Habari Mseto

'Tangatanga' wataka vijana wasio na kazi walipwe

January 28th, 2020 2 min read

VALENTINE OBARA na MACHARIA MWANGI

WANASIASA wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wamerushia vijana ndoano huku wakijiandaa kuanza mikutano yao ya hadhara kuhamasisha umma kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kwenye makubaliano waliyotoa Jumatatu baada ya kukutana mjini Naivasha, wanasiasa hao wa kikundi cha ‘Tangatanga’ walisema wanataka BBI ijumuishe pendekezo la kuwalipa vijana ruzuku wanapokosa ajira.

Viongozi hao wanataka kila mwaka, asilimia tano ya mapato ya kitaifa itengewe mpango walioutaja kama ‘Kazi kwa Vijana’ kuwasaidia vijana wanaokamilisha shule kwa miaka mitano mfululizo wanapotafuta ajira.

Kando na hayo, wanataka asilimia nyingine tano ya mapato ya kitaifa iwe ikitengewa hazina ya kuwapa maskwota makao, kiasi sawa na hicho kiende kwa hazina ya kusaidia wakulima na nyingine tano kwa hazina ya kusaidia vijana, walemavu na wanawake kuwekeza kibiashara.

Wandani hao wa Dkt Ruto vile vile wanataka asilimia isiyopungua 3.5 ya mapato ya kitaifa itengewe hazina ya mahakama ili idara hiyo isishikwe mateka na Afisi ya Rais.

Akizungumza Jumatatu baada ya mkutano wa siku mbili katika hoteli ya Lake Naivasha Resort, Kiongozi wa wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen alisema ingawa watapanga mikutano kuhamasisha umma kuhusu mapendekezo yao, hawataifanya wakati mmoja na mikutano inayosimamiwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet alisema nia yao ni kufikia wananchi wengi zaidi wala si kuleta ushindani.

Mkutano wa hadhara

Wanapanga kufanya mkutano wa kwanza wa hadhara Nakuru ambapo wamepanga kualika viongozi kutoka pande zote akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, Dkt Ruto na Bw Odinga.

Wengi wao waliohudhuria mkutano wa BBI uliofanywa Mombasa wikendi iliyopita hawakupewa nafasi kuhutubia umati.

Bw Murkomen alisema bado watahudhuria mikutano mingine ambayo Bw Odinga anatarajiwa kuongoza katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya zamani.

Alizidi kusema, watachangisha fedha za kupanga mikutano yao na hawatatumia pesa za mlipa ushuru.

Kulingana naye, mikutano wanayopanga italenga kusikiliza mapendekezo ya raia wa kawaida wala si wanasiasa, huku akiomba jopo la BBI kutoa ratiba ya vikao vyao vya awamu ya pili.