Maoni

Tamko la Rais kuhusu ndege za Kenya Airways linaweza kuathiri kampuni hiyo kibiashara

May 28th, 2024 1 min read

NA JUMA NAMLOLA

BAADA ya kupotea kwa siku kadhaa, nimerejea ukumbini nikiwa na maswali chungu nzima kuhusu suala ambalo limeibua gumzo mitaani.

Lakini kabla ya kuuliza maswali yangu, kama kawaida, nina ngano fupi. Hii ni ngano hadithi, si ngano inayotengeneza unga wa chapati.

Bwana mmoja kwa jina Bwanaheri aliwahi kuishi miaka ya awali ya kuingia kwa Waarabu na Wareno Pwani ya Kenya. Bwanaheri alikuwa masikini, maisha yake yalikuwa ya kuungaunga.

Lakini alipenda sana na alitamani kuwa na maisha mazuri. Maisha ya anasa, kuwa na pesa, mamlaka na kuheshimiwa kwa kuwa na vitu vizuri.

Kwake nyumbani kulikuwa na mkeka uliochakaa. Kwa kuwa alikuwa ameanza kujifunza mambo ya dini, alipewa mkeka mpya na watu waliotembelea eneo lake, akawa anatumia wakati wa swala.

Mkeka huo pia aliutumia kulalia kwenye kitanda chake cha mwakisu

Bwanaheri akaona heri imemjia. Akautupa ule mkeka wake wa zamani.

Baada ya kama wiki mbili, wale wageni walipokuwa wakiondoka kwenda kupiga kambi eneo jingine, wakaomba wachukue mswala wake. Masikini Bwanaheri akabakia bila mkeka wake wa zamani.

Ndipo wahenga wakamuonya na kuonya ulimwengu kwa jumla kwamba usiache mbachao kwa mswala upitao.

Sina mamlaka ya kumkosoa wala kumwelekeza Rais William Ruto. Lakini kauli yake ya Jumapili kwamba shirika la ndege la Kenya Airways ni ghali kuliko ndege aliyotumia kwenda Marekani inatoa picha gani kuhusu kilicho chetu?

Kama Kenya Airways ni ghali, serikali ingetafuta mbinu za kufanya bei yake iwe sawa na mashirika mengine ya ndege. Kutangaza hadharani, kunaweza kufanya shirika hilo lililoanza kupata faida liporomoke.

Kama ambavyo Kenya Airways ni The Pride of Africa, yatupasa kuhimiza wengi kusafiri na ndege zake!