Makala

TAMU CHUNGU: Kadhia ya kufanya biashara na serikali

March 30th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI inadaiwa deni la Sh128.88 bilioni na wanakandarasi wa humu nchini, waliopewa tenda ya kuiuzia bidhaa na kusambaza huduma.

Deni hili linasemekana ni la tangu mwaka wa 2013.

Ucheleweshwaji huu wa wakandarasi kulipwa umetajwa kama mojawapo ya kizingiti kikuu cha maendeleo nchini.

Kulingana na Kiragu Chege kutoka Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara na Viwanda nchini, KNCCI, serikali ya kaunti ya Nairobi inadaiwa Sh64.8 bilioni, Mombasa Sh3.705 bilioni, Kisumu Sh2.047 bilioni, Wajir Sh2.619 na Nakuru Sh 2.379 bilioni.

Kaunti zingine zinazodaiwa na wanakandarasi ni Meru ambayo ina deni la Sh2 bilioni, Kwale Sh1.830 bilioni, Narok Sh1.725 bilioni na Nyeri Sh1.411 bilioni, huku Nandi na Nyamira zikidaiwa Sh1.394 na Sh1.349 bilioni, mtawalia.

Bw Chege pia anasema wizara na idara mbalimbali za serikali kuu ziko kwenye orodha hii. Wizara ya Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali inaongoza kwa deni la Sh4.52 billioni, Ugatuzi Sh2.55 billioni na idara ya Upangaji Sh2.55 bilioni. Idara zingine zinazohusishwa na wizara ya usalama zinasemekana kudaiwa Sh1.8 bilioni, huku wizara ya ardhi, nyumba na ukuaji wa miji Sh1.693 bilioni.

“Ucheleweshwaji wa wanakandarasi kulipwa na serikali kuu umedumu kwa muda wa miaka mitano iliyopita. Baadhi ya madeni ya serikali za kaunti ni ya kuanzia 2013,” anaeleza Chege.

Kulemaza shughuli muhimu

Anasema suala hili limelemaza utendakazi wa kampuni na mashirika ya humu nchini yaliyopewa kandarasi, jambo ambalo limechangia kujikokota kustawi kwa uchumi.

Aidha, wafanyakazi wa wanakandarasi wameishia kulemewa na gharama ya maisha ikizingatiwa kuwa hawapati mshahara. “Unapofanya kazi unapaswa kulipwa. Mapato hayo unayalipa wanaokutegemea, lakini katika kisa hiki serikali ikisusia kulipa wanakandarasi madeni yanaendelea kuongezeka na ndiyo yanakwamisha ukuaji wa maendeleo,” Bw Chege akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano.

Seneta wa Nyeri, mhandisi Ephraim Maina ambaye pia ni mwekezaji katika kampuni ya ujenzi, ya Kirinyaga, anasema ukosefu wa kulipa wanakandarasi umekwamisha utendakazi wa biashara.

“Rekodi ya wenye mikopo katika benki imepakwa tope kwa kushindwa kuilipa, na hata kufunga biashara zao kwa ajili ya kufilisika,” anasema Bw Maina.

Ni kufuatia changamoto hizi ambapo KNCCI imejiri na mapendekezo yanayolenga kutahadharisha biashara ndogondogo na zile za wastani (MSMEs) wakati zinashiriki biashara na serikali, hasa kuhusu kucheleweshwa kwa malipo. Mapendekezo hayo yamedokeza athari zinazokodolea macho MSMEs pamoja na kutoa mwelekeo wa sheria za kuzitatua.

Bw Chege ameambia Taifa Leo utafiti ulioshinikiza kubuni sheria hizo maalum, unapendekeza wakandarasi kulipwa pindi wanapokamilisha usambazaji wa bidhaa na huduma. Sheria hizo zinapendekeza kulipwa kwa muda wa siku 30 baada ya usambazaji.

Endapo juhudi za sheria hizo hazitazaa matunda, Chege anasema bodi tawala ya ununuzi wa mali ya umma inapaswa kubuniwa ili kushurutisha serikali kulipa wanakandarasi riba. Anaeleza kuwa Hazina ya Kitaifa inafaa kutathmini na kurekebisha kipengele cha 33 cha sheria za ununuzi wa mali ya umma, 2015, ili kushinikiza ulipaji wa malipo ya kwanza katika usambazaji wa bidhaa au huduma.

Anaongeza kuwa kuna idara ambazo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameibua maswali, baadhi ya wawekezaji wakipuliza kipenga cha ufisadi kusakatwa katika idara ambazo hazijashuhudia ufujaji wa fedha. Anafafanua kuwa baadhi ya MSMEs zinapata kandarasi ya kusambaza bidhaa na huduma bila kufuata sheria za tenda, hivyo basi kusababisha kucheleweshewa malipo.

Katika tenda ambazo hakuna ubadhirifu wa fedha, zote zinapigwa msasa na mchakato mzima wa utoaji kandarasi unakosa imani kwa umma na wawekezaji. “Wanakandarasi wengi huwa na stakabadhi zinazopaswa kujazwa kabla ya kuuza bidhaa na kusambaza huduma. Lakini idara za serikali zinakosa kufuata kanuni za kutoa tenda, na hii inatia wanakandarasi hao katika hatari ya kupigwa marufuku uchunguzi unapofanywa,” anaeleza Bw Chege.

Mwenyekiti wa mfumo wa Nyumba Kumi, na ambaye amewahi kuhudumu kama msimamizi wa sekta ya utendakazi wa hoteli, Bw Joseph Kaguthi, anasema Hazina ya Kitaifa ifanye hima kupiga msasa tenda zote za serikali kuu na za serikali za kaunti ambazo hazijalipwa.

“Licha ya wamiliki wa MSMEs kupata fursa ya kufanya biashara na serikali, wamepitia changamoto nyingi. Uchunguzi ufanywe ili wenye uwazi kupata tenda walipwe bila kucheleweshewa haki yao,” anasema Kaguthi.

Mdau huyu anaunga mkono wakandarasi kulipwa malipo ya kwanza pindi wanaposambaza bidhaa na huduma. Kwa sasa wanakandarasi wa ujenzi wa miundomsingi kama barabara ndio wanalipwa kwa awamu. Kaguthi anasema kufanya kazi na serikali imekuwa ghali kwa sababu wanaoisambazia bidhaa na huduma wanalazimika kutumia fedha zao katika kipindi kizima za kandarasi.

Katika ripoti yake ya kila mwaka, Benki Kuu ya Kenya 2017 ilikiri kuna baadhi ya biashara zilifilisika na zingine kupitia wakati mgumu kuimarika kwa kukosa pesa, kiini kikuu kikiwa serikali imekwama na fedha zao.

Aidha, kufuatia kukawia kulipwa, ripoti hiyo pia ilidokeza kwamba baadhi ya biashara zililemewa kulipa mikopo benkini pamoja na rekodi yao ya fedha kuishia kuwa yenye doa.

Mwaka 2017 sekta za kibinafsi zilitajwa kuwa na mkopo wa Sh234.5 bilioni, hii ikiwa ongezeko la asilimia 54.3 kutoka mwaka 2016.

Dhamana iliyotumiwa na biashara nyingi kuchukua mikopo iko katika hatari ya kunadiwa, huku nyingi zikiorodheshwa katika CRB kwa kushindwa kulipa.