TALANTA: Pacha waimbaji

TALANTA: Pacha waimbaji

NA WYCLIFFE NYABERI

WIKI tatu zilizopita, pacha wawili wasichana waliteka hisia za waombolezaji katika ibada ya mazishi ya mamake mhariri wa michezo wa kampuni ya Nation Media Group (NMG) Elias Makori.

Jasmine Moraa na Shantel Nyaboke (umri wa miaka 6) walifanya kila aliyehudhuria ibada hiyo, wakiwemo wakuu wa kampuni ya NMG na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kakamega Joseph Obanyi kutulia tuli waliporindima wimbo wao uitwao “Kifo.”

Hafla hiyo ilifanyika kijijini Nyakemincha, eneobunge la Mugirango Magharibi, katika kaunti ya Nyamira.

Kutokana na ustadi wao wa uimbaji unaoambatanishwa na ishara, safu ya Elimu Msingi iliwatafuta watoto hawa kufahamu mengi kuhusu talanta yao.

Jasmine na Shantel ni wanafunzi wa gredi ya pili katika shule ya msingi ya Magwagwa. Shule hii inapatikana katika eneobunge la Mugirango Kaskazini.

Wamerekodi vibao vingi lakini vile vilivyopata umaarufu zaidi ni ‘Kifo’ na kingine cha hivi punde cha kumsifia Rais William Ruto.

Wimbo huu waliutunga kwa njia ya kipekee umwendee Rais Ruto. Kufikia wakati wa kuandikwa kwa makala haya ulikuwa umetazamwa na watu elfu moja kwenye mtandao wao wa YouTube, siku sita tu baada ya kuwekwa kwenye akaunti hiyo.

Mama wa watoto hao Bi Jane Kerubo anasema wanawe waliamua kutunga wimbo wa Rais Ruto kumsihi asiwe mtu wa kulipiza kisasi.

Wanaeleza kwa ufupi masaibu aliyoyapitia Rais Ruto katika safari yake ya kuingia Ikulu, huku wakitolea mfano uhasama uliojiri baina yake na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta. Kwa kuwa rais hakuweka kinyongo na “waliomsaliti”, waimbaji hao wanamtunuku koja la maua kupitia kuimba kwao.

“Mbali na kumsifu Dkt Ruto, wanamsihi awe rais wa Wakenya wote na awakumbatie waliokuwa marafiki zake lakini wakamsaliti jinsi Juda alivyomfanyia Yesu,” Bi Kerubo anaeleza.

Ule wa “Kifo”, waliouweka katika YouTube miezi mitano iliyopita, umetazamwa na watu zaidi ya laki mbili na nusu.

Wanazungumzia kwa kina jinsi ambavyo kifo kimewanyakua watu wengi wa matabaka mbalimbali.

Wanazungumzia watu waliokuwa na manufaa mengi maishani lakini kwa bahati mbaya wakaondoka duniani.

Unapoutazama au kuusikiza wimbo huu, bila shaka fikira zako zitakukumbusha kumhusu mtu fulani uliyekuwa unamjua lakini kwa bahati mbaya akafariki.

Watoto hawa wana ndoto kwamba siku moja watakuwa kama mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili Mtanzania Rose Muhando.

Wakati wa likizo, watoto hawa huhudhuria krusedi na mikutano mingine ya injili na kuomba nafasi ya kuzitangaza nyimbo zao.

Shantel anaamini kuwa kutokana na kazi yao, angalau mja mmoja au wawili wataokoka kwa kuguswa na nyimbo zao.

Ombi lao ni kwa Mkenya yeyote mwenye nia njema ajitolee na kuwasaidia warekodi video nyingi iwezekanavyo kwani wana uwezo wa kujitungia nyimbo.

Wakati mwingi mama yao ndiye huwaelekeza na kuhakikisha kuwa hawazami tu katika nyimbo bali pia wanakumbuka masomo yao kwa kutia bidii.

  • Tags

You can share this post!

Kijana mjasiriamali atangaza nia ya kufuata nyayo za Ruto

MWALIMU WA WIKI: Gikundi mwalimu tajiri wa hamasa

T L