Makala

TANA RIVER: Masaibu ya mabinti punguani

September 24th, 2018 3 min read

NA STEPHEN ODUOR

NI watu ambao jamii imewaweka kisogoni katika nguzo nyingi za maisha. Kila waonekanapo huepukwa kama ukoma ilhali wao ni wanadamu sawa na wengine, tofauti ikiwa tu kwamba ni walemavu wa akili.

Wakati wa mchana wao huepukwa mitaani, ila wakati wa usiku hujipata katika mashaka na kuishia kuwa chombo cha mapenzi kwa watu fulani mitaani.

Katika kaunti ya Tana River, sio jambo geni kumwona mwanadada mwenye akili punguani, akiwa amevalia viraka akimnyonyesha mtoto karibu na mapipa ama mbele ya maduka.

Huwabembeleza wanao na kuwalinda, huku wakiomba omba mtaani kuwapa wanao lishe bora.

Wanawake, wanaume na watu mashuhuri huwapa jicho tu, na wakati mwingi kutowatilia maanani wanapowapita kwenye taabu zao.

Swali ambalo mpaka wa leo halijapata jibu ni jinsi wanawake hawa hupata uja uzito.

Asha ni mojawapo ya wanawake wenye akili punguani. Alikuja mitaani pasipo nguo ya kumfinika kikamilifu, na alisaidiwa kujifunika uchi na wasamaria wema.

Alikuwa punguani mwenye maneno mengi, na hakusita kuangua kilio pasipo sababu kamili.

Kila alipotembea alikuwa na lalama chungu nzima, sio akina shangazi, sio marafiki, sio serikali sio mbwa wa kutangatanga, aliishi kulaani kila alipotembea hadi pale, angeliketi chini kula.

“Sisi tulimpa nguo hapa, mara ya kwanza kumuona mtaani alikuwa tupu tupu. Nguo zilikuwa zimefunika pande kidogo tu za mwili lakini baadhi ya uke ulijianika nje,” alieleza Bi Stacy Moraa, mfanyabiashara wa kuuza nguo.

Alikuwa na umri wa kati ya miaka 27 na 35, mwili ulonenepa na mweupe wa rangi, wengi walimtania kwa kumwita “manyanga”.

Kila kulipodunda ngoma, mwanadada huyu alitingika kwa kweli na kuwavutia wengi kwenye sinema za bure, huku wakimchangia vijipesa kidogo kidogo kumpa motisha.

Maskani yake yalikuwa milango ya duka, majumba yaliyokuwa yakiendelea kujengwa, na wakati mwingine hata chini ya mti.

“Hakuna aliyejua alikuwa anatoka wapi mbali na fununu kuwa kabla ya kuja hapa Tana River, alikuwa Garissa,” alieleza Amina Shime, mkazi wa Tana River.

Baada ya mwaka mmoja na nusu wa kuhangaika huku na kule, watu mtaani walipigwa na butwaa kumwona Asha na mabadiliko mwilini. Alikuwa mja mzito.

Wengi walistaajabu huku wakijiuliza maswali kujaribu kubaini aliyemtia dada yule uja uzito, kwani hawangedhani mtu mwenye akili timamu angemtamani kimahaba.

Lakini hakuna aliyeguswa kumshughulikia na kumpeleka hospitali za watu wenye ulemavu wa akili ili asaidiwe, wote mtaani walisalia kumtazama akiilea mimba ile kwa kuombaomba.

“Tulikuwa twamwona akipita pita, hatukujua tufanyeje, ila akija akuombe, wampa tu, ukihisi amekugusa, wajitolea angalau ale kitu,” alieleza Petro Jilo, mwendeshaji pikipiki.

Mara Asha akapotea ghafla, na alipoonekana kwa mara nyingine alikuwa amevalia nadhifu, rinda, na lesso kiunoni amejifunga kibwebwe, mkononi amebeba mtoto mchanga.

Mji ulipigwa na butwaa, huku wanawake wenzake wakimsogea na kumdanganya kwa chakula ili waweze kumwona mwanawe mtanashati.

“Alikuja akiwa safi, hakuna aliyejua alikotoka wala yaliyojiri alikoenda, watu walitaka tu kumwona mtoto wake, “alisimulia Petro Jilo.

Alihangaika na mwanawe kwa muda wa miezi minne, aking’ang’ana kuombaomba mitaani ili kumpa chakula, wahisani wachache walijitokeza kumletea lishe, na wengine kumfariji kwa hela na wakati mwengine nguo za mtoto.

Hata hivyo safari ya mahangaiko ilifikia mwisho pale wasimamizi wa walemavu katika kaunti walipomchukua Asha na kumuunganisha na watu wa kwao, waliomkubali na kumpa usaidizi uliostahili.

Sio yeye tu ambaye amepitia hali hii, kwani miji ya Tana River inazidi kushuhudia wengi kama yeye.

Walemavu wa kiakili katika Kaunti ya Tana River haswa wa kike wanadhulumiwa kimapenzi na kuachwa katika hali ya sintofahamu.

Kufikia sasa, takriban wanawake kumi wenye ulemavu wa akili wako katika miji ya kaunti hiyo, baadhi yao wakiwa wanalea watoto wachanga.

Kulingana na Mwenyekiti wa Walemavu katika kaunti ya Tana River, Said Babwoya, walemavu hao wana familia zao, ambazo zimewatelekeza na kuwaacha kwa meno makali ya ulimwengu.

“Wengi wa hawa wanawake unawaona mitaani wana kwao, wana familia zao na wanawaona kila siku, lakini sasa wamewaachilia kuteseka mjini,” alieleza.

Hata hivyo kundi la maendeleo ya wanawake linajitahidi kuwasaidia baadhi yao waja wazito, kwa kuwatafutia matibabu spesheli, na hata kuwaunganisha wengine na familia zao.

“Tumeingia mjini kujaribu kuwasaidia wenzetu ambao hawako sawa kiakili, maana tumeona jinsi ambavyo wanadhulumiwa kimwili, kwa kubakwa na kupewa uja uzito, ni jukumu letu kuwavisha nguo na kujisitiri na aibu hizi kama wanawake, “alieleza.

Huku hali akiendelea kuzorota na wachache kujitahidi kufanya bidii kuyaboresha, afisi ya walemavu sasa imeiomba serikali ya kaunti kuwatengea makao walemavu hao, ili kuwaepusha na hujuma dhidi yao na hata magonjwa ya zinaa.