Tangatanga wapinga vikali mswada wa BBI

Tangatanga wapinga vikali mswada wa BBI

WINNIE A ONYANDO na CHARLES WASONGA

MJADALA kuhusu Mswada wa Mageuzi ya Katiba chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI), jana uliendelea katika Bunge la Kitaifa na Seneti huku wabunge wa tangatanga wakdhalilisha shughuli hiyo wakisema sio ya dharura wakati huu.

Lakini wabunge wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walishabikia kupitishwa kwa mswada huo, jinsi ulivyo, wakisema mapendekezo yaliyomo yanashughulikia changamoto kadha zinazoikumba nchi.

Wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Aisha Jumwa (Malindi), Glady Shollei (Uasin Gishu), Cecily Mbarire (Mbunge Maalum) miongoni mwa wengine walisema, bunge lilipaswa kujadili changamoto zinazowakumba Wakenya kama vile janga la Covid-19, baa la njaa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Wabunge hao, ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto, pia walidai mswada huo utawaongezea Wakenya gharama kupitia kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi na idadi ya maeneo bunge kutoka 290 hadi 360.

“Mswada huu hauna maana kwa Wakenya wakati huu. Lingekuwa jambo la busara ikiwa kikao kama hiki kingeitishwa kujadili jinsi Wakenya watapata chanjo, chakula na mahitaji mengine ya kimsingi. Aliye na njaa ni mwenye hasira,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge huyo pia alionya kuwa, wakazi wa Nyeri watapinga mswada huo wa BBI kwa sababu kaunti hiyo iliachwa nje katika ugavi wa maeneo bunge 70 mapya yanayopendekezwa.

Bw Gachagua alitaja hatua hiyo kama ubaguzi ambao unalenga kuwafukarisha watu wa Nyeri.

“Wale ninaowawakilisha hawana sababu ya kuunga mkono mswada huu kwa sababu umewabagua na hivyo kuwasukimia umasikini zaidi. Rasilimali za kitaifa hugawanywa kwa misingi ya maeneo bunge lakini hatujaongezewa eneo bunge lolote,” akasema Bw Gachagua.

Kwa upande wake, Bi Mbarire alisema mswada huo ni hatari kwa sababu unadhoofisha uhuru wa Idara ya Mahakama kupitia uteuzi wa afisi ya kupokea malalamishi kuhusu majaji, maarufu kama “ombudsman”.

“Ikiwa mswada huo utapitishwa, majaji watakuwa watumwa wa afisi ya rais ambayo ndio itateua afisa wa kupokea malalamishi dhidi yao. Hii itaathiri shughuli za utoaji wa haki mahakamani,” akaeleza.

Awali, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) Muturi Kigano alipuuzilia mbali wabunge waliotaka mswada huo ufanyiwe marekebisho akisema, madai yao hayana mashiko kikatiba.

Wengine waliounga mkono mswada huo ni wabunge Opiyo Wandayi (Ugunja), Jeremiah Kioni (Ndaragua), Chris Wamalwa (Kimimini), Zulekha Hassan (Mbunge mwakilishi wa Kwale), miongoni mwa wengine.

Katika Seneti, wajumbe waligawanyika kuhusu mswada huo huku wale wa mrengo wa tangatanga wakishiniza ufanyiwe mabadiliko huku wenzao wa kieleweke wakishinikiza upitishwe ulivyo.

Sawa na wenzao wa bunge la kitaifa, maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aaron Cheruiyot (Kericho), na Mithika Linturi (Meru) walisema kuna vipengele hatari katika mswada huo ambavyo vinapaswa kurekebishwa.

Hadi tulipokuwa tukienda mitamboni, wabunge na maseneta hawakuwa wamepiga kura kuhusu mswada huo. Hata hivyo, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alidokeza kuwa huenda mjadala huo ukaendelea Jumanne wiki ijayo.

You can share this post!

Murathe sasa apotosha bunge kuhusu wizi wa mabilioni ya...

Watatu wafariki lori na matatu zikigongana mjini