Habari

Tangatanga wasalimu amri

January 26th, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA na MOHAMED AHMED

WABUNGE na viongozi wanaomuunga Naibu Rais William Ruto, maarufu kama ‘Tangatanga’, hatimaye wamesalimu amri na kukubali kuunga kura ya maamuzi kama njia ya kutekeleza ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Jumamosi, wabunge hao walihudhuria mkutano wa kujadili ripoti hiyo mjini Mombasa na kutangaza kuwa ni lazima mapendekezo yake yafanywe kupitia kura ya maamuzi.

Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, alisema kwa sababu inapendekezwa kubuniwe wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wawili, ni lazima kufanyike kura ya maamuzi.

“Ili kuwepo na Waziri Mkuu na manaibu wawili ilivyopendekezwa, ni lazima twende kwa kura ya maamuzi,” alisema Bw Murkomen.

Wanachama wengine wa ‘Tangatanga’ waliozungumza akiwemo seneta wa Nakuru Susan Kihika, pia walionekana kubadilisha msimamo wao.

Huo ulikuwa mkutano wa kwanza wa BBI kuhudhuriwa na wafuasi wa Ruto. Walisusia mkutano wa kwanza kaunti ya Kisii na wa pili katika kaunti ya Kakamega wakisema, mikutano hiyo ilikuwa ya kuharibu pesa za umma kwa sababu hakuna aliyekuwa akipinga BBI.

Hata hivyo mnamo Jumanne, walitangaza kuwa watakuwa wakihudhuria mikutano yote ya BBI.

Jumamosi, wanachama wa ‘Tangatanga’ eneo la Pwani wakiongozwa na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Likoni Mohamed Ali pia walihudhuria mkutano huo.

Kwenye mapendekezo yao, viongozi wa Pwani walisema kwamba, wanataka mfumo wa utawala wa majimbo katika eneo hilo.

Katika mkutano wa Jumamosi wa BBI jijini Mombasa ambao uliongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga, viongozi wa Pwani waliwasilisha matakwa wanaotaka yazingatiwe kupitia BBI.

Akisoma mapendekezo ya Pwani kwa niaba ya viongozi hao wengine, gavana wa Kilifi Amason Kingi alisema kuwa kuna haja yakuwa sehemu mbili za kanda ya Pwani.

“Tunataka Pwani hii igawanywe na iwe na wasimamizi wa Pwani ya upande wa juu na ule wa chini,” akasema Bw Kingi.

Katika mgawanyo huo, kaunti za Taita Taveta, Mombasa na Kwale ziwe katika upande wa Pwani ya chini na kaunti za Lamu, Kilifi na Tana River ziwe katika jimbo la Pwani ya juu.

Aidha, viongozi hao pia waliunga kupanuliwa kwa serikali kuu ambayo itakuwa na nafasi ya Rais na Waziri Mkuu ambaye atakuwa na manaibu wake wawili.

Suala la ardhi lilikuwa miongoni mwa masuala makuu ambayo wakazi wa Pwani wanataka yaangaziwe katika BBI.

Bw Odinga alisema majimbo ni jambo ambalo litazingatiwa katika BBI.

“Viongozi wa Pwani kama vile Ronald Ngala walipigania mambo haya. Yale matakwa yenu sio mara ya kwanza kutajwa lakini mara hii yatatekelezwa,” akasema Bw Odinga na kutaja suala la ardhi kama donda sugu ambalo lazima litatuliwe.

Bw Wetang’ula alisema ni lazima mapendekezo ya BBI yatekelezwe mwaka 2020.

Gavana wa Mombasa, Hassan Joho pamoja na seneta James Orengo nao pia waliunga kura ya maamuzi ifanyike mwaka huu.

Vilevile, Bw Orengo alitaja kama miujiza hatua ya seneta Kipchumba Murkomen kukubali kura hiyo.

Bw Murkomen ambaye ni miongoni mwa wandani wa Naibu Rais William Ruto aliongoza viongozi wa Tangatanga katika mkutano huo na kusema kuwa kuna haja ya kufanyika kwa kura hiyo ya maamuzi.