TALANTA YANGU: Matunda ya mfumo wa CBC

TALANTA YANGU: Matunda ya mfumo wa CBC

NA PATRICK KILAVUKA

ANALENGA kukuza talanta yake ya ushonaji na usanii hadi awe msanifishaji wa mitindo siku za usoni kwa kutumia mbinu ambazo amezipata kutokana na mtaala wa umilisi na utendaji na uwezo wake asilia wa kuzaliwa kunogesha kipaji chake.

Gracie Gathoni,10, mwanafunzi wa gredi ya tano, shule ya msingi ya Parkroad, Kaunti ya Nairobi ni mwana wa pili katika familia ya watoto watatu wa Bw Chrispus Maina na Susan Muthoni na ana matumaini ya kuafikia malengo yake majaliwa.Kutimiza ndoto yake, anafuma vikapu na vitambaa vya nyuzi za rangi mseto vya kujifunika akitumia sindano maalum ya crocket.

Aidha, yeye hutengeneza mikufu, vishiko vya funguo, mikanda na bangili kwa kutumia sehemu ya ndani ya vibandiko vya plastiki vya chupa ambavyo vina rangi tofuati tofauti.

Mshonaji huyu alianza kujifunza kazi hii akiwa Gredi ya Tatu.

Anasema wakati huo kulikuwa na rafiki yake kwa jina Natasha Nyanjogu aliyekuwa anajua kushona na akamuomba amfunze pasi na kujua kwamba, ni talanta ambayo ilikuwa imetulia ndani yake. Alihitaji tu siku mbili kujua.

Hata hivyo, baada ya kufunzwa, mtaala wa Umilisi ulibakia nguzo muhimu ya kuchonga talanta yake kupitia mwalimu Janeffer Nyamai ambaye alimtambua na kuanza kukikuza kipaji chake na sasa yeye ni moto wa pasi katika kusanii vikapu, vitambaa na shanga.

Gracie Muthoni akishona kwa uelekezi wa mwalimu wake Jannffer Nyamai. PICHA | PATRICK KILAVUKA

“Nimekuwa nikimfuatilia. Alikuwa mwanafunzi bora darasani na hata mradi wake wa kazi yake katika mtaala wa umilisi na utendaji uliibuka bora zaidi akiwa katika gredi ya tatu. Hii ni licha ya kuwa yeye pia ni mchoraji stadi,” anadokeza mwalimu Nyamai.

Kuhusu vikapu anavyovifuma, yeye huviuza kujipatia hela. Kikapu kikubwa hukiuza kwa Sh1,500 na kidogo Sh1,000.

Anaweza kuchukua wiki moja kusuka kikapu kikubwa huku kile kidogo kikimchukua siku mbili au tatu.

Gathoni hutumia wakati wake wa ziada shuleni na nyumbani kushona huku pia akifunza wanafunzi wenza ambao wana ari ya kujua.

Wanafunzi ambao huchota maarifa ya kushona kutoka kwake ni pamoja na Victoria Makhungu, Precious Ndemo na Marwa Mohammed.

Anasema yeye huendeleza maarifa ya usanifishaji mitindo ya ushonaji wake kwa kupanga nyumba yao kwa wanasesere ambao amewapamba vitambaa kama njia ya kujifahamisha na namna ya kutia ulimbwende wa fasheni.

Gathoni anampongeza mamaye kwa kumfaa kwa malighafi ya kutengeneza na kushonea kazi zake pamoja na mwalimu Nyamai ambaye amelea kipaji chake shuleni.

“Wawili hawa hunihimiza na kunitia hamasa ya kuiendeleza talanta yangu,” anasisitiza Gathoni.

Changamoto inayomkabili ni kwamba wakati mwingine inakuwa vigumu kupata aina fulani ya uzi wa rangi fulani kutokana na bei ghali.

Ukosefu wa wa muda wa kutosha kutokana na mbano wa masomo. Hata hivyo yeye hujaribu kusawazisha wakati wake kwa kutumia muda wa ziada na wikendi.

Ushauri wake ni kwamba, wanatalanta watumie vipawa vyao kwa manufaa ya ufanisi na wautanue uwezo wao hadi wazifikie ndoto zao maishani.

You can share this post!

Raila Odinga amteua Martha Karua awe mgombea mwenza wake

Shule ya Sheikh Khalifa kufanya hafla maalum ya kuomboleza...

T L