• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
Zesco United yanyanyua taji la Ligi Kuu Zambia

Zesco United yanyanyua taji la Ligi Kuu Zambia

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Jesse Were alifunga bao lake la 101 na kusaidia Zesco United kuchapa NAPSA Stars 2-0 na kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Zambia uwanjani Levy Mwanawasa, Ndola.

Zesco, ambao pia wameingia Klabu Bingwa Afrika ya msimu 2021-2022, wamefungua mwanya wa alama 11 juu ya ligi hiyo ya timu 18 baada ya kuzoa alama 64 kutokana na michuano 31. Pia, wana mechi tatu mkononi.

Mshambuliaji huyo Mkenya aliyejiunga na Zesco mwezi Januari 2016 akitokea Tusker FC, alimwaga kipa Shaaban Odhoji dakika ya 39.

Odhoji, ambaye pia ni Mkenya, alikuwa amezima Were dakika ya nane na 25, Samuel Sikaonga dakika ya tisa, Winstone Kalengo dakika ya 31 pamoja na Thabani Kamusoko kugonga mwamba, kabla ya Were kucheka na nyavu.

Were alipoteza nafasi nyingine nzuri sekunde chache kabla ya kipindi cha kwanza kukatika baada ya Odhoji kupangua shuti lake.

Odhoji aliokoa makombora mawli kutoka kwa Kelvin Kampamba mapema katika kipindi cha pili kabla ya mchezaji huyo kufanikiwa kutikisa nyavu dakika ya 80.

Wapinzani wa karibu wa Zesco ni Zanaco ambao wamevuna alama 53 kutokana na mechi 31. Hawawezi kufikia Zesco.

Huku Zesco, ambayo pia imeajiri kipa Ian Otieno na mshambuliaji John Makwata kutoka Kenya ikisherehekea taji ililopoteza kwa Nkana msimu uliopita, NAPSA inakodolea macho kutemwa.

NAPSA, ambayo pia beki Mkenya David ‘Calabar’ Owino anachezea, inashikilia nafasi ya 16 kwa alama 36 kutokana na mechi 32. Imedondosha alama zote katika mechi sita zilizopita.

Nkana, ambayo pia ina kiungo mshambuliaji Duke Abuya kutoka Kenya, inaning’inia pabaya katika nafasi ya 15 kwa alama 37 baada ya kujibwaga uwanjani mara 31. Timu zitakazokamilisha ligi hiyo kutoka nafasi ya 15 hadi 18 zitashushwa ngazi.

You can share this post!

Nafula atinga bao AE Larissa ikishinda shaba kwenye Ligi...

Kepa Arrizabalaga kati ya wanasoka sita wa akiba...