• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Virusi vya corona vinavyohangaisha India vilizuka kitambo Uingereza – utafiti

Virusi vya corona vinavyohangaisha India vilizuka kitambo Uingereza – utafiti

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

AINA ya virusi vya corona vinavyohangaisha vibaya raia wa India huenda vilizuka kitambo nchini Uingereza na vimekuwa vikibadilika “pakubwa” tangu Machi.

Onyo hili lilitolewa Jumamosi, Mei 22, na wataalam wakuu wa kisayansi wanaotoa ushauri kwa serikali nchini humo.

Virusi hivyo aina ya B.1.617.2 vyenye athari kali huenda vilijumuisha sehemu “kubwa” ya maambukizi nchini Uingereza kufikia katikati mwa Mei.

Hii ni kwa mujibu wa nakala zilizochapishwa na Kundi la Kutoa Ushauri wa Kisayansi kuhusu matukio ya Dharura nchini humo.

Kundi hilo la wanasayansi lilitafiti kuhusu kusambaa kwa aina hiyo ya virusi mnamo Mei 12, kwa kuzingatia jinsi vilivyosambaa Aprili.

Wataalam hao walitabiri kuwa huenda virusi hivyo vilichangia nusu (asilimia 50) ya maambukizi yote katika taifa la Uingereza kufikia katikati mwa Mei.

Matokeo ya utafiti huo yanapendekeza kuwa idadi rasmi ya visa vilivyoripotiwa na idara inayoshughulikia Afya ya Umma Uingereza, ni ya chini kushinda idadi halisi.

Utafiti huo ulieleza kuwa aina hiyo ya virusi inachukua haraka nafasi ya aina iliyokuwepo awali ya Kent, iliyosababisha kuzuka kwa wimbi la pili la mkurupuko.

Ripoti zilizochapishwa na kuwasilishwa kwa baraza la mawaziri nchini humo mnamo Mei 11, zilionya kuwa aina hiyo hatari ya virusi vinavyotafuna India, ambavyo tayari vinaenea katika miji ya Bolton, Bedford na Sefton, “vinaongezeka kwa kasi.”

Kundi hilo lilihimiza kuwepo mchakato wa kuwapima watu wasioonyesha dalili za virusi hivyo, kuwafuatilia waliotangamana na wahasiriwa na kuwatenga wagonjwa katika maeneo yenye visa vingi vya maambukizi.

Lilidokeza pia kuhusu kuongeza muda wa kufunga nchi hiyo, likionya serikali dhidi ya kusubiri ushahidi zaidi kabla ya kuchukua hatua.

Matabibu hao tayari wameanzisha shughuli ya kuwapima raia katika maeneo kadhaa ambapo aina hiyo hatari ya virusi inasambaa kwa kasi zaidi ikiwemo Bolton na Blackburn.

“Wakati huu ambapo tuna ushahidi ambao bado haujathibitishwa, madhara ya kuchukua hatua kali ni finyu ikilinganishwa na manufaa tunayoweza kupata kwa kuchelewesha wimbi la tatu la mkurupuko hadi watu zaidi watakapopatiwa chanjo,” inasema ripoti ya wanasayansi hao wakisisitiza hatari ya virusi hivyo.

  • Tags

You can share this post!

Maelfu walazimika kuondoka katika makazi yao kufuatia...

NANI ATALIPA HAWA WAZITO?