Habari MsetoSiasa

Takwimu za sensa ni feki sana – Magavana

November 6th, 2019 3 min read

Na WAANDISHI WETU

MATOKEO ya Sensa yaliyotolewa Jumatatu yameibua joto huku baadhi ya wanasiasa na wataalamu wakitilia shaka uhalisi wake na kutaka shughuli hiyo irudiwe.

Magavana kutoka kaunti zilizoorodheshwa kuwa na idadi ndogo ya watu walidai kuwa matokeo hayo yalilenga kutimiza maslahi ya kisiasa hasa wakati huu mjadala unatarajiwa kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Kulingana na viongozi hao, matokeo hayo yalikarabatiwa ili kunyima baadhi ya maeneo haki ya uwakilishi na mapato kutoka serikali ya kitaifa.

Viongozi wa kaunti ya Tharaka Nithi waliojawa na hasira, walitilia shaka matokeo hayo yaliyoonyesha kuwa kaunti yao ina watu 393,177 ikilinganishwa na 365, 847 kwenye sensa ya 2009 kuonyesha kuwa katika kipindi cha miaka kumi ni watu 27,330 waliozaliwa.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, kaunti hiyo ilikuwa na wapigakura 213,156 ambao ni zaidi nusu ya wakazi wote.

Gavana wa kaunti hiyo Muthomi Njuki, wabunge Kareke Mbiuki (Maara), Patrick Munene (Chuka Igambang’ombe) na Gitonga Murugara (Tharaka) walisema kwamba hawataruhusu matokeo hayo yatumike kwenye mgao wa rasilimali kwa kaunti yao, wakiyataja kuwa feki.

“Ni jambo la wazi kwamba matokeo sio ya kweli na tunayahusisha na ripoti ya BBI kwa kuwa ni ajenda inayosukumwa kisiasa na watu wasiotakia watu wetu mema,” alisema Bw Munene.

Akikosoa matokeo hayo, Bw Njuki alishikilia kwamba haiwezekani wakazi waliongezeka kwa watu 27,000 ilhali ripoti ya idara ya usajili inaonyesha watoto waliozaliwa katika kipindi cha miaka saba iliyopita ni 53,930 huku watu walioaga dunia wakiwa 10,411.

“Tunakataa takwimu hizi kwa kuwa zinatumiwa kutimiza malengo ya kisiasa hapo 2022. Haiwezekani kamwe idadi ya watu wazima izidi ya watoto. Tutaelekea mahakamani iwapo KNBS haitarudia sensa eneo letu,” alisema Gavana Njuki.

Wanasiasa hao walidai kwamba dalili zote zilionyesha kuwa idadi ya wakazi wote wa Tharaka-Nithi ilikuwa imefika zaidi ya watu 480,000.

Bw Mbiuki alisema matokeo hayo yamewashangaza hata Wakenya wengine ambao wanafahamu kwamba eneo hilo liliokoa serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwenye uchaguzi wa 2007 kwa kura nyingi ilhali sasa linaonewa ikilinganishwa na maeneo mengine ya Mlima Kenya.

Gavana Kiraitu Murungi wa kaunti jirani ya Meru, Francis Kimemia wa Nyandarua na Wycliff Wangamati na Naibu Gavana wa Samburu Bw Julius Leseeto pia walitilia shaka uhalisi wa matokeo hayo.

Bw Kimemia alisema haiwezekani kuwa wakazi wa Nyandarua waliongezeka kwa watu 40,000 katika kipindi cha miaka kumi.

Kwa upande wake, Bw Wangamati alisema ingawa kaunti yake iliorodheshwa ya tano kwa wingi wa watu, ilishikilia nafasi hiyo miaka kumi iliyopita.

“Kaunti yetu inajulikana kwa kuwa na watu wengi na tuko na bidii kuzaa. Tunashangaa ni nini kilichofanyika,” alisema Bw Wangamati.

Aliyekuwa seneta wa Kakamega, alitilia shaka takwimu za KNBS kwamba idadi ya wakazi wa eneobunge la Ikolomani alilowahi kuwakilisha bungeni lilipungua kutoka watu 143,153 mwaka wa 2009 hadi 111,743 mwaka huu.

“Wacheni zenu. Hakukuwa na mkurupuko wa maradhi Ikolomani! Haya matokeo ni feki na yanalenga kunyima baadhi ya sehemu na jamii mgao wa mapato ya kitaifa,” alisema Bw Khalwale.

Naye aliyekuwa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo alisema matokeo hayo yanaonyesha kuna tatizo na akatoa mfano wa kaunti ya Tharaka Nithi.

“Miaka kumi na miwili iliyopita, Tharaka Nithi ilikuwa na wapigakura 216,000 na sasa watu wote ni 393,000. Kuna jambo lisilo la kawaida,” alieleza.

Kulingana na aliyekuwa seneta wa Mandera, Billow Kerrow, matokeo hayo sio ya kuaminiwa.

“Eneo la Kati ya Kenya lililo na kiwango cha chini kupata watoto sasa lina watu wengi. Kaskazini Mashariki ambalo wanawake wanapata watoto wengi na familia kubwa lina kiwango cha chini cha ongezeko la watu. Hii ni sensa ya vifaranga,” Bw Kerrow aliandika kwenye Twitter.

Aliyekuwa spika wa bunge la taifa Farah Maalim alisema sensa nchini Kenya hutumiwa kutimiza maslahi ya kisiasa naye Fatuma Gedi akahusisha kupungua kwa idadi ya wakazi wa baadhi ya maeneo ya Kaskazini Mashariki na maisha yao ya kuhamahama.

“Baadhi ya watu wametilia shaka matokeo ya sensa katika eneo la Kaskazini Mashariki, watu ni wafugaji wa kuhamahama. Nafikiri baadhi yao huenda walikuwa wamehama sensa ilipofanywa,” alisema.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya uchumi Bw Tony Watima, kuna masuala yanayohitaji ufafanuzi zaidi katika ripoti ya sensa hasa kuhusu kaunti za Kiambu na Mandera.

“Kiambu ina ongezeko la asilimia 49 ya watu ilhali Mandera imepungua kwa asilimia 15 ilhali kiwango cha idadi ya watoto wanaozaliwa hakiungi hali hii. Na haiwezi kuwa wakazi wengi wa Nairobi wamehamia Kiambu,” asema Bw Watima.

Wengine waliokosoa matokeo hayo ni gavana wa Meru Kiraitu Murungi ambaye alitisha kushtaki KNBS akisema idadi ya watu 1.5 milioni ni ya chini, mbunge wa Kandara Alice Wahome aliyedai wakazi wa Murang’a ni zaidi ya 1,056,640 na seneta wa kaunti ya Kisii Profesa Sam Ongeri aliyesema kuwa takwimu kwamba wakazi wa Kisii ni 1.26m na Nyamira ni 605, 576 sio za kuaminiwa.

Ripoti Za: Benson Matheka, Cecil Odongo, Waikwa Maina na Samuel Baya