Makala

Tambua kwa nini asali ya mkokoni imekolea utamu kuliko ya maeneo mengine

April 30th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

ASALI ni zao la nyuki ambalo tangu jadi linasifika kwa utamu wake.

Hutengenezwa na wadudu hao kutoka kwa mkusanyika au mchanganyiko wa vimiminika vyenye sukari nyingi, hasa ile itokayo kwenye mimea ya maua.

Nyuki huhifadhi asali katika sega kwa minajili ya kuwatolea chakula.

Licha ya asali kijumla kuwa na sifa za utamu, wakazi wa Lamu bado wanaamini hakuna asali tamu kuliko ile ya kutoka kwa miti au misitu ya mikoko.

Mikoko ni aina za miti au vichaka vinavyokua katika maji ya chumvi, hasa kwenye fukwe za bahari za kanda za trokipi.

Kaunti za Pwani, hasa Lamu, zinasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya misitu ya mikoko kutokana na kupakana kwake na Bahari Hindi.

Mzee Twaha Omar,78, mkazi wa kisiwa cha Pate kilichoko Lamu Mashariki, anashikilia kuwa asali kutoka kwa maua ya miti ya mikoko ndiyo kusema kwa utamu kinyume na ile itokanayo na maua ya miti mingine yoyote ile.

Bw Omar anafafanua kuwa kama vile miti yoyote mingine ya matunda huchanua maua, mikoko pia iko na maua ambayo hukomaa na kisha kugeuka kuwa matunda madogo ya kijani kibichi.

Bw Omar anasema nyuki mara nyingi hupendezwa na kuvutiwa sana kukusanya vimiminika vipatikanavyo kwenye maua hayo ya mikoko kwa minajili ya kutengeneza asali.

Bw Swaleh Abdalla akiwa amevalia gwanda tayari kuvuna asali kwenye mizinga aliyoitega ndani ya msitu wa mikoko eneo la Chukuchu, kisiwani Pate, Lamu Mashariki. Wakazi wa Lamu wanasema asali ya mikokoni ni tamu kushinda nyingine yoyote ile. Picha|Kalume Kazungu

Anaitaja asali ya mikoko kuwa ya kipekee kutokana na kwamba mazingira inayoundiwa na nyuki ni asili zaidi ikilinganishwa na sehemu zingine zozote.

“Tunapenda sana asali ya mikoko. Ni tamu kushinda zote. Ni ya asili. Kwanza mazingira yenyewe inayoundiwa na nyuki ni yenye uasilia wa kipekee. Ni mikoko inayokua yenyewe kwenye fukwe na maji ya Bahari Hindi ambayo hayajaathiriwa na mchanganyiko wa kemikali zozote zile,” akasema Bw Omar.

Swaleh Abdalla,26, mfugaji nyuki mashuhuri eneo la Chukuchu lililoko ndani ya msitu wa mikoko, Lamu Mashariki, anasema sababu ya kimsingi inayowasukuma kuipenda sana asali ya mikokoni ni kutokana na rangi yake iliyokoleza weusi.

Bw Abdalla anasema kuwepo kwa mikoko mingi na maua, kumefanya ni rahisi kwa nyuki kutengeneza asali nyingi na yenye ukwasi wa virutubishi na kwa muda mfupi zaidi.

“Twaipenda asali ya mikokoni. Huwa imekoleza weusi kinyume na asali ya miti mingine. Mbali na utamu wake, mchanganyiko uliokolea wa asali ya mikokoni pia hutusaidia sana tunapoutumia kama tiba asili ya maradhi mbalimbali,” akasema Bw Abdalla.

Bi Rafa Aboud,50, anauelezea upekee wa asali ya kutoka mikokoni, akitaja kuwa huwa na utamu unaoambatana na unyevunyevu na mguso wa aina yake kinywani mwa mlaji, hivyo kumwacha akiwa ameridhika na kuburudika.

Mizinga ya nyuki ikiwa imetundikwa kwenye mikoko ndani ya msitu eneo la Chukuchu, kisiwani Pate, Lamu Mashariki. Picha|Kalume Kazungu

“Nimeonja asali karibu aina zote katika maisha yangu. Utapata hata kumbe kuna asali chungu, hasa ile ambayo nyuki wataitengeneza kutokana na maua ya miti kama vile mwarobaini. Lakini hii ya mikokoni imenifanya kuganda kwayo kama kigaga. Ni tamu si haba na ni tiba pia,” akasisitiza Bi Aboud.

Naye mjuzi wa tiba asili eneo la Milimani ndani ya msitu wa Boni, Lamu Mashariki, Ali Abdi, anasema asali ni suluhu ya ugumba (infertility), hasa kwa wale wanaokosa ashiki chumbani.

“Hapa msitu wa Boni sisi huipenda sana asali. Inaamsha hisia au ashiki ya kitandani si haba, iwe ni kwako wewe mwanamume au mwanamke. Tunapokunywa vijiko kadhaa kabla ya kwenda kulala mambo huwa yanakuwa bambam,” akasema Bw Abdi.

Lakini je, ni kweli asali, ikiwemo hii inayosifiwa ya mikokoni ni tiba? Je, ni nini hasa faida za asali mwilini?

Wataalamu wa Afya na Lishe Bora waliozungumza na Taifa Leo walitaja asali kuwa chakula muhimu na cha faida tele za kimsingi, hasa kwa siha ya binadamu.

Daktari na Mtaalamu wa Lishe Bora katika kituo cha afya cha Bluenile Mkoroshoni Medical Centre, Kaunti ya Kilifi, Duncan Amani Chai, anataja asali kuwa suluhu ya haraka ya kuponya vidonda, hasa vile vitokanavyo na wagonjwa kujipata wamelala mahali pamoja kwa muda mrefu.

Asali ikiwa imehifadhiwa kwenye chupa tayari kuuzwa mjini Mombasa. Picha|Kalume Kazungu

Dkt Chai anashikilia kuwa ingawa haijafanyiwa vipimo vya kitaalamu kuthibitisha ubora wake katika kutibu maradhi mbalimbali, yeye binafsi yuko na ushuhuda, hasa kwa wateja wake mbalimbali wanaofika kituo chake cha matibabu kutibiwa, hasa wale wa vidonda kwa kutumia asali.

“Kuna wagonjwa wa vidonda wanaofika hapa wakiwa wamekata tamaa ya vidonda vyao kupona. Tumewaosha kwa kutumia asali na kisha kuwapaka hiyo hiyo asali. Asali hukausha na hata kuponesha kidonda haraka. Ni tiba ya msingi, hasa kwa vidonda kama tunavyoshuhudia wenyewe hapa kituoni,” akasema Bw Chai.

Dkt Chai pia anataja asali kuwa suluhu ya mafua au kukohoakohoa.

Anasema kupitia kutumia mchanganyiko wa asali, wengi, ikiwemo yeye mwenyewe, wameshuhudia mafua yakipotea au kuondoka kabisa.

“Wenye mafua washaelewa wazi kwamba suluhu mwafaka ya maradhi hayo ni asali. Punde unapotumia kijiko kimoja hivi cha mchanganyiko wa asali utapata mafua yakiondoka masaa au dakika chache baadaye. Hutaona tena chafya za ovyo ovyo au kuvimba koo,” akasema Dkt Chai.

Naye Mtaalamu wa Lishe kisiwani Lamu, Bi Maryam Ali, anasema asali ikichanganywa na mdalasini kwenye chai na kisha mja kunywa husaidia pakubwa kuondoa maumivu ya viungo na uvimbe mwilini-yaani Arthritis.