Makala

Talanta imemwezesha kukutana na Rais Kenyatta

March 1st, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

MTAA wa Majengo, Nyeri kwa muda mrefu umekuwa ukigonga vichwa vya vyombo vya habari kwa sababu ya visa vya uhalifu visivyokosa kushuhudiwa aghalabu kila wakati.

Unapouzuru, utakabirishwa na majengo ya mabanda, hasa mabati.

Jamal Kigundu Njambe maarufu Lehman, ni mzawa wa eneo hilo na amelelewa mumo humo, hivyo basi anaelewa kwa undani matukio yanayofanyika.

Hata hivyo, historia ya waliovalia njuga nia ya kubadili taswira ya mtaa huo ikiandikwa, jina lake halitakosa kujumuishwa.

Kwa zaidi ya miaka mitano, kijana huyu amekuwa katika mstari wa mbele kutumia sanaa kubadilisha mawazo potovu ya vijana, haswa dhidi ya kushiriki uhalifu. Ni maarufu kwa Hip Hop na Rap, michezo ya kuigiza na sarakasi, malenga na mwanamasumbwi hodari.

Juhudi zake Jamal Kigundu Njambe katika uundaji wa mapambo yakiwa na nembo ya bendera ya Kenya zimemuwezesha kukutana na Rais Uhuru Kenyatta. Picha/ Sammy Waweru

Anatumia vipaji vyake kunoa wale chipukizi, na ni katika hali hii anahusisha vijana kwa kuteka bakunja mawazo yao ili kujiepusha na visa haramu.

“Mafunzo huyatoa kuanzia kwa watoto hadi vijana waliobaleghe. Ni jukumu langu kama kijana mzalendo wa nchi hii kunusuru kizazi kijacho,” anasema Jamal.

Isitoshe, barobaro huyu ni muundaji wa kipekee wa bidhaa za urembo na utanashati kwa kutumia shanga. Kinachovutia zaidi katika gange hii, huzitengeneza kwa kuzingatia nembo ya bendera ya Kenya. “Fahari yangu ni kuona mtu amevalia bidhaa nilizounda, hususan zenye nembo ya Kenya. Muacha mila ni mtumwa, kwa nini tuache mila, tamaduni na itikadi zetu?” anahoji.

Kukutana na Rais Kenyatta

Mapambo anayounda ni; bangili/vikuku, mikufu, mapochi, mikoba, pete, mishipi, herini, tai, haya yakiwa machache tu kuyataja. “Pia hutengeneza bendera kwa shanga,” afichua kijana huyu mkakamavu. Ni kufuatia juhudi za uzalendo wake, 2017 alipata nafasi ya kipekee kukutana ana kwa ana na Rais Uhuru Kenyatta, katika maonyesho ya sanaa mjini Mombasa.

Ni wachache mno wanaopata fursa ya kuamkuana na viongozi wa nchi walio mamlakani, lakini Jamal alipata mwanya wa kipekee kumvisha bangili.

Jamal Kigundu Njambe akionyesha picha ya Maonyesho ya Sanaa, Mombasa, akimsalimia Rais Uhuru Kenyatta na kumvisha bangili mwaka 2017. Picha/ Sammy Waweru

“Alinipongeza kwa kazi kuntu ninayofanya, akiwa mwingi wa hamu kwamba tutapatana baadaye ili tujadili namna ya kuimarisha sekta ya sanaa nchini,” akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano, akionesha picha akiwa na Rais.

Karakana yake ni nje ya makazi anayoishi, shughuli ya kuunda bidhaa akiiendeshea kwenye meza.

Kuna wanaomdhalilisha, lakini hawapi sikio kamwe kwani bidii zake za mchwa zimemuwezesha kukutana na kiongozi wa nchi.

Baadhi ya mataifa hutumia sanaa kudumisha mila na tamaduni zake. Wizara ya Michezo na Turathi za Kitaifa ndiyo imetwikwa jukumu la kuangazia sanaa, lakini hapa nchini kwa kiasi fulani imeonekana kuipuuza.

“Shida kuu iliyopo wizara husika haionekani kutilia maanani wasanii, hasa wa nyimbo za kiasili. Hukumbukwa tu katika sherehe za maadhimisho ya kitaifa,” anasema Bi Hellen Jepkemoi, ambaye mbali na kuwa mkulima Uasin Gishu, hushiriki nyimbo asilia za jamii ya Kalenjin.

Bw Jamal alitambua amejaaliwa talanta za fani mbalimbali katika sanaa akiwa kidato cha tatu mwaka wa 2009.

Alikuwa akishiriki tamasha za mashindano ya nyimbo za kitaifa. Vilevile, alikuwa akihudhuria maonyesho ya sanaa.

“Nilikutana na mama ya mwanafunzi mwenza, ambaye alikuwa akiunda bidhaa za mapambo kwa shanga na ndiye alinipa motisha,” anasimulia msanii huyu.

Mtaji

Alivamia usanii rasmi 2015, na iligharimu mtaji wa Sh5,000 pekee. Mali ghafi anayotumia kuunda bidhaa za mapambo ni; shanga za rangi tofauti, kamba maalumu aina ya singa, fishing twine na nyuzi, vifaa vikiwa wembe na makasi. Kwa siku huunda mapambo yasiyopungua 10, akitumia mitandao ya kijamii, maonyesho ya sanaa na kuchuuza, kufanya mauzo.

Bidhaa zake zinagharimu kati ya Sh100 hadi Sh10,000

Wakati wa mahojiano alisema kwa siku hakosi kutia kibindoni zaidi ya Sh1,000.

Hakuna jitihada zisizokosa milima na mabonde, alisema mali ghafi wakati mwingine huadimika na yanapopatikana huwa ghali. Hugawanya ratiba yake, kiasi kuwa anapata muda wa kutoa mafunzo ya michezo ya kuigiza na sarakasi, mashairi na masumbwi.

Ili kupiga jeki vijana katika sanaa, Beatrice Mwaura msusi wa mikeka anahimiza serikali kuwa ikitengea sekta hii mgao wa fedha katika makadirio yake ya bajeti ya kila mwaka.

“Kupitia ugatuzi, serikali za kaunti zishirikiane na ile kuu kuinua sanaa ili suala la ukosefu wa kazi litatuliwe,” ashauri Bi Beatrice. Wizara husika pia ifanye hamasisho la sekta hii kwa minajili ya kuvutia wafadhili.