Makala

TANA RIVER: Maji yageuka bidhaa ghali baada ya mafuriko

May 14th, 2018 2 min read

Na STEPHEN ODUOR

KAUNTI ya Tana River inakumbwa na uhaba wa maji safi baada ya gharika kugubika na kuharibu mitambo ya kusambaza maji maeneo ya Madogo, Mwa Tana na eneo bunge la Tana Delta.

Zaidi ya watu elfu sitini katika kaunti hiyo wanazidi kukosa huduma hiyo muhimu, huku takriban watu 20,000 kati yao wakiwa ni wakazi wa mji wa Madogo.

Wakazi wa Madogo wanakadiria wiki tatu za kiu ya kukata koo sasa tangu kuharibika kwa mitambo ya kusambaza maji katika kampuni ya maji ya Madogo (MAWASCO).

Wakazi hao wamelazimika kuchota maji katika vidimbwi vilivyosimama baada ya mafuriko, huku wengine wakinunua kwa watu wa mikokoteni wanaouza mtungi mmoja wa lita ishirini kwa Sh30.

Akizungumza na Taifa Leo katika eneo la Madogo, Bi Fatuma Bona Gafo alielezea kuwa mji huo ulikuwa umekosa maji kwa muda mrefu sana kinyume na matarajio ya wananchi, na hivyo kuwalazimisha kununua maji kwa wachuuzi, huku wengine wakielekea vidimbwi.

“Hatuna la budi, kama huwezi kununua maji kwa wachuuzi kwa Sh30 kwa kila mtungi wa lita 20, basi utachota kwa vidimbwi vya barabara,” alisema.

Hali hiyo pia imekumba mji wa Bura ambapo zaidi ya watu 30,000 wamekuwa wakiishi katika hali hii kwa muda wa miezi mitatu sasa.

Inakisiwa kuwa baada ya kuharibika kwa mitambo ya kusambaza maji katika eneo hilo, wakazi wamebaki kuchota maji katika kidimbwi kimoja cha shirika la unyunyizaji mashamba maji (NIB).

Wakazi hao walidai kuwa juhudi zao kuirai serikali ya kaunti na hata serikali kuu kuangazia swala la mitambo hiyo hazijafua dafu, kwani mpaka sasa hawajapokea majibu mbali na wazee wa jamii kutuma ombi la kutaka swala la maji lishughulikiwe.

“Tumeteta, tumesema na tukaandika barua zaidi ya moja swala hili liangaziwe, lakini mpaka wa leo twazidi kuhangaika, “alisema Hassan Gwiyo, mkazi wa Bura.

Wakazi hao wangali wanazidi kuchota maji ya kidimbwi hicho, ambacho zaidi ya mara moja kimekuwa chimbuko cha ugonjwa wa kipindupindu.

Tana Delta nayo haijasazwa kwani hata huko, maelfu ya watu wanazidi kuhangaika wakitafuta maji safi ya kunywa baada ya mitambo ya kusambaza maji ya Garsen kuzamishwa kwenye maji ya mafuriko.

Zaidi ya watu elfu ishirini wanaotegemea huduma za mitambo hiyo wamesalia hoi, huku wakiomba msaada wa serikali ya kaunti katika kutatua janga linalowakumba.

Katibu Mkuu wa Afya Bi Mwanajuma Habwoka hata hivyo aliielezea Taifa leo kuwa mbali na kuwa mtambo wa Madogo ulikuwa na hitilafu, maji ya kutoka kwenye tangi hizo hayakuwa safi kwa afya ya mwanadamu.

Bi Mwanajuma alisema kuwa maji hayo yalishukiwa kuathirika na hivyo hayakuwa sawa kwa watu kunywa.

“Tunashuku kuwa maji hayo ya Madogo yameathirika kwa njia fulani na tumeitisha vifaa vya kuopima kutoka Mombasa ili tuweze kutathmini kabla ya kufanya usambazaji wowote,” alisema.

Hata hivyo alisema kuwa serikali ya kaunti ilikuwa imetoa magari ya maji tano kwa ajili ya wakaazi wa Madogo, huku mengine yakiwekwa kusaidiabkatika usambazaji maji maeneo ya Tana Delta na Galole.

Haya yanajiri wakati ambapo hofu ya mchipuko wa kipindupindu inazuka, huku mtu mmoja akishukiwa kufa eneo la Madogo na wengine saba wakiripotiwa kutibiwa na kupewa fursa ya kwenda nyumbani.