Tangatanga Pwani wakata tamaa ya kuunda chama, wataingia UDA

Tangatanga Pwani wakata tamaa ya kuunda chama, wataingia UDA

Na MOHAMED AHMED

BAADHI ya wanasiasa wa Pwani ambao wanamuunga mkono Naibu Rais William Ruto na waliokuwa wanasukuma mpango wa kuunda chama cha Pwani sasa wametangaza kuachana na mpango huo na badala yake kuamua kuingia chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Wakati wa ziara yake ya Pwani wikendi, Dkt Ruto alionekana wazi kuchukua usukuni wa chama hicho kinachohusishwa naye na kuwataka viongozi wa eneo hilo kuingia UDA.

Baada ya ombi lake hilo, viongozi hao wa kikundi cha Tangatanga walitangaza kuwa mipango yao ya kuunda chama cha Pwani sasa imeporomoka.

Waliwalaumu magavana Amason Kingi (Kilifi) na Hassan Joho (Mombasa) kwa kuteka mipango hiyo na wakasema sasa wataunga mkono chama cha UDA.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Mohammed Ali (Nyali) na aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar. Walisema kuwa wataingia kwenye chama hicho.

Dkt Ruto pia alimtaka Bw Baya awe katibu mkuu wa chama hicho na asaidie katika kuandika manifesto yake.

“Mimi ninataka kumwambia Owen Baya kuwa yeye ni msomi na kwa sababu hiyo aje aunge hiki chama cha toroli (wilbaro) ili tuweze kutembea pamoja. Mimi sina shida kabisa kwa sababu kuja kwake kutasaidia masuala ya Pwani kutatatuliwa,” akasema Dkt Ruto.

Alisema kuwa yeye anataka kushikana na watu ambao watakuwa washirika wake na si wafuasi tu.

Wabunge hao wanaomunga mkono Dkt Ruto walisema kuwa mipango yao ya kuunda chama cha Pwani iliharibika baada ya kuvurugwa na magavana Hassan Joho na na Amason Kingi.

“Mapema mwaka huu 2021 tulianza mipango ya kuunda chama na kuunganisha Pwani lakini Bw Joho akaleta ukiritimba na kutatiza mipango hiyo lakini tunawaambia kuwa si mwisho wa safari. Saa hii tutatembea na toroli,” akasema Bw Ali.

Bi Jumwa naye alisema kuwa washikane na Dkt Ruto na kuhakikisha kuwa anapata Urais ili Pwani ipate ukombozi. Vilevile, aliwakejeli Bw Joho na Kingi kuhusiana na mipango yao ya kuunganisha Pwani.

Sisi tunataka kuwaambia waache kutupotezea wakati. Mwanzo Joho anapaswa kuondoka makwapwani mwa Raila alafu ndio atuunganishe na aende kuwania urais kama alivyotangaza,” akasema.

Viongozi wengine wanaomuunga mkono Dkt Ruto ni pamoja na Benjamin Tayari (Kinango) Athman Shariff (Lamu East), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Lydia Haika (Taita Taveta), Paul Katana (Kaloleni) miongoni mwa wengine ambao walikuwa wameandamana naye.

You can share this post!

Utepetevu Kenya Power ulivyoiletea familia mahangaiko

TAHARIRI: Madai kuhusu SGR yawekwe bayana