Makala

Tambiko lafanywa kulaani ‘wanaochochea vijana kubishana na serikali’

July 5th, 2024 2 min read

WAZEE wa jamii ya Pokot, Jumatano walifanya tambiko la kuwalaani watu ambao wanadai wamekuwa wakiwachochea vijana wa Gen Z kupigana na serikali ya Kenya Kwanza.

Bila kutaja majina, wazee hao ambao walichinja ndume katika kijiji cha Kachang’uya  eneo la  Masol, kaunti ndogo ya Pokot ya Kati waliandaa maombi ya kitamaduni kumuombea Rais William Ruto na amani iwe nchini Kenya.

Kwenye sherehe iliyofana na kuvutia mamia ya wakazi, wazee hao waliwasha moto, kuchoma nyama na kuketi kwenye mviringo wakiwa wameweka matawi mbele yao kwa jina Kriket wakila nyama.

Baadhi ya wazee ambao walikuwa wamevalia mavazi ya kitamaduni waliongoza tambiko hilo wakiwa wameshika mishale na matawi wakisema sala kwa lugha ya Kipokot huku umati ukiitikia.

Wazee wafanya tambiko kwa kuchoma nyama katika kijiji cha Kachang’uya, eneo la Masol, kaunti ndogo ya Pokot ya kati. Picha|Oscar Kakai

Wazee hao walirusha fimbo ambayo iliashiria kuwa kumkana shetani ambaye ‘amewachanganya’ vijana nchini.

Wakiongozwa na mzee Samuel Kamar, wazee hao walisema kuwa wamekerwa kutokana na maandamano ambayo yanaendelea kote nchini.
“Kuna watu ambao wanasukuma vijana na ndio sababu tumeandaa tambiko kulaani wale ambao wanawachochea. Hatujataja majina lakini hatujafurahia tabia yao,” alisema.

Alisema kuwa joto la kisiasa limepanda na kuathiri maendeleo nchini.

“Wakati kuna mapigano, kila mtu ataumia hata kina mama vipofu. Tumeshuhudia jinsi vita viliharibu mataifa ya Rwanda, Sudan na Uganda ndio sababu tuko na hofu,”alisema.

Anasema kuwa Rais William Ruto anafaa kupewa nafasi kuongoza Kenya.

Karimo Lodia, mzee mwingine, alisema kuwa wamekerwa na vijana ambao wanamsumbua Rais.

“Ruto ni Mkalenjin na hatutaki ghasia na wachochezi kumharibia uongozi,” alisema.

Alimtaka Rais kupuuza kelele ambayo inaendelea na badala yake kuendelea kuhudumia Wakenya.

“Tunamwambia Ruto kuketi na kutulia,” alisema.

Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye alihudhuria sherehe hiyo alisema kuwa wamefanya mashauriano na wazee kuhusu uongozi wa nchi huku wakiwalaumu wale ambao wanapanga kupindua serikali.

“Tulifikiri lalama zilikuwa kuhusu mswada wa fedha lakini imegeuka kuwa mambo mengine na haja ya kupindua serikali ambayo iliwekwa na Wakenya. Kuna watu wametumia vibaya vijana wa Gen Z bila wao kujua Hata baada ya Rais kutupilia mbali mswada huo,vijana bado wanataka kuwa Rais aondoke ofisini,” alisema.

Mzee akisema sala ya tambiko katika kijiji cha Kachang’uya, eneo la Masol, kaunti ndogo ya Pokot ya kati. Picha|Oscar Kakai

Bw Lochakapong alisema kuwa anamuunga mkono kwa dhati Rais akisisitiza kuwa bado atamtetea.

Alikashifu vikali wale ambao wanapanga na kufadhili maandamano akiongeza kuwa Kenya iko kwenye mkondo mzuri.

“Wacha wangoje hadi 2027 ama 2032. Tunaunga mkono Rais Ruto kwa asilimia 100. Dola imeshuka na shilingi imepanda. Kenya imebadilika na hakuna vile mtu atapata uongozi kupitia mlango wa nyuma bila kufuata katiba ya nchi. Uchumi umeimarika lakini kuna wale ambao hawajafurahia,” alisema.

Aliwatahadharisha vijana dhidi ya kutumia vibaya mitandao huku akiwasuta wale watu ambao hakutaja kwa majina kwa kufadhili vijana kutekeleza maovu.

“Kenya ikiharibika kila mtu ataathirika. Rais yuko tayari kusikiza. Kulikuwa na hamasisho na wadau kushirikishwa kabla ya mswada wa fedha kuletwa. Ni nini mnataka ikiwa hamtaki mazungumzo? Tunataka kujua ni nani ambaye yuko na vijana hao. Wengine ni wanasiasa, mashirika ya kijamii na wanabiashara. Tunataka kuwajua na lengo lao lijulikane,” alisema.

[email protected]