Michezo

Tanzania Ikitoka sare, itasare AFCON2023

January 24th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

WAWAKILISHI wa Afrika Mashariki, Tanzania, wanaingia katika mechi yao ya mwisho ya Kundi F wakiwa butu mno mbele ya lango.

Ni mara ya tatu kushiriki katika Shindano la Kandanda la Taifa Bingwa Barani Afrika (AFCON).

Taifa Stars watamenyana na The Leopards wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Jumatano Januari 24, 2024 saa tano usiku.

Ukiangalia matokeo ya Tanzania katika mechi ya kwanza dhidi ya Morocco, utadhani walienda kushiriki tu.

Lakini, licha ya kurambwa magoli matatu-nunge, walionyesha mchezo maridadi sana wakakosa makali katika thuluthi ya mwisho ya uga.

Kocha Hemedi Suleiman anafaa kurekebisha ubutu huu sababu huenda wakajitoma katika mkondo wa muondoano wakiweka mambo yao sawa.

Katika Kundi F, Morocco wanaongoza kwa alama 4, Zambia na DRC wana alama mbili mbili na Tanzania wakiwa wa mwisho kwa alama moja.

Vijana wa Hemedi wanakutana na timu ambayo wametoshana nguvu katika mapambano manane yaliyopita.

Katika migaragazano hiyo, Tanzania na DRC wameshinda mechi tatu-tatu wakitoka sare mara mbili.

Ila mgongano wa hivi punde zaidi uliwafaidi The Leopards waliponyuka Taifa Stars tatu bila 2021 wakiwania upenyu kushiriki Kombe la Dunia.

Tangu kushiriki AFCON mara ya kwanza 2019, Tanzania imetoka sare mbili na kupigwa mara sita.

Ila wana motisha ya hali ya juu katika makala ya 2023 wakihitajiwa kushinda DRC ili kuweka hai matumaini ya kuendelea kukaa nchini Ivory Coast.

Endapo watashinda mechi ya Jumatano usiku nao Morocco wapiku Zambia ama kutoka sare, wataingia raundi ya 16.

Na ni bayana kuwa kutoka sare dhidi ya DRC kutakuwa tiketi yao ya kurudi Dar es Salaam.

Mashabiki wanasubiri mchezo wao wa kuburudisha na pengine kurejelewa kwa tukio la bao maridadi la fowadi Simon Msuva alipocheka na nyavu baada ya kupokezwa pasi nyerezi na staa wao Mbwana Samatta dhidi ya Zambia Jumapili iliyopita.

Morocco wanahitaji angalau sare ili wafuzu mkono wa 16 wakitoana kijasho na Zambia wenye ‘lazima’ ya kushinda ili wafuzu.

Mchambuzi wa Kandanda Peter Pinchez Mwaura anaambia Taifa Leo kuwa Tanzania wanajiandaa kurudi nyumbani akidokeza hawatakuwa na nafasi dhidi ya DRC.

“Ili kocha Hemedi awahi nafasi nzuri ya kushinda DRC, itabidi awaweke wachezaji wenye haiba kama Samatta kwenye benchi na kuwatumia baadaye katika mchuano kama wachezaji wa akiba,” alisema akisifu DRC kwa kubadilisha wachezaji na kuwa na timu mpya kila makala.

Hata hivyo, Bw Mwaura anashauri kuwa timu ambayo itacheza bila presha ndiyo itaibuka mshindi katika kundi la F.