NA PATRICK KILAVUKA
AMEZAMIA katika kukuza kipaji cha tenisi kwa kuiga mchezaji mahiri Angela Okutuyi ambaye amekuwa mwiba katika ulingo wa kimataifa na Mrusi Daniil Sergeyevich Medvedev, 26 ambaye anashikilia nafasi ya tano duniani katika tenisi.
Baraka Ominde,12, mwanafunzi wa Darasa la Nane katika Shule ya Msingi ya Ribeiro Parklands na mwana wa tatu katika familia ya watoto watano wa Bw Jared Ominde na Bi Rosemary Achieng Ominde, anasema alianza kuwa na kiu ya kucheza tenisi akiwa na umri wa miaka mitano akiwa katika Shule ya Msingi ya Simoga Valley, Ruaka.
Wakati huo, alikuwa anapigia zoezi klabu ya Karura Forest, Gigiri kabla ya kuguria Nairobi Sports kisha kupiga hema lake la mazoezi katika uga wa Oshwal Sports Complex hadi wa leo.
Mkufunzi wake wa kwanza alikuwa babaye ambaye amemchochea zaidi na kumhimiza kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa kwa hali na mali. Isitoshe kakaye Derrick Ominde pia amekuwa akifanya mazoezi naye.
Hata hivyo, amekuwa mikobani mwa makocha wengine wa kitaifa Carol Oduor na Kevin Kiango ambao wamekumbatia pia talanta yake na kumtoatoa ubutu kiasi kwamba,sasa anaweza kutetemesha anga ya kitaifa na kimataifa.
Baraka ameshiriki mashindano kadha wa kadha humu nchini pamoja na kimataifa ambapo alishiriki kama mchezaji au na timu ya wanatenisi chipukizi ya Kenya.
Amekuwa jabali wa ITF nchini U12 na U14 mwaka 2018 na 2019 mtawalia.Pia ameshirii katika mashindano ya kimataifa ya Bingwa wa Chipukizi ya Bara la Afrika (AJTC) katika nchi za Morocco 2018, Tanzania 2019, Tunisia 2021 na Eygpt mara mbili 2021 na Rwanda kama timu.
Alikuwa katika kikosi ambacho kiliwakilisha Kenya katika mashindano ya mabingwa Chipukizi wa Bara Afrika nchini Misiri mwaka huu ambapo timu ya Kenya ilimaliza katika nafasi ya tano bora miongoni mwa mataifa manane. Kikosi hicho kilijumuisha Ayush Brian, Baraka Ominde, Sheline Ahoya, Stacy Chepkemoi na Melisa Mwaka.
Ominde hujinoa kila Jumamosi na Jumapili kujiweka fiti kiafya kwa kujiundia usuli wa kukabiliana na dhoruba za kuwa mwanatenisi.
“Mimi hula vyakula vyenye lishe bora – vya kuujenga na kuukinga mwili pamoja na kujipatia nguvu kupitia kwa kula samaki, ugali, mboga na matunda ili kujiongezea vitamini. Zaidi ya yote, mimi hunywa maji kwa wingi,” anasema mwanatenisi Ominde.
Anasema mipango yake ni kujisuka vyema ili uchezaji tenisi uwe taaluma yake siku za majaliwa akiwa na matamanio ya kuwa na akademia kubwa ya tenisi na kuwa kocha mtajika.
Uraibu wake ni kuogelea na kusakata kabumbu.
Uchezaji tenisi umemwezesha kutembelea pembe mbalimbali nchini na nje ya Kenya na kushiriki mashindano yenye ushindani ambayo yamempa changamoto ya kusimama imara katika kuhakikisha anapiga hatua katika fani hii.
Ominde anashauri chikupizi wenzake kufuata ndoto zao na kutia bidii katika wanachofanya pasi na kukata tamaa katika kujikuza.
Subscribe our newsletter to stay updated