Makala

TANA RIVER: Miundomsingi mibovu ndicho kiini cha wanafunzi kupata 'D'

August 13th, 2018 2 min read

NA STEPHEN ODUOR

BAADHI ya shule za upili katika kaunti ya Tana River zinakumbwa na uhaba wa miundo misingi, inayodaiwa kuchangia matokeo duni kwenye mitihani ya kitaifa.

Mkurugenzi wa elimu katika kaunti, Bw Gitonga Mbaka alisema baadhi ya shule ziliandikisha matokeo duni haswa katika masomo ya sayansi kwa kukosa maabara.

“Matokeo duni katika sayansi yamechangiwa sana na ukosefu wa maabara katika shule zetu,wanafunzi hukutana na vifaa hivyo wakati wa mtihani tu, ambapo huwa taabu kubwa, “alisema Bw Mbaka.

Katika mtihani wa kitaifa mwaka 2017, ni wanafunzi 12 tu katika kaunti nzima waliofanikiwa kujiunga na vyuo vikuu kwa masomo ya diploma na digrii.

Biolojia, Fizikia na Kemia ni baadhi ya shule yaliyoshuhudia matokeo duni zaidi, huku shule bora ikipata alama ya D Hasi na D mtawaliwa.

Masomo ya Kingereza, Kiswahili na Kilimo yalitarajiwa sana kufana kuliko mengine, lakini kwa mshangao yaliandikisha alama ya D mtawalia, sawia na masomo ya sayansi, jambo ambalo limewatia walimu na wahisani wengine wasiwasi mkubwa.

Bw Mbaka alisema kuwa mbali na kukosa miundo misingi, baadhi ya wanafunzi walikwisha jenga dhana potovu kwa masomo mengine, na hivyo hawakuvutilia maanani kama ipasavyo.

Hata hivyo alishangazwa sana na jinsi wanafunzi hao mbali na kuzingatia dini sana,jitihada hizo hazikuwa zikidhihirika kwenye mtihani.

“Ukiangalia kwa makini matokeo ya baadhi ya shule, ni somo la kiarabu tu ndilo wafanyalo vizuri, hata somo la dini I. R. E wanalianguka kisawasawa mpaka tunashindwa kuelewa tatizo liko wapi,”alisema kwa mshangao.

Bw Mbaka pia alieleza kusikitishwa sana na matokeo ya baadhi ya shule za kitaifa zilizopigiwa upato mkubwa kutoa matokeo bora, kwani matarajio yalikuwa yakija kinyume, mbali na kuwa shule hizo zilikuwa na vifaa vyote kikamilifu.

Kwa upande mwengine Bw Mbaka aliwalaumu wazazi katika kuchangia pakubwa matokeo duni, kwani hawakuhusika moja kwa moja na masomo ya watoto wao.

Alisema kuwa wazazi mbali na kuwa na dhana hasi katika elimu, walichelewa kulipa karo, hawakujali watoto wao wakikaa nyumbani mradi tu wafanye mtihani, na pia hawakujituma kikamilifu katika ujenzi wa miundo misingi katika shule husika.

“Kuna kiwango cha serikali, na pia kuna kiwango cha wanafunzi na kile cha wazazi, wazazi wamezembea nkatika wajibu wao, na wanafunzi nao wakafuata mkondo huo huo,” akasema.

Hata hivyo alisema mkutano huo uliowahusisha walimu wa vyuo vya upili, haswa wanaofunza masomo ya sayansi ulinuia kubadilisha mkondo wa matokeo katika kaunti hiyo.

Alifafanua kuwa itabidi kubadili mtindo wa kufunza kuanzia muhula wa tatu, ili kuwaandaa wanafunzi kwa mtihani unaowakabili kwa kuwaongoza katika marudio, na kuwafunza jinsi mitihani ya kitaifa hunakiliwa, na jinsi ya kuandika majibu kwenye karatasi za mtihani.

“Tunahisi kwamba kuna siri ambayo wanapaswa kuijua, hasa watahiniwa wa mwaka huu, na ni bora tuwaelezee mwanzo wa muhula huu ili tuepuke aibu ya kuvuta mkia nchini kila mwaka, ” alisema.

Hata hivyo amewataka wanafunzi watahiniwa kushirikiana kwa karibu na walimu wao,ili kubadili matokeo duni ambayo yameshuhudiwa kwa miaka ya hapo awali.