Afya na Jamii

Tambua kwa nini wanaume wakongwe hawafai kuwa na homoni za juu za kiume

May 7th, 2024 2 min read

NA CECIL ODONGO

KIWANGO cha juu cha homoni za kiume (testerone) miongoni kwa wanaume wazee kunawaweka kwenye hatari ya mpigo wa moyo kupanda katika kiwango cha hatari, Watafiti wamebaini.

Kuongezeka kwa mpigo wa moyo kunazuia kuenea vyema kwa damu sehemu mbalimbali za mwilini na kunaweza kusababisha mauti haraka kwa wanaume ambao wametinga umri wa miaka 70 na zaidi.

Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la kimatibabu la eclinical unaonyesha kuwa wanaume ambao huathirika na hali hii ni wale ambao wana mafuta mengi mwilini.

Kibayolojia, kiwango cha homoni za kiume huwa kinapungua mwanaume anapoingia uzeeni. Hata hivyo kutokana na tofauti ya jeni, hali ya kiafya na mtindo wa maisha, kuna wale ambao homoni hizo hupanda licha ya ukongwe wao na hapo ndipo utafiti wa sasa unaonyesha hatari unatokea.

Watafiti waligundua kuwa wanaume ambao wana unene kupita kiasi ndio huathirika sana na kupanda kwa kiwango cha homoni za kiume.

Katika utafiti huo, ilibainika kuwa kiwango cha juu cha homoni za kiume husababisha mishipa kutanuka sana kisha hubana njia za kusafirisha damu mwilini. Wanaume waliohusishwa katika utafiti huo ni wale wanaotatizwa na maradhi mbalimbali hasa magonjwa ya kansa na ya moyo.

Katika utafiti huo, ilibainika kuwa wanaume ambao wana umri mkubwa na huathirika na mpigo wa moyo si lazima wawe wakiugua ugonjwa wa moyo, kansa ya tezi dume ama magonjwa mengine ambayo huathiri wanaume wakongwe.

Hata hivyo, kwa kuwa uzee huandamana na magonjwa mengi, hilo halina maana kuwa wanaougua saratani, kisukari au magonjwa ya moyo hawawezi kukosa kiwango cha juu cha homoni za kiume kwenye hali yao.

Hata hivyo, wakati wa utafiti huo, ilibainika kuwa hali hiyo ya kupanda kwa kiwango cha homoni za kiume si ya kurithiwa kutoka kizazi kimoja au kingine au ukoo bali hutokana na mtindo wa maisha ya mwanaume husika na takwimu zinaonyesha huwa haiathiri wanaume wengi.

Pendekezo katika utafiti huo ni kuwa tafiti nyingine zitakazofanywa zinastahili kutoa takwimu za wanaume wazee ambao wameangamia kutokana na hali hii.

Hii ni kwa sababu utafiti wa sasa haukutoa idadi ya wale ambao waliangamia na mikakati inayostahili kukumbatiwa kuhamasisha wanaume kuhusu mbinu za kuepukana na hali hii.