Taita Taveta huru kutoza kodi miji inayozozania na Kaunti ya Makueni

Taita Taveta huru kutoza kodi miji inayozozania na Kaunti ya Makueni

Na PHILIP MUYANGA

WAFANYABIASHARA mjini Mackinon Road na Mtito Andei sasa watahitajika kulipia ada zao za kibiashara kwa Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta kwa muda.

Hii ni baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi iliyo Mombasa kutoa uamuzi wa muda kwamba kaunti hiyo pekee ndiyo iwe ikitoa vibali vya biashara na kutoza kodi katika miji hiyo miwili jinsi ilivyokuwa ikifanywa na baraza la mji wa Taita Taveta kabla serikali za kaunti zilipobuniwa.

Kumekuwa na mzozo kwa muda mrefu kati ya kaunti hiyo na zile za Kwale na Makueni kuhusu maeneo ya mipaka ya miji hiyo miwili.

Kaunti ya Kwale hudai kumiliki Mackinon Road huku Makueni ikidai kumiliki Mtito Andei, ilhali Taita Taveta inasisitiza miji hiyo miwili ni yake.

Kando na agizo hilo, Jaji Lucas Naikuni pia aliagiza Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta kuweka pesa zote zitakazokusanywa katika akaunti ya benki itakayozaa riba, ambayo itafunguliwa kwa pamoja na Kaunti za Kwale na Makueni.

Agizo hilo lilitolewa baada ya mwanaharakati Okiya Omtatah kuwasilisha kesi mahakamani akitaka bunge la kitaifa na seneti kuagizwa kuunda tume huru ya kutatua mzozo huo.

Jaji Naikuni alisema agizo litadumu hadi Oktoba 27, wakati ambapo kesi inatarajiwa kusikilizwa.Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani, wafanyabiashara waliokuwa wakilipa kodi kwa baraza la mji wa Taita Taveta kabla serikali za kaunti kubuniwa, wamekuwa wakilazimika kulipa kodi mara mbili kwa kaunti mbili.

“Wafanyabiashara hawajui wanafaa kuitisha wapi huduma au uwajibikaji wa pesa wanazotozwa,” sehemu ya stakabadhi hizo inasema.

Bw Omtatah alisema alipokea barua kutoka kwa wakazi wa Taita Taveta wakimwomba aingilie kati ili kuwasaidia kupata suluhisho kuhusu mzozo wa mipaka kati ya kaunti hizo tatu, ambao umekuwepo tangu kabla nchi ilipopata uhuru.

Alisema kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya mipaka iliyoandaliwa mwaka wa 2015 na kamati iliyobuniwa na Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta, hakuna minara ya kuonyesha mipaka kati ya Taita Taveta na Kaunti za Kwale na Makueni.

“Mzozo huu hauhusu tu mipaka ya Kaunti ya Taita Taveta, bali pia unahusu madai kuwa mipaka ya kaunti iliyopo kwa sasa si ya haki kwa vile iliekwa kwa misingi ya dhuluma za haki za kihistoria,” akadai Bw Omtatah.

Zaidi ya hayo, alieleza kuwa mzozo unahusu ni nani anayestahili kukusanya kodi katika miji hiyo iliyo na biashara nyingi.

“Bunge halijapitisha sheria ambayo itatatua mizozo kuhusu mipaka ya kaunti mbalimbali ilhali ni lazima kuwe na sheria ya kutekeleza Ibara 118 ya Katiba ili kutatua masuala haya kikamilifu,” akasema.

Bw Omtatah anataka pia serikali kuu iagizwe kufanya usoroveya na kuweka minara inayoonekana vizuri katika mipaka ya kaunti zote nchini, kukiwa na kipaumbele kwa Taita Taveta, Kwale na Makueni.

You can share this post!

TAHARIRI: Sekta ya elimu yahitaji mageuzi

Safaricom ilichangia Sh557 bilioni kwa pato la taifa...