Habari

'Tangatanga' warai Rais ataje chaguo lake kura za 2022

January 28th, 2020 2 min read

ONYANGO K’ONYANGO na MWAMUYE MORGAN

WANDANI wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta auheshimu muafaka ulioratibu kuwa yeye atakaa mamlakani kwa mihula miwili kisha amuunge mkono naibu wake.

Viongozi hao walimshasuri Rais atangaze msimamo wake ikiwa atamuunga mkono Dkt Ruto mwaka wa 2022 au la. Walitangaza hadharani kuwa mpango huo usiposimamiwa vyema, utasababisha mtikisiko wa kisiasa.

Wakiongozwa na mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome, viongozi hao walisema kuwa ahadi ya Rais na Naibu wake bado ipo na lazima iheshimiwe.

Wakiongea wakati wa misa ya kutoa shukrani Jumapili katika kanisa la St Marys Kipkaren eneobunge la Turbo, viongozi hao wa mrengo wa Tanga Tanga waliapa kutokubali mtu ‘wa nje’ kumshauri Rais kutomuunga mkono Naibu wake mwaka 2022.

“Umefikia wakati ambao Rais anafaa kutangaza kwa umma msimamo wake juu ya atakayemrithi. Baadhi yetu bado tunafuata ahadi aliyotoa mwaka wa 2013 kuwa angeongoza miaka 10 yake na mingine kumikwa William Ruto. Ninavyojua, hakujakuwa na mabadiliko katika ahadi hiyo,” akasema Bi Wahome.

Aliongezea kuwa hawataruhusu mwanasiasa yeyote kumdharau Dkt Ruto, na wale wanaopanga kutatiza malengo yake ya kuwa rais watajipata taabani.

Viongozi hao walieleza hofu yao kuhusu uwezekano kuwa kinara wa mrengo wa ODM, Bw Raila Odinga anamshauri Rais aende kinyume na ahadi aliyotoa.

Walisema kuwa Bw Odinga amenyakua BBI kwa nia ya kujiweka katika nafasi nzuri ya kisiasa mwaka 2022, badala ya kuunganisha nchi.

“Hii mikutano ya BBI imeleta michakato mingi sana. Rais anafaa kuwa mwangalifu sana akiwa na Raila kwa sababu mambo tuliyoyasikia katika mkutano wa Mombasa unaeza kupeleka nchi katika enzi za Kanu,” alisema mbunge wa Endebess, Bw Robert Pukose.

Hisia zake ziliungwa mkono na Seneta wa zamani wa Kakamega Bw Bony Khalwale na mbunge wa Kapseret Bw Oscar Sudi wakisema kuwa mikutano ya BBI ilianza ili kumtenga Dkt William Ruto ila kwa kuwa sasa wandani wa Naibu wa Rais wamejiunga na mikutano hii hivyo basi wandani wa Raila wanatafuta njia mbadala za kummaliza Naibu wa Rais kisiasa.

Wandani wa Naibu wa Rais wameapa kuwa wataunga mkono BBI iwapo itafufua uchumi wa Taifa ambao walidai inadidimia na kama ni ya kuunda nafasi mpya tu wataipinga vilivyo.

“Ikiwa BBI haiwezi toa suluhu kwa shida zinazokumba nchi hii kama kufufua uchumi ambao unadidimia na ikiongeza ukosefu wa ajira, bei duni ya mahindi na maziwa basi hakuna haja ya BBI.Umoja wa taifa ni wakati uchumi wa taifa umeimarika,” alisema mwakilishi wa wanawake kaunti ya Uasin Gishu, Bi Gladys Shollei.

Hisia zake ziliungwa mkono na mwenzake wa Kirinyaga, Bi Purity Ngiciri aliyerudia yaliyosemwa akidai mjadala wa BBI unafaa kutumika kuangazia shida zinazokumba nchi hii na sio kuwapigia debe wanasiasa fulani.

Bwana Khalwale alisema kuwa pesa zinazotumiwa katika hamasisho la BBI katika sehemu tofauti za nchi zinafaa kutumika kuunda nakala za ripoti ili kusambazwa kwa wananchi.

“Raila anazunguka nchi nzima akiwaalika watu kwa mikutano yake ili kutoa maoni yao juu ya ripoti ya BBI, je mtu atatoaje maoni kuhusu kitu ambacho hajakisoma?” alisema Bw Khalwale.