TANA RIVER: Kafyu vijijini polisi wakimsaka raia wa Italia aliyetekwa nyara

TANA RIVER: Kafyu vijijini polisi wakimsaka raia wa Italia aliyetekwa nyara

Na STEPHEN ODUOR

ZAIDI ya vijiji vitano katika kaunti ya Tana River vimewekewa vizuizi vikali huku polisi wakiendelea kumtafuta mwanadada Mwitaliano aliyetekwa nyara Kilifi na kutoroshewa kaunti hiyo.

Wakazi wa baadhi ya vijiji eneo bunge la Tana Delta wamepigwa marufuku kusonga hata karibu na mto Tana, hivyo basi kuwazuia kufikia mashamba yao, ambayo kufikia sasa wanahofia yameharibiwa na viboko na yonda.

Njaa kwa upande mwengine yazidi kuwakodolea macho ya ujasiri, kwani sasa wamelazimika kula mboga za mwituni na chakula cha akiba ili kujikimu, chakula ambacho kila kunapokucha kinazidi kupungua kwenye maghala.

“Ili kufikia mashamba yetu yafaa tuvuke mto, na ufanya hivyo hata nyakati za jioni ili tukayachunge yasiharibiwe na kiboko na nyani, lakini sasa hatuwezi kwa sababu maafisa wa usalama wamekuwa wakali sana,” anaeleza Ibrahim Hakoka, mkulima.

Miezi michache imepita tangu gharika kuvuruga mashamba yao, walijitahidi baadaye na kupanda tena ila mazao yao yaliharibiwa na viwavi jeshi pindi tu, yalipoanza kukomaa.

Walidhani matatizo yao yamekwisha, lakini mambo kangaja tu, ghafla magaidi wakamteka nyara mwanadada Mwitaliano maeneo ya Kilifi na kumtoroshea Tana River kama inavyokisiwa, jambo ambalo sasa limewafanya wote washukiwa, na mahabusu manyumbani mwao.

“Wametuharibia sana, majuma matatu hatujaweza kuona mashamba yetu maana hatuaminiki, twaonekana kama wahalifu, tumekuwa mahabusu kwetu,” alilalama mzee huyo.

Hapana unga, wala mchuzi kwa wakazi wa Maziwa na viungo vyake, watu hao, sasa wamesalia kutegemea mboga za mwituni, maharagwe na pojo zilizopo kwenye maghala yao.

Kuingia katika miji hiyo imekuwa kama kuvuka boda, kila anayefika anatakiwa kuwa na kitambulisho, na awe na uwezo wa kutambua rais wa nchi, gavana wa kaunti, na zaidi ya watu watatu kutoka kijiji hicho, mbali na kutambuliwa na mzee wa kijiji hicho.

Uhuru wa kutembea umewekewa vikwazo vya saa, huku wakazi wakitakiwa kutoka makwao saa moja asubuhi na kuwa nyumbani kabla ya saa kumi na mbili jioni.

Sherehe za harusi za usiku na matanga zimepigwa marufuku.

“Leo ukileta mwili kuzika kesho hata mziki huwezi cheza usiku haturuhusiwi kuimba wala kuketi nje, nyote na mwili mwakaa ndani, kimya kama mfu mwenyewe ama kuimba kwa kunong’ona,” anasimulia Joseph Malibe.

Biashara vile vile zimetatizika, serikali ya kaunti imeshindwa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara eneo hilo, kwani hali iliyopo haiwaruhusu wakusanye ushuru kufika eneo hilo kwa kuhofia kuhangaishwa na maafisa eneo hilo.

Wafugaji nao hawajasazwa, wao huvamiwa hata usiku wa manane na kuamshwa kwa oparesheni za misako ya mara kwa mara, huku maafisa hao wakidai kuwa na taarifa ya kuwepo kwa wahalifu.

Wanasema kuwa misako hiyo hufanywa zaidi ya mara mbili kwa wiki moja, huku baadhi yao wakishikwa na kuwekwa korokoroni kwa siku kadhaa.

“Wako kila mahali, wametusakama sana, watoto na wake zetu wanaishi kwa hofu, wakija wanatandika mpaka wanyama wetu, huwezi kutembea huru hapa, ole wako ikiwa hapa na huwezi kuzungumza Kiswahili, hapo utakielewa tofauti,” anasimulia Badhru Dado Bile, mzee wa kijiji. Utovu wowote wa nidhamu hata kujibizana na wanajeshi hukabiliwa vikali,kwa kichapo, kuruka au kuogelea mavumbini, ni sharti kutii.

Viongozi katika kaunti wamelalamika kuhusu mateso wanayopitia wakaazi, huku wakirai maafisa wa usalama kulegeza kamba na kuwahurumia wakaazi hao.

Viongozi hao wakiongozwa na gavana Dhadho Godhana waliwaomba naafisa hao kuwaruhusu wakaazi hao kulisha mifugo ya kwa amani na wanaovua kuvua kwa amani.

Ni mahangaiko haya ambayo yamewafanya wakaazi kuongea na viongozi wao, huku wakiomba kupewa fursa ya kusaidia katika msako.

“Tumehangaika sana, ni heri tupewe nafasi tuingie msituni tutafute hao watu, maana inasemekana ni wafugaji, na wamekuja huku, sisi tunaelewa hapa vizuri zaidi, tumalize hii shida mara moja,” alisema Aden Bakero, mkaazi wa Jire.

Kamishna wa kaunti Bw Oningo’i Ole Sossio naye alisema kuwa hapana marufuku iliyowekwa kwa jamii zinazotegemea uvuvi, Ila oparesheni iliyopo maeneo hayo imetokana na taarifa za ujasusi.

Kuhusu wakaazi waliojitolea kusaidia kwa msako, Bw Olesosio alisema kuwa ni swala la kuangaliwa na kujadiliwa kwa upana.

“Ni vyema kusikia kuwa wako na nia ya kusaidia, ila lazima nasi tujadiliane ili tusije tuafanya maamuzi ya kuongeza maadui kikosi msituni,” alisema.

Hata hivyo,Sylvia Romano angali mikononi mwa mahasidi, vijiji vya Tana River vikiwa chini ya ulinzi mkali wa wanajeshi na vikosi vya polisi, baadhi ya wakaazi wakiishi kwa hofu, na wengine wakihisi usalama zaidi.

You can share this post!

Wakulima wakerwa na serikali kuwacheleweshea fidia

Kisura atolewa uzuzu na mama ya kalameni

adminleo