• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Utekaji nyara uliozidi Mlimani wazua hofu

Utekaji nyara uliozidi Mlimani wazua hofu

Na NICHOLAS KOMU

HOFU imetanda katika Kaunti za Nyeri, Meru, Laikipia na Nyandarua kufuatia ongezeko la visa vya watu kutekwa nyara mchana katika hali ya kutatanisha na watu wenye silaha.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa watu wasiopungua 15 wametekwa nyara katika kaunti hizo ndani ya miezi minne iliyopita. Miongoni mwa waliotekwa nyara ni afisa wa ujasusi wa Shirika la Wanyamapori nchini (KWS).

Mashahidi wanasema kuwa watekaji nyara hao hujitambulisha kama polisi Wanasema watu hao huvaa sare za polisi, kubeba silaha na kuwateka nyara watu hadharani bila uwoga.

Hata hivyo, serikali imekana kabisa kuhusika na utekaji nyara huo unaoendelea.

Wakazi wa kaunti zilizoathiriwa wamebaki ‘gizani’ huku baadhi yao wakiishi katika hofu.

Japo utekaji nyara ulifanyika katika kaunti nne, baadhi ya walioathirika wanatoka katika eneo la Solio na Naromoru linalopakana na Solio Ranch, makazi ya wanyamapori.

John Mwiti, mkulima katika eneo la Kihato, Kaunti ya Laikipia, ndiye aliyekuwa wa kwanza kutekwa nyara mnamo Juni 26, 2021.

Bw Mwiti alikuwa shambani mwake alipokabiliwa na mwanaume mmoja aliyetambuliwa kama polisi. Aliingizwa katika gari na kupelekwa kusikojulikana.

“Nilikuja kugundua jioni kuwa mume wangu alitekwa nyara. Tangu hiyo siku, sijawahi kuzungumza naye wala kujua alipo,” akasema Damaris Wanjugu, mke wa mwathiriwa.

Siku moja baada ya Bw Mwiti kutekwa nyara, Isaac Mwangi na mfanyakazi wake Wilson Mwangi walitekwa nyara.

Bw Isaac alitekwa nyara akiwa na mkewe na mwana wao katika eneo la Kianugu.

Elijah Karimi alikuwa mwathiriwa wa nne kutekwa nyara. Alitekwa nyara mnamo Juni 28 katika mji wa Naromoru.Uchunguzi ulibaini kuwa kati ya tarehe Juni 30 na Agosti 28, Samuel Ngacha, Bernard Wanjohi, Peterson Mutwiri, Peter Mugweru, Patrick Maina na afisa wa KWS, Francis Isaack Oyaro walitekwa nyara kwa njia sawa.

  • Tags

You can share this post!

Mvita yawaniwa vikali Nassir akijiondoa

Watoto wa marais wakwama na Raila