Habari za Kaunti

Taita Taveta yalia miradi ya serikali kuu kukwama

March 17th, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA

UJENZI wa barabara ya Mto Mwagodi-Msau-Mbale-Werugha-Mgange-Bura ya kilomita 54 umekoma, licha ya serikali kuhakikishia wakazi na viongozi wa Taita Taveta kuwa mradi huo utaendelea.

Miezi kadhaa imepita tangu mradi huo usimame, na kuacha barabara hiyo ikiwa haijakamilika.

Hilo ni licha ya ahadi za kuifufua tena, maendeleo yaliyoanzishwa na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, kwa sasa akiwa mstaafu, yakionekana kukwama.

Jambo hilo aidha linazua maswali kuhusu kuchelewa kwa maendeleo ya miundomsingi yanayotekelezwa na serikali ya kitaifa eneo hilo.

Ujenzi wa barabara hiyo inayokadiria kugharimu karibu Sh2 bilioni unatekelezwa na Kampuni ya Stecol ambayo kwa sasa imesimamisha shughuli zake.

Mradi huo ulizinduliwa Novemba 2021 na ujenzi wake ulitarajiwa kuanza mara moja na ukipaniwa kukamilika Septemba mwaka huu, 2024.

Hata hivyo, changamoto mbalimbali zimekuwa zikikwamisha ujenzi wake haswa kutokana na ukosefu wa fedha kutoka serikalini.

Mwanzoni mwa 2023, serikali ililipa Stecol Sh98 milioni dhidi ya malipo ya awali ya Sh208 milioni yaliyotakiwa kufanywa.

Aidha, Wizara ya Barabara ilitangaza kuwa ilitenga Sh89 milioni ili kulipa kiasi kilichosalia.

Licha ya kulipwa kwa fedha hizo, mradi huo umekuwa ukikwama na mkandarasi ameondoka tena katika eneo la kazi.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita, viongozi kutoka Kaunti ya Taita Taveta wakiongozwa na Gavana Andrew Mwadime walikutana na Waziri wa Barabara, Bw Kipchumba Murkomen ambapo waliiomba serikali ya kitaifa kuharakisha mradi huo.

Mbunge wa Wundanyi Bw Danson Mwashako alisema kuwa mkandarasi anadai serikali kima cha Sh333 milioni.

“Malipo ya awali ya hatua ya kwanza ya kilomita 5.5 ya lami yalifanyika,” alisema.

Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa kuchelewa kwa muda mrefu kwa ujenzi wa barabara hiyo kumeathiri pakubwa usafirishaji wa bidhaa za mashambani na vilevile maendeleo ya kiuchumi ya maeneo hayo.

Barabara hiyo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya serikali ya kitaifa katika eneo hilo na ni mpango muhimu wa maendeleo ya miundomsingi ili kuboresha usafiri na kukuza uchumi wa eneo hilo.

Wakulima, wafanyabiashara, na wanajamii hushindwa kusafirisha bidhaa na mazao yao sokoni wakati wa msimu wa mvua na kusababisha ongezeko la gharama na hasara za kiuchumi.

Mara tu itakapokamilika, barabara hiyo itapunguza matatizo ya usafiri kwa wenyeji kwa kurahisisha usafiri, uchukuzi wa bidhaa, na huduma katika maeneo ya Mwatate na Wundanyi.

Inatarajiwa kufungua fursa za biashara na uwekezaji, kuendesha ukuaji wa uchumi wa ndani, na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, elimu, na huduma nyingine muhimu kwa wakazi.

“Tunaomba serikali kuharakisha mradi huu kwa kuwa kwa miaka mingi tumepata hasara kutokana na barabara kutopitika,” alisema mkulima wa Mghange Cosmas Kaligha.

Wakati wa ziara zake katika kaunti hiyo, Rais William Ruto alihakikishia wenyeji kuwa mradi huo utaendelea na utaharakishwa hadi kukamilika.