Habari Mseto

Tamasha ya kumuenzi De' Mathew kuandaliwa leo Ijumaa

August 23rd, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE na MARY WANGARI

MASHABIKI wa marehemu mwanamziki nyota wa Benga, John Mwangi Nga’ng’a, almaarufu John De’ Mathew, wamepata fursa ya kipekee ya kumpa heshima ya mwisho, baada ya Gavana wa Murang’a, Mwangi wa Iria kufadhili tamasha ya Mugithi, Ijumaa, Agosti 23, kabla ya mazishi yake Jumamosi.

Kulingana na gavana huyo, tamasha hiyo itakayofanyika usiku kucha katika hoteli ya Golden Palm mjini Kenol, itawapa mashabiki wa mwanamuziki huyo tajika wa nyimbo za Kikuyu, fursa ya kumkumbuka kwa kucheza albamu zote zake za mziki.

Wasanii kutoka eneo la Mlima Kenya pia wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hiyo itakayoendelea usiku wote.

Mashabiki wa marehemu pia wameunda kikundi cha mtandao wa kijamii cha Watsapp ambapo wanajitolea kutoa mbuzi watakaochinjwa wakati wa hafla hiyo.

Gavana huyo alisema tamasha hiyo itawakumbusha wanajamii wa Agikuyu kuhusu maisha na nyakati za marehemu John De’ Mathew.

“Tunataka kumkumbuka kwa kusikiza nyimbo zake zote zinazochangia nafasi muhimu katika kuiunganisha jamii ya Agikuyu pamoja na kuwashauri na kuwaburudisha watu wetu,” alisema gavana.

Kulingana na gavana huyo, marehemu alikuwa kiongozi halisi wa wasanii kutoka eneo la Kati nchini Kenya, baada ya kifo cha mwanamuziki Joseph Kamaru aliyefariki mwaka 2018

“Mwendazake hakuwa mwanamuziki wako wa kawaida, alichukua usukani kutoka kwa marehemu Joseph Kamaru na kwa hakika, ni baada tu ya kifo cha Kamaru, ambapo muungano wa wanamuziki wa eneo la Kati ulibuniwa na De’ Mathew akachaguliwa kuwa mwenyekiti wake,” alisema gavana.

Marehemu atazikwa Jumamosi katika kipande cha ardhi cha familia yake eneo la Mukurwe, Gatanga katika hafla ambayo Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuhudhuria.

Mwimbaji huyo wa kibao kilichovuma cha ‘My dear Nduku’ ambacho pia kilionekana ‘kutabiri’ kuhusu kifo chake, alifariki mnamo Jumapili, Agosti 18, 2019, katika ajali barabarani, iliyotikisa taifa.