Afya na Jamii

Tambua ugonjwa wa ‘appendicitis’ unaonyemelea watu kimya kimya

March 5th, 2024 3 min read

NA WANGU KANURI

KAREN Nyambura anakumbuka kuwa mnamo mwezi wa Septemba mwaka wa 2008, alianza kuhisi uchungu mwingi upande wa kulia chini ya tumbo.

Maumivu yale, yalizidi tu pindi tu siku zilisonga huku akihisi kama sehemu ile imeanza kufura. Zaidi na hayo, Bi Nyambura anaeleza kuwa uchungu huo ulimlemaza akashindwa kufanya chochote.

“Niliamua kufika hospitalini kwa sababu sikuwa ninajua ni kwa nini nilihisi maumivu kiasi hicho. Baada ya vipimo kadha wa kadha, nilielezwa kuwa ni kidole cha tumbo (appendix) langu kilichokuwa kimefura,” anakumbuka.

Ilimbidi afanyiwe upasuaji wa mara moja ili kiungo hicho kitolewe huku madaktari wakimweleza kuwa angechelewa kutibiwa, hicho kidole cha tumbo lake kingepasuka.

“Hii ni kwa sababu, kilikuwa kimefura na kujaa usaha,” anasema.

Jinsi maradhi ya ‘kidole cha tumbo’ Kimombo, appendicitis yanavyofanana tumboni. Picha|Hisani

Ugonjwa huu hutokea baada ya kiungo hicho kinachoambatanishwa na utumbo mkubwa (large intestine) kufura (appendicitis).

Kwa mujibu wa Dkt Gideon Kiprono, mtalaamu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Olenguruone, ugonjwa huu humwathiri mtu mmoja kati ya watu 1,000 huku watu wenye umri wa miaka 10 hadi 30 wakiwa kwenye hatari zaidi.

“Kijinsia, ugonjwa huu huwaathiri wanaume zaidi ikilinganishwa na wanawake kwa takribani mara 1.4,” anaongezea.

Japo chanzo cha ugonjwa huu bado hakijabainika, wataalamu wa afya wamehusisha ugonjwa huu na mtu kutokwa na kinyesi kilicho kigumu, kufura kwa tezi (lymph nodes) na kwa nadra sana, kuwepo na vifaa mwilini. Isitoshe, bakteria pia husababisha ugonjwa huu inapokua kwa kingi.

Dkt Kiprono anasema kuwa mgonjwa wa kidole cha tumbo huonyesha dalili kama kuhisi uchungu kwenye kitovu na sehemu ya chini ya tumbo.

“Kutapika au kuhisi kichefuchefu. Hii hutokea pindi tu baada ya kuanza kuhisi uchungu. Mgonjwa pia hukosa hamu ya kula, akawa anahisi joto jingi na hata kukaukiwa aendapo msalani au hata anapoendesha,” anafafanua Dkt Kiprono.

Dalili hizi hujionyesha chini ya saa 48 kwa angalau asilimia 80 ya watu wazima. Hata hivyo, nyingi ya dalili za mgonjwa wa kidole cha tumbo huweza kufananishwa na magonjwa mengine kama maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), ugonjwa wa bakteria wa njia ya uzazi (PID), na maumivu wakati wa yai kutoka kwenye ovari (ovulation).

Pia, Dkt Kiprono anaeleza kuwa dalili za appendicitis huiga ugonjwa unaosababisha madini na chumvi zenye asidi kushikamana na kusababisha mkojo uliokolea rangi ya manjano (kidney stones) na maambukizi kwenye tumbo yanayosababisha kutapika, kuhisi joto jingi, kichefuchefu na kuendesha (gastroenteritis).

Hali kadhalika, ugonjwa huu unaweza ukatibiwa kwa kufanyiwa upasuaji au hata bila. Dkt Kiprono anasema, mgonjwa anapofanyiwa upasuaji, sehemu hiyo iliyofura ya kidole cha tumbo hutolewa kabla haijapasuka.

Dkt Gideon Kiprono, mtalaamu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Olenguruone. Picha|Hisani

“Upasuaji huu huenda ukafanywa kwa kukata sehemu kubwa la tumbo la chini (open surgery) au kwa kukata kidogo na kutumia vyombo maalum kama kamera kuona na kuondoa sehemu iliyofura (laparoscopic surgery).”

Katika visa nadra sana, mgonjwa wa kidole cha tumbo huweza kumeza dawa za antibiotiki pekee na akapata nafuu. Hata hivyo, Dkt Kiprono anaeleza kuwa ni muhimu kujua kuwa kidole cha tumbo kinaweza kupasuka wakati wa anapotumia antibiotiki na kusababisha madhara makubwa kama kuambukiza tumbo la ndani.

“Kama upasuaji wowote ule, kutolewa kidole cha tumbo kupitia upasuaji huwa na hatari ya kupata maambukizi kwenye tumbo la chini, kutokwa na damu baada na wakati wa upasuaji, viungo vilivyo karibu kuumizwa na mgonjwa akawa na kidonda,” anasema Dkt Kiprono.

Hata hivyo, anapofanyiwa upasuaji wa laparoscopic, mgonjwa huweza kurejea nyumbani kwake ndani ya siku moja au mbili na hata akarejea kazini mwake baada ya wiki moja au mbili.

“Anapokatwa sana, mgonjwa huyo hukaa hospitalini kwa siku tatu hadi tano na akachukua muda wa wiki mbili hadi nne akipona.”
Dkt Kiprono anashauri kuwa mgonjwa huyu anapaswa kumuona daktari baada ya wiki moja kuangalia iwapo kidonda kinaendelea kupona inavyofaa.

“Anapaswa pia kurejea kufanya kazi zake za kila siku pole pole na kuziongezea anapoendelea kupata nafuu. Fuata ushauri wa daktari wako iwapo unataka kufanya mazoezi yoyote yale,” anaongezea.