Habari Mseto

Tamaduni za Wamakonde sasa kuhifadhiwa Bomas

December 20th, 2018 1 min read

Na KNA

UTAMADUNI wa kabila la Makonde ambalo liliidhinishwa kuwa la 43 humu nchini sasa utahifadhiwa na kuonyeshwa katika maonyesho ya kitamaduni ya kitaifa, Bomas of Kenya.

Serikali ya Kaunti ya Kwale ilisimamia kurekodiwa kwa utamaduni wa jamii hiyo ili uwe sehemu ya taifa kulingana na Waziri wa Utamaduni na Huduma za Kijamii, Ramadhan Bungale.

“Nilipeleka ujumbe wa watu wa jamii hiyo ambao walikuwa wakihusika na masuala ya kitamaduni, ambapo mambo ya kitamaduni kama densi zilirekodiwa katika shughuli zilizotuchukua wiki mbili,” Bw Bungale akasema.

Watu wa jamii hiyo walitambuliwa rasmi kuwa moja ya makabila ya Kenya mnamo 2017, baada ya watu 300 wa kabila hilo kutembea kutoka Kwale hadi Nairobi mnamo 2016 wakitaka serikali kuwapa vitambulisho.

Baada ya ziara hiyo, Rais Uhuru Kenyatta alikutana nao katika ikulu na kuwaidhinisha, na majuzi wakati Rais wa Mozambique Filipe Nyusi alipozuru humu nchini, ni watu hao tu ambao waliruhusiwa kukutana naye.

Kabila hilo lilishiriki uchaguzi wa kitaifa kwa mara ya kwanza mnamo 2017, tangu mababa na mababu zao walipofika nchini miaka ya 30, walipokuja kufanya kazi katika mashamba ya miwa, katika kiwanda cha Ramisi, eneo la Msambweni.

Hata wakati kiwanda hicho kilianguka baadaye, watu hao hawakurejea nchi yao, bali waliendelea kuishi humu nchini kama maskuota katika mazingira ya kichochole katika mashamba hayo yaliyokuwa ya miwa.

Watu hao wanapatikana maeneo ya Kitsakamkwaju, Pongwe-Kidimu na Pongwe-Kikokeni, eneo la Msambweni.

Baada ya kutambulika, baadhi ya watu wa jamii hiyo wamepewa kazi za utumishi wa umma ili wawe sehemu ya serikali.