Kimataifa

Taliban yasema haijaacha mapigano dhidi ya serikali ya Afghanistan

December 31st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

KUNDI la Taliban lilikanusha Jumatatu ripoti kuwa lilikubali kusitisha vita dhidi ya serikali ya Afghanistan baada ya uvumi kuenea kuwa liliafikia mkataba wa kumaliza vita vya miaka 18.

“Katika siku chache zilizopita, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa habari za uwongo kuhusu kusitisha vita. Ukweli wa mambo ni kuwa Islamic Emirate of Afghanistan haina mipango ya kuacha vita,” Taliban ilisema kwenye taarifa.

Taarifa hiyo inajiri huku wanajeshi wa serikali na wa kimataifa wakijiandaa kwa vita vikali msimu wa baridi huku Amerika ikiongoza mazungumzo na Taliban kumaliza vita Afghanistan.

Hata hivyo, vita vimekuwa vikiendelea hata Amerika inapoendelea kujadiliana na magaidi hao. Amerika inataka kuondoa wanajeshi wake iwapo wanamgambo hao watakomesha vita.

Afghanistan pia imekubwa na msukosuko wa kisiasa huku maafisa wakitangaza matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa urais ambao ulionyesha Rais Ashraf Ghani akielekea kushinda kwa kipindi cha pili.

Maafisa wa uchaguzi hawajatangaza matokeo ya mwisho baada ya kupokea malalamishi zaidi ya 16,000 kuhusu uchaguzi huo.

Taliban husema Ghani ni kibaraka wa Amerika na wamekataa kuzungumza na serikali yake na kufanya watu wengi kuhofia kuwa watarudia vita dhidi ya wanajeshi wa serikali iwapo Amerika itakubaliana nao na kuondoa wanajeshi wake.

Mnamo Jumapili, vyombo vya habari viliripoti kuwa Baraza tawala la Taliban lilikubali kusitisha vita kwa muda ili kutoa mwanya wa muafaka wa amani na Amerika. Ripoti zilizonukuu maafisa wakuu wa kundi hilo.

Amerika imekuwa ikilitaka kundi hilo kusitisha vita kabla ya kutia sahihi muafaka wa amani.

Kabla ya muafaka huo, Amerika inataka Taliban kuhakikisha kuwa Afghanistan haitatumiwa kama makao ya makundi ya kigaidi. Amerika ina wanajeshi 12,000 Afghanistan.

Ni lazima mkuu wa Taliban aidhinishe uamuzi wowote wa kusitisha mapigano na inaonekana hakufanya hivyo.

Inasemekana kuwa wanachama wanne wa Taliban wanaoshiriki mazungumzo ya amani walikutana na baraza tawala kabla ya kukanusha ripoti kwamba linapanga kuacha vita.

Wanachama wanaoshiriki mazungumzo walirudi Afghanistan Jumapili kutoka Qatar ambako kundi hilo lina ofisi za masuala ya kisiasa na ambako mjumbe wa Amerika Zalmay Khalilzad amekuwa akikutana nalo kwa mazungumzo tangu Septemba 2018.

Taliban na wanajeshi wa Afghanistan wanaosaidiwa na Amerika wamekuwa wakishambuliana mara kwa mara.

Ingawa Taliban hulenga wanajeshi na maafisa wa serikali, maelfu ya raia wamekuwa wakiuawa kupitia mabomu.

Umoja wa mataifa umezitaka pande zote mbili kutolenga raia.