Habari Mseto

'Tangatanga' wakutana kuhusu BBI

January 27th, 2020 1 min read

Na WAANDISHI WETU

WANACHAMA zaidi ya 150 wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, Jumapili walielekea Naivasha kupanga mikakati kuhusu ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Imebainika mkutano huo utakaokamilika leo Jumatatu umepangiwa kutafuta mbinu za kukabiliana na athari za kisiasa zilizosababishwa kwao na mikutano ya uhamasisho ya BBI inayoongozwa kitaifa na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Kupitia mkutano huo unaofanyika katika Hoteli ya Lake Naivasha, wanasiasa hao wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wamenuia kutafuta msimamo mmoja kuhusu ripoti ya BBI.

“Tumeamua kuandaa mkutano ili tuelewane kuhusu mikutano ya BBI na kama masuala yote ya wafuasi wetu yamejumuishwa kwenye ripoti,” akasema Mbunge wa Soy, Caleb Kositany.

Aliongeza kwamba wangali wanasubiri ratiba rasmi ya uhamasisho itakayotolewa na jopo la BBI linaloongozwa na Seneta Yusuf Haji.

“Sisi pia tuna lengo la kuandaa mikutano yetu ya uhamasisho,” akasema Bw Kositany.

Wabunge mbalimbali waliohojiwa na ‘Taifa Leo’ walisema wanataka kukusanya mapendekezo yao ambayo watawasilisha kwa jopo la Bw Haji.

Kufikia Jumapili jioni, wabunge karibu 120 kutoka Mlima Kenya, Rift Valley, Magharibi na maeneo mengine ya nchi walikuwa wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo.

Imefichuka kwamba, ijapokuwa baadhi ya wandani wa Dkt Ruto walihudhuria mkutano wa BBI jijini Mombasa mnamo Jumamosi, kuna mpango wa ‘Tangatanga’ kuzuru maeneobunge yasiyopungua 200 kueneza misimamo yao kuhusu mchakato huo.