Habari

'Tangatanga' wakosoa kukamatwa kwa Aisha Jumwa

October 16th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wamekosoa kukamatwa kwa Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa akihusishwa na vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mwanamume nyumbani kwa mgombea wa ODM katika wadi ya Ganda, Kaunti ya Kilifi.

Wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Uasin Gishu Gladys Shollei, wabunge hao wapatao 15 walidai Bi Jumwa alikuwa ameenda kuuliza ni kwa nini mgombea wa ODM Reuben Katana alikuwa akiendesha kampeni nyumbani kwake baada ya muda rasmi wa kampeni kuisha.

“Mbona Bi Jumwa anakamatwa ilhali alikuwa akipinga kampeni ambazo zilikuwa zikiendeshwa kinyume cha sheria baada ya polisi kudinda kuchukua hatua dhidi ya wafuasi wa ODM?” akahoji Bi Shollei kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano.

Wabunge wengine waliokuwa pamoja naye ni; Lydia Haika (Mbunge Mwakilishi wa Taita Taveta), Rahab Mukami (Mbunge mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nyeri), Kimani Ichungwa (Kikuyu), Didmus Barasa (Kimilili), Ndindi Nyoro (Kiharu), na Rigathi Gachagua (Karatina) miongoni mwa wengine.

 

Baadhi ya viongozi wanaoegemea upande wa ‘Tangatanga’ wakati waliandaa kikao na wanahabari Oktoba 16, 2019, katika majengo ya bunge. Picha/ Charles Wasonga

Wabunge hao walisema haikuwa haki kwa polisi kumkamata Bi Jumwa kutokana na vurugu za kisiasa ilhali hawajachukua hatua zozote dhidi ya wabunge wa ODM ambao walichochea fujo katika eneobunge la Kibra.

“Je, Jumwa anakamatwa kwa sababu yeye ni mwanamke? Mbona polisi hawajawakamata wabunge wanaume waliozua ghasia juzi Kibra kwa kukodi wahuni walioharibu gari la mgombea wa Jubilee McDonald Mariga?” akauliza Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Wangui Ngirici.

“Bi Jumwa hakuua mtu kwa sababu tujuavyo ni kwamba hana bunduki wala leseni ya kumiliki silaha kama hiyo,” akaongeza.

Naye Bw Barasa alimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kuamuru kukamatwa kwa wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), Junet Mohamed (Suna Mashariki), Simba Arati (Dagoretti Kaskazini) na aliyekuwa Mbunge wa Embakasi Kusini Irshad Sumra kwa kuchochea fujo katika eneobunge la Kibra.