• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Uwekezaji: Kenya yapakwa tope na ripoti ya IMF

Uwekezaji: Kenya yapakwa tope na ripoti ya IMF

NA WINNIE ONYANDO

SHIRIKA la Fedha la Kimataifa (IMF) limeorodhesha Kenya kuwa nchi ya pili mbaya zaidi duniani kuwekeza hasa kibiashara, kutokana na joto la kisiasa.

Ripoti hiyo inasema kuwa mazingira ya Kenya hasa katika kipindi cha uchaguzi yanaifanya kuwa vigumu zaidi kwa wawekezaji, wanaotaka kuweka mabilioni ya pesa zao katika miradi mbalimbali nchini.

Katika ripoti hiyo, nchi ya Colombia ndiyo iliyofanya vibaya zaidi kuliko Kenya, katika tathmini ya miezi ya Aprili na Juni.

Ripoti hiyo pia inabainisha kuwa wawekezaji wanahofia kupoteza mabilioni nchini kutokana na kupanda kwa joto la kisiasa kati ya wawaniaji wa urais.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa wasiwasi wa wawekezaji nchini umeongezeka kwa asilimia 84 huku uchaguzi wa Agosti ukikaribia.

Hali hiyo inawafanya wawekezaji wengi kusitisha mipango ya kuwekeza nchini kwa hofu kuwa huenda wakapoteza pesa zao.

IMF iliunda kundi la kukagua athari za kisiasa kwa wawekezaji (WUI) ili kukagua usalama wakati wa uchaguzi katika nchi 143 ambazo zinawakilisha asilimia 99 ya Pato la Dunia (GDP).

Nchini Kenya, IMF imeainisha uchaguzi kuwa mojawapo ya vyanzo vikuu vya vinavyowafanya wawekezaji kuhofia kuwekeza.

Hii ni baada ya vurugu kutokea nchini baada ya uchaguzi wa 2007.

Kura za maoni zinaonyesha ushindani mkali kati ya wawaniaji wawili wa kiti cha urais, Raila Odinga na Naibu wa Rais, William Ruto.

Kura hizo zinaonyesha kuwa ikiwa uchaguzi ungefanyika leo, hakuna mmoja kati yao ambaye angepata asilimia 50 ya kura.

Kutokana na hayo, wawekezaji sasa wanasubiri kuona ikiwa uchaguzi utakuwa wa amani ndipo waweze kuwekeza nchini.

Kwa upande mwingine, janga la corona pia limetajwa kuwa miongoni mwa sababu ambazo ziliwafanya wawekezaji kusitisha mipango yao ya kuwekeza nchini.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Patrick Njoroge, hata hivyo, katika mahojiano mwaka 2021, alisema ongezeko la joto la kisiasa kufuatia kura za maoni kuhusu uchaguzi wa Agosti 9, huenda likawafanya wawekezaji kuhofia zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Pigo baada ya Chebukati kukataa orodha ya wabunge, maseneta...

Serikali yazimwa kutwaa ardhi ya KU

T L