Habari

TALAKA: Madiwani wa kike Lamu wawalaumu akina mama wapendao 'vitu vya bei ghali'

March 3rd, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MADIWANI wanawake katika Bunge la Kaunti ya Lamu wamewakashifu akina mama wanaoishi maisha ya gharama ya juu kupita kiasi wakisema tabia hiyo imechangia ongezeko la talaka eneo hilo.

Kulingana na ripoti ya mwaka 2019 kutoka kwa Ofisi ya Kadhi, Kaunti ya Lamu, ilirekodi asilimia 60 ya ndoa zinazovunjika eneo hilo ilhali nyingine 60 zikiwa hazijasajiliwa.

Hii inaashiria kwamba ni asilimia 40 pekee ya ndoa zinazofungwa kote Lamu ambazo hudumu.

Katika kikao maalum na wanahabari nje ya majengo ya Bunge la Lamu, madiwani hao wa kike walisema baadhi ya wanawake wamejipandisha sana hadhi na kuzoea ‘vitu vya bei ghali’ kupita kiasi na hivyo kuwagongesha ukutani waume ambao baadaye hulazimika kudai talaka.

Wakiongozwa na diwani maalum, Bi Amina Kale, viongozi hao wamewashauri wanawake kuishi maisha yanayolingana na kazi na mapato ya waume ili kuepuka kuwafinya na hata kukosa kuhisi ladha ya maisha ya ndoa.

Bi Kale pia amewataka akina mama kupunguza starehe nyingi, ikiwemo kuhudhuria kila hafla za harusi zinazofanyika eneo hilo, hatua ambayo pia aliitaja inaongeza gharama ya maisha.

“Hii tabia ya wanawake kutaka kuishi maisha ghali ambayo waume hawawezi imechangia ndoa nyingi kuvunjika. Wanaume wengi hapa Lamu ni wavuvi na kipato chao ni cha chini; sasa inakuwaje wewe mke umfinye kwa kuishi maisha ya thamani ya juu ambayo si uwezo wako au wa mumeo?”  akasikitika Bi Kale.

Amewashauri kina mama wakubali hali zao na kuishi kulingana na uwezo wao na wa waume ili kuziokoa ndoa Lamu.

Mwakilishi wa Wadi ya Hindi, Bi Anab Haji pia ameunga mkono kauli hiyo, akishikilia kuwa kutojikubali kwa wanawake kuishi maisha yanayolingana na mifuko yao ni sababu kuu ambayo imewasukuma wengine kuvunja uaminifu katika ndoa zao.

Kulingana na Bi Haji, baadhi ya wanawake wamewadharau waume zao na kukimbilia kutafuta marafiki wa nje wa kuwasaidia kukimu maisha yao ghali.

“Baadhi ya wanawake wanadharau waume zao hasa punde wanaposhindwa kukimu gharama ya juu ya maisha wayatakayo. Wanaishia kutafuta wapenzi wa nje ili kukimu maisha yao ya gharama ya juu,” akasema Bi Haji.

Viongozi hao aidha wamewataka wanaume kusimama imara na kuongoza familia zao vyema ili kuepuka mahangaiko ambayo mara nyingi huwafika watoto punde ndoa zinapovunjika na talaka kutolewa.

Pia wamewataka wanaume na wanawake kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na uraibu mwingine, ikiwemo utafunaji miraa na muguka ambao mara nyingi pia huchangia kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa wanafamilia.