• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:37 PM
Wanafunzi 110 walazimika kurudi nyumbani baada ya kukosa nafasi shuleni Mukuru

Wanafunzi 110 walazimika kurudi nyumbani baada ya kukosa nafasi shuleni Mukuru

Na SAMMY KIMATU

ZAIDI ya watoto 100 wamelazimika kurudi nyumbani baada ya kukosa nafasi kujiunga na shule ya msingi ya Sancta Maria Mukuru katika wadi ya Landi Mawe, Kaunti ya Nairobi.

Akiongea Jumatatu, chifu wa eneo hilo, Bw Richard Kikuvi amethibitisha watoto 110 wamekosa nafasi baada ya madarasa ya shule hiyo kujaa kupita kiasi.

Bw Kikuvi alikuwa ameambatana na naibu wake, Bi Christine Litswa kukagua ikiwa shule zinatimiza kanuni zilizowekwa na serikali kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Bw Kikuvi ameongeza kuwa wanafunzi watano katika shule hiyo ni wajawazito.

“Licha ya kuwa na ujauzito, wasichana wanne wanasoma ilhali msichana wa tano haji shuleni,’’ Bw Kikuvi akasema.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi Reginah Nzomo amesema wanafunzi 1,130 kati ya 1,790 wameripoti shuleni Jumatatu na kuongeza kwamba wazazi wa wanafunzi waliokosa kuripoti wameomba ruhusa ya wana wao kuchelewa kutokana na changamoto mbalimbali.

“Baadhi ya wazazi waliopiga simu walisema wamechelewa maeneo ya mashambani kufuatia changamoto za usafiri,’’ Bi Nzomo akasema.

Bi Nzomo ameongeza kwamba kila darasa katika shule hiyo lina wanafunzi 92, idadi iliyo kinyume na matakwa ya wizara ya afya na elimu kufuatia janga la corona.

Aidha, Bi Nzomo amesema shule yake ina upungufu wa walimu sawia na upungufu wa ardhi ya kujenga madarasa zaidi.

Vile vile, amesema shule hiyo hutegemea misaada kutoka kwa wahisani ili kujikimu.

“Tuna walimu 24 kwa sasa huku mwalimu mmoja akiwa likizoni na mwingine akipata uhamisho,’’ akasema.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Bw Peter Okari alisema kuna hitaji kubwa ya barakoa za wanafunzi kutokana na umaskini mwingi uliokithiri kwa jamii ya Mukuru. ‘’Hii ndio shule ya pekee ya umma katika mitaa ya mabanda inayozunguka hapa Mukuru. Tunahitaji hema za madarasa ya ziada, ’’Bw Okari akanena. Mapema mwezi jana, shule ilipokea msaada wa dawati 70 kutoka kawa wizara ya elimu na zingine 159 kutoka kwa mbunge wa eneo hilo, Bw Charles Njagua Kanyi.

“Mnamo Desemba 2020, tulipokea msaada wa madawati 70 kutoka kwa Wizara ya Elimu na mengine 150 kutoka kwa mbunge wa Starehe, Bw Chrales Njagua Kanyi,’’ Bi Nzomo akaambia waandishi wa habari.

Kadhalika, Bw Okari aliongeza kwamba darasa la nne na la saba ndiyo madarasa yaliyo na idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganishwa na darasa zingine zote kwenye shule hiyo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wizara ifuatilie ili pesa zisichelewe

ODONGO: Wetang’ula atumie Matungu na Kabuchai...