Habari za Kitaifa

Tangazo la Raila kuhusu AUC laibua mzozo ODM


TANGAZO la kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa anapanga kuachana na siasa za humu nchini ili kutekeleza majukumu katika asasi kuu ya Umoja wa Afrika (AU) limechochea mvutano kuhusu urithi wa uongozi ndani ya ODM

Bw Odinga alitoa tangazo hilo kwenye kikao na wanahabari wiki jana jijini  Nairobi akiwa ameandamana na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Aliweka wazi kwamba sasa ataelekeza juhudi zake katika kampeni za kuwania cheo cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

“Kuanzia sasa sitajihusisha zaidi na siasa za Kenya kwani nitalenga zaidi kampeni katika mataifa yote barani Afrika. Hii ni awamu ya mpito kutoka kuzamia siasa za Kenya na kuingia katika siasa za bara la Afrika,” Bw Odinga akawaambia wanahabari katika afisi ya Bw Mudavadi.

“Nitaanza kuhudumia bara la Afrika nikichaguliwa na hiyo itakuwa Februari mwaka ujao,” akaongeza.

Gavana wa Siaya James Orengo, ambaye ni mwanasiasa mkongwe na mwana mapinduzi ni miongoni mwa wale ambao majina yao yametajwa kama wanaoweza kumrithi Bw Odinga.

Duru katika chama hicho zilisema kuwa Bw Orengo anaungwa mkono na magavana wenzake kutoka Nyanza na eneo la Magharibi.

Gavana wa Kisumu Profesa Peter Anyang’ Nyong’o ambaye anahudumu muhula wake wa mwisho pia anasema kuwa ni miongoni mwa wanaopigiwa upatu kurithi kiti cha Bw Odinga.

Idadi kubwa ya wafuasi wa ODM wanatoka Luo Nyanza hali inayowafanya wengine kuamini kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa kiongozi atakayechukua nafasi ya Bw Odinga atatoa eneo hilo.

Bw Orengo amekuwa mwaminifu kwa Bw Odinga tangu kifo cha babake Jaramogi Oginga Odinga.

Gavana huyo ambaye ni wakili maarufu anajivunia sifa kama mwanasiasa jasiri  ambaye amedumu katika siasa za upinzani kwa miaka.

Yeye na Bw Odinga walianza kutembea pamoja kisiasa mwishoni mwa miaka ya 80 na 90  wakati ambapo walikuwa miongoni mwa wanasiasa wachanga waliopigania ukombozi wa pili.

Bw Orengo ni miongoni mwa viongozi wakuu wa ODM ambao Bw Odinga aliwaacha nje alipojaza nafasi kuu chamani zilizoachwa wazi na wale walioteuliwa mawaziri.

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitaifa kuchukua mahala pa John Mbadi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.

Gavana wa Mombasa Abdullswamad Nassir, mwenzake wa Kisii Simba Arati na Seneta wa Godfrey Osotsi waliidhinishwa na Kamati Kuu ya ODM kuwa manaibu kiongozi wa chama.

Watatu hao walichukua nafasi iliyosalia wazi kufuatia kuteuliwa kwa Ali Hassan Joho na Wycliffe Oparanya kuwa mawaziri wa Madini na Ustawi wa Vyama vya Ushirika, mtawalia.

Mnamo Jumapili Bi Wanga aliambia Taifa Leo kwamba ni mapema kwa mjadala kuhusu ni nani atachukua wadhifa wa kiongozi wa chama kuanza.

Alisema wanaomezea mate kiti hicho wasubiri hadi Bw Odinga atakapotwaa cheo cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.