Habari Mseto

Tandaza ataka wakazi Dongo Kundu wafidiwe

March 6th, 2019 1 min read

Na Fadhili Fredrick

WAKAZI zaidi ya 256 kutoka vijiji sita katika eneobunge la Matuga, watakaoathirika na ujenzi wa awamu ya tatu ya barabara ya kisasa ya Dongo Kundu, bado hawajafidiwa.

Mbunge wa eneo hilo, Bw Kassim Tandaza, sasa anataka serikali iwafidie waathiriwa hao kabla ya mradi kuanza.

Alisema licha ya orodha hiyo kupewa mamlaka husika miaka minne iliyopita, waathiriwa hao hawajafidiwa mashamba na mimea yao.

“Tayari mwanakandarasi wa Kichina yuko eneo la ujenzi na wakazi walioathirika bado hawajapokea fidia yoyote,” akasema.

Alisema wale wanaopaswa kulipwa kwa ardhi na mali zao ni pamoja na wanakijiji kutoka Mkumbi, Tuliani hadi kiijiji cha Kibundani na waathiriwa wengine pia.

Pia anataka wenyeji kupewa kipaumbele katika nafasi za ajira katika mradi huo.