HabariSiasa

'Tangatanga' wazidi kubanwa

May 12th, 2019 2 min read

Na NDUNG’U GACHANE

VIONGOZI wa kisiasa wa kundi la ‘Tangatanga’ linalomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, wanaendelea kujioata pabaya baada ya kupuuza agizo la Rais Uhuru Kenyatta kutaka kampeni za mapema zisitishwe.

Imebainika viongozi wanaoegemea upande wa Rais Kenyatta, almaarufu kama ‘Kieleweke’, sasa wameanzisha mikakati ya kuwaondoa wandani hao wa Dkt Ruto kwenye kamati za Bunge la Taifa na Seneti.

Haya yamefichuka wiki chache baada ya wanasiasa wa Tangatanga kulalamika kwamba baadhi yao walipokonywa walinzi. Baadaye teuzi zilizofanywa na Rais katika usimamizi wa mashirika ya umma zilionekana kutuza watetezi wa Kieleweke.

Juma lililopita, iliripotiwa kwamba shinikizo kutoka kwa serikali pia zilichangia kufutiliwa mbali kwa mkutano mkubwa wa maombi kundi hilo lilipanga kufanya jana katika Kaunti ya Murang’a.

Viongozi wa Kieleweke waliohojiwa na ‘Taifa Jumapili’ walisema mbinu hizi zinalenga kuwadhibiti na kuwanyamazisha wale wa mrengo wa Tangatanga ambao wamesemekana kumdharau Rais ilhali ndiye “aliwadhamini kupata nafasi za uongozi.”

Baadhi ya wanaolengwa ni Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a), Mbunge Mwakilishi wa kaunti hiyo Sabina Chege, Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa, miongoni mwa wengine.

Bw Kang’ata ambaye ni kiranja wa wengi na mwanachama wa kamati ya ushirikishi katika Seneti, Bi Chege ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya naye Bw Ichung’wa anaongoza Kamati kuhusu Bajeti yenye wajibu mkubwa katika utayarishaji wa bajeti ya kitaifa.

Mbunge wa Gatanga, Bw Nduati Ngugi jana aliiambia Taifa Jumapili kwamba, viongozi hao wanapaswa kuwa mabalozi wa Rais katika kamati hiyo lakini wamekaidi ushauri wake wa kukomesha kampeni ila waelekeze juhudi zao katika utekelezaji wa Agenda Nne Kuu za Serikali.

“Nafasi ambazo wabunge hao wanashikilia ni muhimu zaidi katika mpango wa Rais wa kufanikisha utekelezaji wa ajenda zake za maendeleo lakini wamekuwa wakiendesha kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 ili kufaidi mkuu wao. Nafasi zao zinapasa kuchukuliwa na wabunge ambao wataendesha ajenda za Rais Kenyatta,” akasema.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba, mikutano ya kupanga kuondolewa kwa wabunge hao waasi kutoka kamati za bunge ilianza kufanyika Alhamisi wiki iliyopita.

Baadhi ya wabunge wa mrengo wa Tangatanga walioomba wasitajwe walisema, wanafahamu kuhusu mipango ya kuwafurushwa kutoka kamati za bunge.

“Tutageuza suala hili lionekane kama vita dhidi ya Murang’a. Tutasimama kidete na kuelezea wananchi wetu jinsi licha ya wao kuunga mkono Jomo Kenyatta mnamo 1963 na Mwai Kibaki, bado mwana wetu Kenneth Matiba alisalitiwa. Wacha wajaribu tena,” Mbunge mmoja akasema.

Kwa upande wake, Bi Chege alisema hana habari kuhusu mipango hiyo lakini akashikilia kuwa hofu yake kuu ingekuwa “kuondolewa mamlakani na watu wa Murang’a.”

“Cheo cha mwenyekiti wa kamati ya bunge huwa ni cha kujitolea tu. Hatuogopeshwi na vitisho na propaganda kutoka kwa baadhi ya wanachama ambao wanajifanya kuwa katibu wa kibinafsi wa Rais Kenyatta,” akasema.

Seneta Kang’ata alisema hataki kuzungumzia suala hilo kwa sababu yeye ni rafiki wa karibu wa Rais.

“Rais ni rafiki yangu na hajaniambia nimpigie debe mtu yeyote bali niunge mkono ajenda yake ambayo nimekuwa nikivumisha kila wakati,” akasema.