TAHARIRI: Tangazo kuhusu karo kuzifikia shule Jumatatu lisiwe ahadi tupu

TAHARIRI: Tangazo kuhusu karo kuzifikia shule Jumatatu lisiwe ahadi tupu

Na MHARIRI

HUKU shule zikitarajiwa kufunguliwa kwa muhula wa tatu mnamo Januari 3, 2022, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha jana Jumatatu alisema kuwa serikali itatoa mgao wake kwa kila mwanafunzi kufikia siku hiyo.

Kila mwaka, serikali hutoa Sh22,244 kwa mwanafunzi wa shule ya upili huku pia ikimpa kila mwanafunzi wa shule ya msingi Sh1,420.

Wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosomea shule spesheli nao hulipiwa Sh57,974 kila mwaka.

Kando na karo, Profesa Magoha alitangaza kuwa mitihani ya Kitaifa ya KCPE na KCSE itakuwa tayari kufikia Februari kabla ya watahiniwa kuifanya mnamo Machi.

Pia aliongeza kuwa vitabu vyote vya kiada vya kusaidia kutekeleza Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC) vitawasilishwa katika shule mbalimbali mwanzo wa mwaka.

Kauli ya Profesa Magoha inaonyesha kuwa serikali imekamilisha maandalizi ya wanafunzi kurejea shuleni baada ya mapumziko ya siku 10 tangu na sasa kazi ni kwa walimu na wanafunzi, kila mmoja atekeleze wajibu wake darasani.

Kwanza, kutuma fedha mapema kwa shule kutawaondolea walimu wakuu shinikizo za kuwafukuza wanafunzi ambao hawajakamilisha karo.

Mwaka huu pekee kumekuwa na mihula minne na kila unapoanza muhula, wazazi wamekuwa wakilipa karo, hali ambayo imewaumiza zaidi ikizingatiwa kuwa wengi wao wanapitia wakati mgumu kiuchumi.

Hii ni licha ya kuwa baadhi ya wazazi walipoteza ajira kutokana na athari ya janga la virusi vya corona na sasa wanapitia wakati mgumu kujipanga na kupata fedha za kulipia karo.

Katika baadhi ya shule zilizoshuhudia mgomo, wanafunzi wametozwa fedha za ziada za kugharimia uharibifu wa mali ya shule, hali ambayo pia itawaumiza wazazi zaidi kwa kuwa watatakiwa kulipa fedha za ziada.

Ingawa hivyo, ni vyema walimu wakuu wasifukuze wanafunzi ambao watarejea shuleni bila karo na badala yake wawape wazazi muda zaidi wa kutafuta fedha kisha kukamilisha kiasi kilichosalia.

Si wazazi wote huwa wana tatizo la kifedha.

Baadhi bado wapo kwenye ajira na biashara zao zinafanya vizuri. Hawa hawafai kutumia sababu au mwanya wa serikali kulipa mgao wake kisha wao nao wachelewe kuwalipia watoto wao ilhali uwezo wanao.

Wazazi wajizuie kufuja pesa kwa anasa na sherehe zinazoendelea za Krismasi na mwaka mpya.

Itakuwa ni makosa makubwa kwa mwanafunzi kufukuzwa kwa kutolipa karo ilhali mzazi alitumia fedha zote kwenye sherehe.

Wazazi wawausie watoto wao waonyesha tabia nzuri wakirejea shuleni. Hii itazuia kutokea tena migomo na kuteketezwa kwa mabweni.

You can share this post!

NMS haijamaliza miradi ikisalia miezi 3 pekee

CHARLES WASONGA: Msimamizi mpya wa Mumias Sugar apaswa...

T L