa kwa vitambaa maalum, lakini vyenye sehemu za kuonyesha midomo ya wazungumzaji kinyume na maski zingine zinazotumika kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Aidha, wamepewa chakula kitakachowafaa pakubwa wakati huu ambapo wakazi wanapitia wakati mgumu kutokana na athari hasi za kiuchumi kufuatia janga la Covid-19.

Bi Hamisa Zaja (kulia) na wanachama wengine wakitoa chakula kiwafae walioathirika vibaya sana kiuchumi na janga la Covid-19 Kaunti ya Mombasa Mei 21, 2020. Picha/ Mishi Gongo

Akizungumza Alhamisi katika hafla iliyofanyika Tudor, muuguzi katika hospitali kuu ya eneo la Pwani Bi Fatma Ngoto ambaye pia anashughulikia lugha ya ishara katika hospitali hiyo, aliwafuwandisha jinsi ya kutumia maski hizo na kudumisha usafi.

“Maski hizi zitawawezesha kuzungumza kati na baina yenu kwa urahisi,” akasema.

Muuguzi huyo alisema kukosa uhamasisho na mafunzo ya kutosha ni changamoto kuu katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Afisa mkuu katika muungano huo Bi Hamisa Zaja aliilaumu serikali kwa kuwaacha nyuma katika vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

“Serikali inapaswa kujumuisha watu wanaoishi na ulemavu katika vita hivi. Katika ugavi wa chakula na maski, watu wanaoishi na ulemavu wanafaa kuwekwa katika mstari wa mbele,” akasema.

Bi Hamisa Zaja (kulia) na Bi Fatma Ngoto (kati nyuma) wakipeana maski spesheli kwa wakazi wa Kaunti ya Mombasa. Picha/ Mishi Gongo

Aidha Bi Zaja aliiomba serikali kuleta maski maalum.

Alisema maski zilizoko sokoni kwa sasa haziwafai watu wanaoishi na ulemavu; hasa wasio na uwezo wa kusikia.

“Ni vigumu kutumia lugha ya ishara bila kuona midomo na maski zilizoko sokoni kwa sasa zinaficha midomo hivyo kuwanyima wasio na uwezo wa kusikia fursa ya kuzungumza,” akasema.

Wanafunzi walezea kuhusu kifaa walichovumbua kuwafaa walemavu

RICHARD MAOSI NA KATE WANDERI

Salome Njeri na Esther Amimo mwaka huu waligonga vichwa vya habari kwa kushinda tuzo ya kimataifa walipovumbua kifaa kinachoweza kuwasaidia walemavu.

Wanafunzi hao kutoka Shule ya Upili ya Keriko, Kaunti ya Nakuru walijishindia jumla ya Sh200,000 miongoni mwa zawadi nyingine.

Ni uvumbuzi wa kipekee ambao uliashiria kuwa hakuna kisichowezekana katika dunia mradi binadamu atajikakamua na kutumia mawazo yake kujifikisha kwenye hatua nyingine ya mafanikio.

Upekee wa kifaa hiki kilichoshinda tuzo ya kimataifa ni kutokana na uwezo wake, kurahisisha mambo mbali na kutumia malighafi yanayopatikana kwenye mazingira ya kawaida kama vile mbao.

Kifaa hiki kimekopa jina kutoka kwa wanafunzi waliokibuni yaani Esther na Salome kisha wakakipatia jina la ESSA (Esther/Salome)-METER.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, Salome Njeri na Esther Amimo ni mfano wa kuigwa, kwa kuongeza mawazo yao katika ulimwengu wa uvumbuzi kuwakomboa walemavu.

Wanafunzi waliovumbua kifaa hiki walipozuru Marekani kupokea tuzo la kimataifa. Picha/ Richard Maosi

Kifaa chenyewe kilipania kutatua matatizo ya watu wasiokuwa na uwezo wa kusikia na kuona.

Wanafunzi hao wanasema licha ya kuishi mashinani, juhudi zao hazikuwazuia kuingia katika vitabu vya kumbukumbu.

Kulingana na Salome anaona kuwa mbali na kutafuta elimu ya vitabuni, inawapasa wanafunzi kutalii nyanja za utafiti wakati wao wa ziada badala ya kupoteza muda wao mwingi wakitazama filamu.

Mtambo huu una kifaa kinachoweza kuwasaidia vipofu na viziwi kutatua maswala ya Hisabati hasa kupima urefu.

Salome anasema alipata hamasa ya kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo wa kusikia na kuona kutokana na mwalimu wake wa shule ya msingi ambaye hakuwa na uwezo wa kuona wala kuskia.

Licha ya mwalimu huyo kuwa na mapungufu haya alijibidiisha kufundisha somo la Kiingereza na dini kwa ustadi jambo lililowafanya wanafunzi kumpenda.

Salome aliona kuwa ipo siku angekuja kuwa mtu wa manufaa kwa watu wengine wenye mapungufu kama hayo,ndiposa akashirikiana na mwenzake kuvumbua kifaa hiki.

Kifaa chenyewe kinafanana na saa ya ukutani lakini huzimika ghafla pale mtumiaji anapofikia lengo lake.

Lango la Shule ya Upili ya Keriko, Kaunti ya Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na Salome anatarajia kuwa kifaa hiki kitatumika kote ulimwenguni kuwasaidia watu wenye matatizo kama hayo ili waweze kuwa katika nafasi nzuri ya kuendeleza taaluma zao.

Kwa mujibu wa Salome kifaa chenyewe kiligharimu shilingi 100 tu, na kuibuka bora miongoni mwa miradi mingine waliyowakilisha katika mashindano ya kuonyesha ubunifu kwa shule za upili almaarufu kama Science Contest.

“Ingawa mradi wetu ulitumia gharama ndogo cha kushangaza ni jinsi tuliibuka kuwa bora kitaifa na kuwashangaza wengi ambao hawakuwa na mawazo kama yetu,” Salome aliongezea.

Taifa Leo Dijitali ilikutana na Bi Njeri ambaye alifafanua kuhusu namna ya kutumia kifaa hiki adimu.

Alieleza kuwa walikusanya vitu vya kawaida kama vile mbao, nyaya na kalamu kutengeneza kifaa hiki ambacho hawakujua kingewafikisha Ulaya.

Mwaka wa 2017, wanafunzi hawa hawakuwa na uwezo wa kugharamia tiketi ya ndege kuwasilisha kifaa hiki katika ulingo wa kimataifa Arizona, Marekani lakini hawakufa moyo.

Mnamo 2019 walipata habari kuwa wamefanikiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi watakaopata ufadhili wa kuwasilisha ubunifu wao mbele ya kijopo cha waamuzi wa Science and Engineering Fair.

Anasema kifaa chenyewe ni rahisi kutumia kwani, hurahisisha kupima urefu, badala ya kutumia rula ambapo watu wengi wasiokuwa na uwezo wa kuona hupata matatizo kutumia rula.

Kwa wasiokuwa na uwezo wa kusikia kifaa chenyewe kina rangi tofauti ambapo kila rangi hutumika kutambulisha nambari maalum.

Salome Njeri anasema kifaa chenyewe kinafaa kuwasaidia walemavu kusoma hisabati. Picha/ Richard Maosi

Na kwa wasiokuwa na uwezo wa kuona , kifaa hiki kina sehemu mbalimbali kama vitufe ambapo mtumiaji anaweza kuvishika na kutambua nambari.

Ni kifaa rahisi ambacho kinaweza kutumia miundo mbalimbali ya rangi kurahisisha upimaji wa urefu kutokana na miundo miepesi ya aina mbalimbali ya rangi na vitufe.

Kulingana na Salome ambaye sasa ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Keriko,anasema kifaa chenyewe kinafaa kuboreshwa ili kiwafikia watumiaji wengine wengi kote ulimwenguni.

Anaona kuwa kitawafaa watumiaji endapo kitashirikisha teknolojia katika matumizi yake ili kuwapunguzia walemavu changamoto za kusoma.

Hivisasa wanalenga kushirikiana na serikali ya kitaifa, kuweka mikakati ya kufanya kifaa chao kiwe katika nafasi ya kutumia teknolojia ili kurahisisha mambo, kwani kimeunganishwa na mbao pamoja na nyaya za kawaida.

Salome anawashauri wanafunzi wenzake kujitahidi masomoni,mbali na kutumia vipaji vyao kujiendeleza kimaisha ili waje kuwa watu wa kutegemewa katika jamii siku za mbeleni.

 

UNYAMA: Mke kutoka kuzimu alivyompa mumewe upofu daima milele

Na CECIL ODONGO

KILA mwaka Kenya inapowakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi la Westgate lililotokea Septemba 21, 2013, uchungu, ukiwa na masikitiko humvaa Dan Matakaya, mzaliwa wa kijiji cha Shakunga, eneobunge la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega.

Bw Matakaya ambaye ni afisa wa polisi wa hadhi ya konstebo katika kituo cha polisi cha Industrial Area, Nairobi, milele daima hatawahi kusahau siku hiyo ya mauti si kwa Wakenya hao tu bali hata kwake yeye mwenyewe.

Kwake, tukio la kusikitisha alilowahi kukumbana nalo mikononi mwa aliyekuwa mkewe limemfanya kipofu ingawa alizaliwa mzima wa afya tena bila kasoro au tatizo lolote la kimaumbile.

Kama ada, Bw Matakaya ambaye wakati huo alikuwa afisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Kisii ya Kati mjini Kisii siku hiyo alirejea katika makazi yake kituoni humo baada ya kuwajibikia majukumu yake ya kikazi usiku kucha.

Akiwa amevamiwa na uchovu na usingizi mwingi, afisa huyo aliingia chumbani saa 11 asubuhi na kujilaza kitandani ili kupumzika huku aliyekuwa mkewe ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa sababu za kiusalama na kesi iliyoko mahakamani, akiwa anajishughulisha na usafi wa nyumba yao.

Wawili hao walikuwa wamevurugana siku iliyotangulia baada ya Bw Matakaya kumzima mkewe aliyefaa kusafiri kwao siku hiyo kutobeba nguo za marehemu mtoto wao aliyefariki miezi michache ya awali, hadi kwao.

Suala hilo siku iliyotangulia lilikuwa limezua ubishi mkali kati yao.

“Tulikuwa tumejaaliwa mtoto katika ndoa yetu changa lakini kwa masikitiko makuu akafariki miezi michache baada ya kuzaliwa kwake. Mke wangu alifaa kuenda kwao lakini sikuelewa kwa nini alitaka kupeleka nguo za mwanangu kwao. Niliwapigia simu wakwe wangu na kuwaeleza kuhusu suala hilo na wakakubaliana nami kwamba binti yao hakufaa kubeba nguo hizo ndipo nikamkataza,” Bw Mataya akasema wakati wa mahojiano katika jumba la Nation Centre, jijini Nairobi.

Akiwa amepata usingizi wa pono, mkewe, aliyekuwa na umri wa miaka 23 wakati huo na mara nyingi akionekana mnyamavu na mtulivu, alikuja kitandani akiwa amebeba kemikali ya Sulphur aliyotia ndani ya maji moto na kummwagia usoni.

“Nikiwa usingizini nilihisi maumivu makali machoni ila sikuweza kuonana hata baada ya kutapatapa kama mfa maji. Nilijizoazoa kumkabili lakini nikashindwa baada ya kukanyaga nyaya za stima alizokuwa ameunganisha kisha kuzimwagia maji sakafuni ili nichomeke,” akafafanua Bw Matakaya.

Akiwa na maumivu makali, afisa huyo ambaye pia aliwahi kudumu katika kituo cha polisi cha Etabwa mjini Embu alisimulia namna majirani walivyofika na kunusuru maisha yake baada ya kupiga ukemi akilia na kuitisha msaada.

Mkewe naye baada ya kitendo hicho aliingia mafichoni ila akaibuka baada ya siku mbili na kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi kituoni humo ambako alizuiliwa kabla ya kufikishwa katika mahakama ya Kisii kujibu mashtaka ya nia ya kuua. Aliachiliwa kwa dhamana siku chache baadaye.

Akiwa amesononeka, Bw Matakaya alisema kwamba harakati ya kupata haki imekuwa ikijikokota sana. Hii ni kutokana na mazoea ya jaji anayeshughulikia kesi hiyo kuiaihirisha kila mara bila sababu za kuridhisha.

“Kesi imekuwa ikijikokota sana tangu mwaka wa 2013 lakini nina imani kwamba ipo siku nitapata haki,” akasema Bw Matakaya akiwa ameandamana na Wycliffe Manyengo ambaye alimwajiri kama mwelekezi wake baada ya kupofuka.

Katika hali ya kushangaza, afisa huyu anasema kwamba hana kinyongo na mkewe na amemsamehe rohoni lakini hawezi kuondoa kesi kortini maana ameshauriwa kutofanya hivyo.

Anafichua kwamba amekuwa akipokea jumbe za watu kutoka familia ya mkewe wanaosikitikia hali yake na kumwomba amsamehe ila anasisitiza kwamba hawezi kurudiana naye kamwe na wao hukutana tu wakati wa vikao vya kesi wala hawajawahi kuzungumza kwa simu tangu mwaka wa 2013.

Bw Matakaya pia alituelezea kwamba tukio hilo liliathiri sana wazazi wake John Matakaya na Bilha Matakaya ambao walichukua muda sana kukubali kwamba mwanao tegemeo amekuwa kipofu bila kosa wala hatia.

Kikazi, afisa huyo aliwashukuru sana wenzake wa kituoni kwa kumpa msaada mkubwa kila mara anapowahitaji japo alisisitiza kwamba hali yake haijamzuia kutekeleza wajibu wake kama kawaida baada ya kupokea masomo ya namna ya kuwasiliana na kuandika kutumia mashine za Braille zinazotumiwa na wasioona.

“Masomo hayo yamenisadia sana kwasababu naweza kuandika, kusoma, kupiga simu na kazi nyingine za polisi baada ya simu yangu kuwekewa teknolojia ya kisasa inayonirahisishia kuandika na kuongea. Pia maafisa wenzangu na mwelekezi wangu Bw Manyengo wamekuwa wazuri sana kwangu. Kwa kweli namshukuru Mungu na namwomba awazidishie neema,” akaongeza Bw Matakaya.

Akilenga ufanisi na kuwaokoa wanaodhulumiwa, afisa huyo yuko kwenye mchakato wa kuanzisha wakfu kwa jina Dan Shieshie utakaowanusuru waume na wake wanaopitia madhila katika ndoa zao na mambo mengine mabaya yanayotokea katika jamii.

Kulingana naye, wanaume wengi huathirika sana katika ndoa zao japo huwa hawajitokezi kusema kwa hofu ya kuchekwa au kutazamwa tofauti na jamii ambayo huwachukulia kama wakuu wa familia wasiofaa kupigwa na wake.

Hata hivyo yeye amejitolea kuwasaidia kwa kuwapa ushauri na misaada mingine akitumia hela zake.

“Jambo la kweli ni kuwa ndoa nyingi zina pandashuka na wanaoumia zaidi ni wanaume wanaosalia kimya wakiwa na hofu ya kuchekwa. Nimeweka nambari yangu wazi ili waweze kuwasiliana nami kwa sababu niko tayari kuwasaidia hata kwa fedha zangu wasije wakajiua au kufanya mambo yasiyofaa baada ya kuathiriwa kisaikolojia,” akasisitiza afisa huyo.

Ili kudhihirisha matamanio yake ya kuwapa msaada wanaoathirika ndipo yaliyomkuta yasiwapate, Bw Matakaya anasomea shahada ya Ushauri Nasaha katika Chuo Kikuu cha Mlima Kenya bewa la Nairobi.

Anatumai masomo haya yatamwezesha kushughulikia kesi zitakazowasilishwa kwa wakfu wake ama zile atapokea kupitia mawasiliano ili kuwaepusha wengi kukumbana na msiba kama wake.

Pendekezo lake kwa serikali kupitia wizara ya afya ni kwamba mauzo ya wazi ya asidi au kemikali hatari yanafaa kudhibitiwa.

ERIC MALANDA: Aanzisha timu yenye makali ligini licha ya kuwa mlemavu

Na PATRICK KILAVUKA

UTU na ari ya Eric Malanda imemwezesha kuanzisha timu ya Tinganga Community FC, Kaunti ya Kiambu ambayo inatia fora ligini japo yeye mlemavu. Isitoshe, anamini kwamba wema hauozi kwa kuchochea na kukuza vipaji vya soka mtaani.

Muasisi Malanda anasema kiu ya kutandaza boli kilimsakama akiwa bado angali mdogo lakini ulemavu ukakikatiza.

Aliamua kufikiria kwa kina na kuwa na mtazamo chanya mwaka wa 2016 kuhusu kutimiza ndoto yake ya kusakata boli kisha akaamua kustawisha timu ambayo atakuwa anaitolea mawaidha na ushauri nasaha kuijenga zaidi katika ulimwengu wa kabumbu.

“Sikuwa na kosekana uwanjani haswa timu ya mtaani ya Tinganga United ilikuwa inacheza kwa minajili ya kuishabikia japo miye mlemavu. Lakini niliamini soka inaweza kuchezwa kiakili na hapo ndipo niliibua wazo la kuwa na timu,” asema muasisi huyo ambaye pia ni meneja wa timu hii ambayo ilifungua milango miaka miwili iliyotuga.

Timu hii chini ya usimamizi wake, inapigia mechi zake na kujinolea katika uga wa Tinganga/ Kamunyonge Stadium, Kiambu.

Tinganga United yaondoka uwanjani baada ya mazoezi huku kinara wao (mwenye kigari cha walemavu) akiwapa maelekezo. Picha/ Patrick Kilavuka

Ina wanasoka 30. Aliianza tu na wachezaji watano ambao aliwavua baada ya kuwaelezea nia yake ya kutosa ndaono kwao kustawisha timu na wakaitikia wito huo.

“Nilitoa hawa vijana katika uraibu wa ulevi na nikawashawishi kucheza boli kwani ninauthamini mchezo huu licha ya hali yangu. Isitoshe, niliwaambia kwamba, ningependa kuirudishia jamii mkono kupitia kukuza vipaji vya soka. Fauka ya hayo, nilipenda kuona vipawa vya soka vikitumika ipasavyo,” aeleza mraibu huyo wa soka ambaye alianza timu na wanasoka James Gatho, Brian Kameri, James Waweru, Josphat Mwangi na Robert Wahiti.

Kutokana na nia yake njema, timu inazidi kupanuka huku akiwa anasaidiana na kocha George Gitau kuwapokeza malezi ya soka wanakandanda hawa ambao wamekuwa moto wa kuotewa mbali kwani, wanahemesha timu pinzani katika ligi ya Kaunti ya Kiambu.

Eric Malanda (kati) akiwafunza vijana wake mbinu za soka. Picha/ Patrick Kilavuka

Mwaka 2017, walichomoa makucha kwenye ligi ya FKF, Kauntindogo ya Kiambu na kuibuka wa tatu bora baada ya kuzoa alama 54 miongoni mwa timu kumi na tano wakiwa nyuma ya Tinganga United (55) na mabingwa Maria FC (57) na kupewa fursa ya kuendeleza usogora wao katika ligi ya FKF, Kaunti Tawi la Aberdare.

Ni mwaka wao wa kwanza ligini lakini makali yao yamehisiwa kutokana na matokeo ya kufurahisha ambayo inayasajili katika michuano ambayo wamepepeta dhidi Maradona ambapo waliinyorosha 6-0, kuandikisha sare ya 2-2 katika mechi yao dhidi ya TCM na Destiny FC, sare zingine mbili za 1-1 dhidi ya TNT na Mwimuto Wailers Jr uwanjani Approved, Lower Kabete na hatimaye, kupoteza moja dhidi ya Nyamathombi kwa kucharazwa 2-1.

Kuifumbatia timu, uthamini wa kila mchezaji, kuweka kando ukabila na kuzingatia nidhamu kama silaha yao na mashabiki wengi kujitokeza kushabikia zaidi katika kila mechi, uvuvuo wa talanta mtaani na matokeo bora yanaonekana.

Fauka ya hayo, dukuduku ambalo lilikuwa ndani mwa wengi wakati alipokuwa anaianzisha eti hatafua dafu, liliyeyuka baada ya timu kuvuka daraja ya ligi ya Kauntindogo ya Kiambu kwa matao na kuanza kukita mizizi katika ligi ya Kaunti.

Vijana wa Tinganga United wakiwa mazoezini. Picha/ Patrick Kilavuka

Pia, wanajamii wameanza kuisaidia kuimarika zaidi.

“Changamoto ambayo nimekuwa nayo ni kwamba wanajamii mwanzoni hawakubali kwamba, ninaweza kuidumisha lakini baada ya kungangana nayo katika ligi ya Kauntindogo na kupata matokeo ya kuridhisha, wahisani katika jamii ya Tinganga wameona umaana wa timu kuwepo katika kulea vipawa vya soka na wameniunga mkono ili, ndoto ya vijana kucheza soka tamanifu itimie.

Kando na hayo kujitolea kwa wachezaji kikamilifu, kunanipa motisha ya kuwatia moyo zaidi kwa kuwekeza pato langu japo ndogo katika kuikuza timu na hivyo ndivyo tumekuwa tukiendeleza kampeni yetu katika ligi,” aeleza Malanda ambaye ni muuzaji viazi mjini Kiambu na ni shabiki sugu wa timu ya Chelsea.

Ili kuendelea kuvuta ya kamba ya timu, mwanzilishi huyo anajaribu kuongea na viongozi wa eneo hilo kuhusu kuihisani timu, lakini hajapata jibu la kuridhisha ila, angeomba wahisani kujitokeza kwa hali na mali kuisaidia kuinua vipawa.

Mipango? Ni wacheza sasa katika ligi ya Kanda ya Mkoa wa Kati mwakani na kulenga ligi kuu nchini majaliwa. Anaamini kwamba wakiwa na umoja na mshikamano wa mnato zaidi, wataweza!