HabariSiasa

Tangatanga wakunja mikia

August 1st, 2019 2 min read

WAANDISHI WETU

WANASIASA ambao wamekuwa wakimpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022, maarufu kama Tangatanga, wameingiza baridi kutokana na mbinu zinazotumiwa na Serikali kuwanyamazisha.

Mbinu hizo ni pamoja na vitisho vya kuwafungulia mashtaka ya ufisadi, kuzima miradi ya maendeleo maeneo yao na kufadhili wapinzani wao kuwakabili kwenye uchaguzi ujao.

Baadhi ya walio katika Tangatanga wanadai kushtakiwa kwa magavana Ferdinand Waititu wa Kiambu na Moses Lenolkulal wa Samburu kwa madai ya ufisadi kunatokana na kuwa wako kwenye kambi ya Dkt Ruto.

Baadhi yao waliozungumza na Taifa Leo wamelazimika kunyamaza kutokana na vitisho wanavyopata kutoka kwa maafisa wakuu serikalini, ambao wana nia ya kumzima Dkt Ruto asimrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Wengi ambao wamejipata katika hali hiyo ni wanasiasa kutoka Kati, Kisii, Magharibi na Pwani.

Kati ya viongozi hao ni Mbunge wa Kandara, Alice Wahome, ambaye amesema kuwa serikali inapanga njama za kumnyamazisha kwa kumfungulia kesi mahakamani.

Mwenzake wa Kiharu, Ndindi Nyoro, naye amedai kuna njama za kumkamata kwa madai ya matumizi mabaya ya Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) ili kumnyamazisha.

Kuomba radhi

Katika kile kinachoonyesha kuwa Tangatanga wanakunja mkia, wiki iliyopita Mbunge wa Sirisia, John Waluke aliitisha kikao cha habari kuomba msamaha kwa kutoa matamshi yaliyoonekana kumharibia sifa Bw Odinga.

Naye Mbunge wa Kilifi, Owen Baya, amerejea katika kambi ya Bw Odinga baada ya kuwa katika upande wa Dkt Ruto kwa muda.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, Mwakilishi wa Wanawake, Bi Wangui Ngirichi pia amenyamaza akisema kuwa “dalili si nzuri kwa sasa.”

Katika eneo la Kisii, wabunge waliomuunga mkono Dkt Ruto pia wamenyamaza ama kubadilisha misimamo yao.

Katika Kauti ya Nyamira, Mwakilishi wa Wanawake, Bi Jerusha Momanyi na Mbunge wa Borabu, Ben Momanyi wamehamia kambi ya Dkt Matiang’i kutoka kwa ile ya Naibu Rais.

Hata hivyo, Dkt Ruto bado anaungwa mkono na wabunge Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini) na Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi).

Katika Kaunti ya Kisii, Mbunge wa Kitutu Chache, Richard Onyonka pia ameondoka katika kambi ya Dkt Ruto na kutangaza kumuunga mkono Dkt Matiang’i.

Waziri huyo pia anaungwa mkono na wabunge Richard Tong’i (Nyaribari Chache), Samuel Arama (Nakuru Magharibi), Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache), Zadoc Ogutu (Bomachoge Borabu), Seneta Sam Ongeri na Mwakilishi wa Wanawake Janet Ong’era.

Mbunge wa Mugirango Kusini, Sylvanus Osoro, ndiye anayeonekana kuwa mtu pekee wa Dkt Ruto katika Kaunti ya Kisii.

Kulingana na mdadisi wa siasa Gachucha Gachanja, onyo la Rais Kenyatta kwa wanaoendeleza siasa limezima Tanga Tanga huku akidhibiti ngome yake ya siasa.

“Baada ya onyo kali la Rais kuhusu Tangatanga, viongozi waliingiwa na baridi na kupatia Kieleweke ujasiri wa kujiendeleza Mlima Kenya,” alisema Bw Gachucha.

Hata hivyo, alisema ni mapema mno kupuuza Tanga Tanga akisema huenda kundi hilo linajipanga upya.

Ripoti Za Justus Wanga, Kamau Wanderi, Ndungu Gachane Na Benson Matheka