Habari za Kaunti

Taka zafunga barabara Murang’a, panya wakionekana waziwazi

May 1st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

UTUPAJI taka kiholela katika Kaunti ya Murang’a umezidi, katika visa vingine barabara za mjini zikigeuzwa dampo.

Barabara zimegeuka za kutupa taka bila mpangilio hali ambayo imezigeuza kuwa hatari kwa wasafiri na wafanyabiashara.

Hali hii inahatarisha afya za raia. Isitoshe, panya wanaonekana waziwazi wakikimbizana katika barabara zilizoathirika.

Katika mji wa Murang’a, barabara inayoelekea katika mtaa wa Grogon imefungwa na rundo la taka huku serikali ya Gavana Irungu Kang’ata ikitoa onyo kwa wachafuzi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mazingira wa Serikali ya Kaunti ya Murang’a Mary Magochi, “tunajizatiti kukabiliana na hali hiyo”.

Hata hivyo, alikiri kuwa mafuriko yaliyosababishwa na mvua inayonyesha katika maeneo mengi mjini humu yamefanya shughuli ya usafishaji mji kujikokota.

Taka zikiwa zimefunga barabara mjini Murang’a mnamo Mei 1, 2024. PICHA | MWANGI MUIRURI

Bi Magochi alisema kwamba kwa sasa, maafisa wa utekelezaji sheria za miji wameombwa waimarishe misako ya wanaotupa takataka kiholela.

“Kuna mapipa ya serikali ambayo tumeweka katika kila pembe za miji ya kuwasaidia wenyeji kutupa takataka yao nasi tuwe na wakati rahisi wa kuikusanya. Lakini kunao wanatulemaza kupitia ujambazi wa kuitipa kiholela,” akasema Bi Magochi.

Huku watoto wa shule wakiwa katika likizo iliyorefushwa, baadhi ya wazazi wamelalamika kwamba vishoroba vya miji kadha ni vichafu huku baadhi ya nyumba za upangaji zikivamiwa na taka zilizosafirishwa na maji ya mafuriko.

“Tunaomba utawala wa Kang’ata uwaandame wanaochafua mazingira kiasi hata cha kutupa kiholeka mipira ya kondomu na sodo zilizotumika,” akasema Bi Sarah Njahira, ambaye ni mkazi wa Murang’a.

Taka zikiwa zimefunga barabara mjini Murang’a mnamo Mei 1, 2024. PICHA | MWANGI MUIRURI

Bw Charles Ngigi ambaye ni mpangaji katika mji wa Murang’a aliteta kwamba ukaguzi wa nyumba za upangaji umetelekezwa huku wamiliki wengi wa majengo wakikosa kuzingatia usafi wa kimsingi.

“Nyumba nyingi za kukodisha hazijapakwa rangi huku miundombinu ya kutupa majitaka ya baadhi ya nyumba ikiwa katika hali duni. Hali hizi zinafanya afya ya wapangaji kuwa hatarini huku ugonjwa hatari wa kipindupindu ukituvizia,” akasema.

Mwenyekiti wa muungano wa uzingatiaji usalama wa mazingira kupitia kilimo asili Bw Martin Ndirangu, alilalama kwamba “tumekuwa tukiteta kuhusu uchafuzi kiholela wa mazingira lakini tunaambiwa kuwa kaunti haina maafisa wa kutosha wa kuzingatia utekelezaji sheria”.

Lakini Bi Magochi alisema kwamba amekuwa akipata tetesi hizo kutoka kwa baadhi ya wakazi “lakini huwa natuma maafisa kuwajibika.”

[email protected]