Habari Mseto

Taita Taveta katika ushindi wa mapema kwenye mvutano na kaunti mbili

February 19th, 2024 2 min read

NA PHILIP MUYANGA

SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta, sasa itaendelea kukusanya kodi za kibiashara katika miji ya Mackinon Road na Mtito Andei inayozozaniwa na kaunti nyingine mbili, hadi kesi kuhusu mzozo huo itakapokamilika.

Jaji Lucas Naikuni wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi alithibitisha maagizo yanayoruhusu Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta kuwa mamlaka pekee inayotoa vibali vya biashara na kutoza kodi katika miji hiyo.

Aliagiza kuwa, Serikali ya Taita Taveta itaweka mapato yote itayokusanya katika akaunti ya benki ya kupata riba iliyofunguliwa kwa pamoja na Serikali za Kaunti za Kwale na Makueni.

Jaji huyo pia alitoa agizo la kupiga marufuku Kwale na Makueni na maajenti wao kukusanya kodi kwa vyovyote vile katika miji ya Mackinon na Mtito Andei ambapo watangulizi wao hawakukusanya mapato kabla ya kuanzishwa kwa serikali za kaunti.

Maagizo hayo yalitolewa kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa ombi lililowasilishwa na Seneta Okiya Omtatah kuhusiana na mizozo ya mipaka kati ya Kaunti za Taita Taveta, Kwale na Makueni.

Bw Omtatah analenga kulishurutisha Bunge la Kitaifa na Seneti kuteua tume huru ya kutatua mizozo inayoendelea ya mipaka kati ya kaunti hizo tatu.

Katika uamuzi wake, Jaji Naikuni alibainisha kuwa, ni wazi kwamba kesi hiyo ilikuwa ya manufaa makubwa kwa umma inayohusu mizozo ya mipaka inayoathiri kaunti tatu, ukusanyaji wa ushuru na dhuluma za kihistoria.

Aidha, alisema uamuzi huo wa mahakama hausubiriwi tu na wakazi wa kaunti hizo tatu, bali pia nchi nzima ambapo masuala sawa na hayo yameenea na kusababisha hali ya taharuki kwingineko.

“Mlalamishi amefungua kesi ya msingi, itakuwa si haki kwa wakazi wa Mackinon na Mtito Andei kwa mahakama hii kukunja mikono. Maombi yanayoombwa ni kuhakikisha kaunti moja inatoza na kukusanya mapato na amana kwa faida ya pamoja,” alisema Jaji Naikuni.

Kaunti za Kwale na Makueni zilipinga kupitishwa kwa maagizo hayo zikisema kwamba ombi hilo lilikosa umuhimu kwa kukosa kuanzisha kesi ya msingi.

Jaji Naikuni pia aliruhusu ombi la kutaka kuongezwa kwa muda kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi ambayo mahakama iliamuru kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti kuhusu mzozo wa mipaka kati ya kaunti hizo tatu.

“Muda wa kutekelezwa kwa maagizo yaliyotolewa mahakamani Machi 23, 2022 kwa NLC utaongezwa kutoka Desemba 31, 2023 hadi Aprili 15, 2024,” sehemu ya amri hiyo inasema.

Kulingana na stakabadhi hizo, mizozo hiyo imesababisha wafanyabiashara waliokuwa wakilipia kodi kwa mamlaka yaliyotangulia Kaunti ya Taita Taveta, kabla ya kaunti kuanzishwa, kulazimika kulipa ushuru mara mbili kwa kaunti mbili tofauti. Kesi hiyo itatajwa Aprili 22.